Kinachotuzuia sisi binadamu tusiweze kuruka angani kama jamii ya ndege ni kwa sababu hatuna njia ya kuishinda nguvu ya mvutano ya dunia. Mabawa ya ndege yanawawezesha kutengeneza nguvu inayokinzana na nguvu ya mvutano wa dunia na hivyo kuweza kuruka angani.
Lakini kwa kuwa sisi binadamu tumepewa kitu ambacho wanyama wengine hawana, uwezo wa kufikiri na kuyabadili mazingira, tumeweza kutengeneza vyombo vya usafiri ambavyo vinaruka angani. Kupitia kujifunza kwa viumbe wanauruka angani, tumeweza kuweka mfumo wao kwenye vyombo vya usafiri na vimeweza kuruka angani.
Sasa nguvu hii ya mvutano haipo tu kwenye dunia na anga, bali ipo kwenye kila eneo la maisha yetu.
Tabia zetu zina nguvu ya mvutano, kila tunachofanya kwenye maisha yetu, kinawezeshwa au kuzuiwa na tabia zetu. Tukishajijengea tabia fulani, hiyo inakuwa ndiyo nguvu ya mvutano kwenye maisha yetu, kila mara tutavutwa kwenye tabia hiyo. Hivyo ili kuvuka nguvu hii ya mvutano, lazima tuweze kutengeneza nguvu mbadala inayokinzana nayo na itakayoishinda ili kuondoka kwenye tabia hiyo.
Jamii na tamaduni zetu ni nguvu ya mvutano pia, vinatufanya tuendelee kufanya yale tuliyozoea kufanya, ambayo pia ndiyo kila mtu anayafanya. Tunapojaribu kufanya kitu cha tofauti nguvu hii inatuzuia na kuturudisha kwenye kile tulichozoea. Ili kuvuka nguvu hii ya mvutano, lazima utengeneze nguvu mbadala itakayokinzana nayo na kukuwezesha wewe kuvuka mazoea hayo.
Rafiki, nimekushirikisha leo kuhusu nguvu ya mvutano, maana ni nguvu isiyoonekana lakini ina nguvu kubwa sana. Na nguvu hii ipo kwenye kila eneo la maisha yetu. Hivyo unapotaka kubadili eneo lolote la maisha yako, kwanza ijue nguvu ya mvutano iliyopo kwenye eneo hilo na jinsi utakavyoweza kuivuka.
Wale waliojaribu kuruka kama ndege kabla ya kujua nguvu ya mvutano ya dunia waliishia kuumia vibaya. Kadhalika wale wanaojaribu kubadili maisha yao kabla ya kujua nguvu ya mvutano kwenye eneo wanalotaka kubadili huwa wanajikuta wamerudi kwenye mazoea yao baada ya muda mfupi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Shukrani kocha, hili nimekuwa naliona sana kwangu. Kuna wakati natamani kujijengea tabia Fulani kwenye maisha yangu labda tabia ya kuamka asubuhi mwanzoni naweza kufanya hivyo baadae najikuta nimerudi kwenye mazoea. Kweli kuna nguvu ya uvutano kwenye kila eneo la maisha yangu.
LikeLike
Hili nalishuhudia kwangu kocha, asante nakwenda kulifanyia kazi.
LikeLike