Mtu mmoja amewahi kusema kwamba sehemu pekee ambapo mafanikio yanapatikana bila ya kuweka kazi ni kwenye kamusi. Kuna neno hulijui, unafungua kamusi na jibu unalipata mara moja, hakuna haja ya kusumbuka. Vitu vingine vyote vinahitaji kazi kabla hujapata matokeo unayotaka.

Kwenye zama tunazoishi sasa, kumekuja kitu kingine cha kushangaza. Kitu hicho ni umaarufu bila ya kazi.

Kipindi cha nyuma umaarufu ulikuwa unakuja kutokana na kazi ambayo mtu amefanya na kuweza kuleta matokeo makubwa na ya tofauti kabisa. Watu walijulikana kwa kile walichofanya, ambacho kinakuwa na manufaa kwa wengine.

Lakini siku hizi watu wamegundua njia ya kupata umaarufu bila ya kuweka kazi yoyote. Na njia hiyo ni kupitia mitandao ya kijamii. Kwa sababu ni rahisi kwa yeyote kuwafikia wengi kupitia mitandao hii, na kwa sababu kwa asili sisi binadamu tunapenda habari hasi na umbeya kuliko habari chanya, wapo ambao wameweza kulitumia hilo vizuri. Wanakuwa wasambazaji wa habari hasi na mambo ya umbeya ili kuwanasa wengi na hilo linawapa umaarufu.

Kuna kitu wanaita ‘kiki’, kwamba mtu anafanya kosa la makusudi kabisa ili azungumziwe na wengine, lakini akijifanya kama hajafanya kosa hilo, au ameonewa. Hii ni njia nyingine ambayo watu wamekuwa wanaitumia kupata umaarufu bila ya kazi.

Rafiki, umaarufu unaopatikana bila ya kazi huwa haudumu, unapotea haraka kama ulivyokuja na mara nyingi unamfanya mtu kuwa mtumwa, kwamba ili watu waendelee kukuongelea au kukufuatilia inabidi uendelee kuwasisimua zaidi na zaidi.

Wakati umaarufu unaotokana na kazi huwa ni wa kudumu, ukishafanya kitu mara moja watu wataendelea kukumbuka miaka na miaka

Weka kazi rafiki yangu, siyo kwa sababu ya umaarufu, bali kwa sababu ndiyo kitu sahihi kwako. Kama umaarufu utakuja basi upokee, lakini usiwe ndiyo msukumo wa wewe kufanya kitu. Ukishasukumwa na umaarufu, kitakachotokea ni kufanya mambo yasiyo sahihi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha