Mbuni anapojikuta kwenye hali ya hatari ambayo hawezi kuikabili, huwa anafanya kitu kimoja, anafukia kichwa chake kwenye mchanga ili asiione hatari hiyo. Lakini hatari hiyo haiondoki, na mwili wake wote unabaki wazi kwenye hatari hiyo.
Unaweza kumcheka mbuni, na kusema kiumbe huyu hana akili yoyote ya kujua kwamba hatari haitaondoka kwa kujificha usiione? Lakini nikutahadharishe kabla hujaendelea, kwamba humcheki mbuni, bali unajicheka wewe mwenyewe.
Sisi binadamu, mara nyingi tumekuwa na tabia hizi za mbuni, tabia za kujificha ili tusiyaone matatizo yanayotukabili, tukiamini yatapotea yenyewe au kwa kutoyaona hayatakuwa na madhara kwetu. Huku ni kujidanganya na kuyapa matatizo nafasi ya kukua zaidi na madhara yake kuwa makubwa.
Na kama kwa namna yoyote ile unataka kubisha kwamba wewe huna tabia ya kuficha kichwa chako kwenye mchanga unapokutana na matatizo, tafakari matatizo mbalimbali ambayo umekuwa unakutana nayo kwenye maisha, ni hatua zipi ambazo umekuwa unachukua?
Kwa wengi, hatua ya kwanza ni kukataa, kuona tatizo hilo haliwezi kuwa lao au kujiuliza kwa nini kila wakati wao.
Kinachofuata ni kutafuta mtu wa kumlaumu kwa tatizo hilo, kutafuta nani amesababisha au kupelekea tatizo hilo kutokea, na huwa hakosekani mtu wa kulaumiwa kwa tatizo lolote lile.
Baadaye mtu hutafuta njia ya kulikwepa tatizo kwa muda mfupi, na hapa ndipo jamii imetuandalia kila njia ya kuweza kutoroka matatizo au hali fulani tunazopitia. Simu zetu za mkononi ndiyo kituo cha kwanza, kuzurura mitandaoni, hasa ya kijamii na kufuatilia mambo ya wengine ni njia ambayo wengi wamekuwa wanayakimbia matatizo yao.
Kuangalia tv na njia nyingine za kupoteza muda pia hutumika kama njia ya kutoroka. Wengine hutumia kufanya manunuzi au kula kama njia ya kuwaondoa kwenye fikra za tatizo fulani wanalopitia.
Halafu sasa kuna matumizi ya vitu ambavyo vimeandaliwa kwa ajili ya kupumbaza akili zetu kwa muda. Vilevi vimekuja kwa kazi hiyo, pombe, sigara, madawa ya kulevya na vilevi vingine, vimekuwa vinapumbaza akili kwa muda mfupi, na mtu kuyasahau matatizo yake, lakini baada ya muda uhalisia unarudi.
Rafiki yangu mpendwa, ujumbe ambao nataka kukupa leo ni huu; hiyo tabia yako ya kukimbia matatizo yanayokukabili ndiyo inayafanya maisha yako kuwa magumu.
Kila unapojikuta kwenye matatizo makubwa unayojiambia huwezi kuyatatua, jua kuna wakati matatizo hayo yalikuwa madogo na ukawa unayakimbia, ila yenyewe hayakukimbia, yaliendelea kukua mpaka sasa yamekomaa na yanakuzidi nguvu.
Hakuna mtu anayeamka siku moja na kujikuta yuko kwenye madeni makubwa, madeni hayo huwa yanatengenezwa kidogo kidogo, kwa mtu kushindwa kukabiliana na ukweli wa tatizo kwamba kipato chake ni kidogo kuliko matumizi yake. Na yeye badala ya kukazana kukuza kipato, anakimbilia kukopa, hivyo analiacha tatizo likue.
Hakuna mtu anayeamka siku moja na kukuta mahusiano yake yapo kwenye hali mbaya, bali ni kitu ambacho kinatengenezwa kila siku, kwa kushindwa kutatua changamoto ndogo ndogo za mahusiano.
Rafiki, kila tatizo kubwa linalokukabili leo, jua kuna wakati lilikuwa dogo sana, lakini wewe ukalipuuza au ukajaribu kulikimbia, lakini halikuondoka, liliendelea kukua na sasa linakukabili kwa nguvu kubwa zaidi.
Ukiwaona watoto wa nyoka nyumbani kwako hutawaacha ukisema hawana shida, badala yake utawaua kwa sababu unajua wakiwa watoto hawana shida, ila wakikua na kuwa nyoka kamili, shida yao ni kubwa sana.
Kadhalika ndivyo ilivyo kwa matatizo unayokabiliana nayo kwenye maisha, usidharau tatizo lolote, hata liwe dogo kiasi gani. Chukua hatua sahihi ya kukabiliana na kila tatizo unalokutana nalo, pale tu unapogundua kuna tatizo, usiendelee kusubiri kwa kujificha au kujisumbua na njia ambazo jamii imekuandalia.
Kila siku jiulize ni kitu gani hakipo sawa kwenye maisha yako, ni eneo lipi la maisha yako ambalo huridhiki nalo na kisha chukua hatua sahihi kwa majibu utakayoyapata.
Usijaribu kwa namna yoyote ile kukimbia tatizo lolote lile, kuwa jasiri na kabiliana na kila tatizo kama linavyotokea. Na kila unapojikuta kwenye njia maarufu za kuyatoroka matatizo, jiulize ni tatizo gani unalojaribu kukimbia kwenye maisha yako. Mfano unapojikuta unaperuzi mitandao ya kijamii kwenye muda ambao ulipanga kufanya kazi, jiulize ni kitu gani unajaribu kukikimbia, maana kuperuzi mitandao muwa wa kazi, ni kiashiria kuna kitu unajaribu kukikimbia, labda ni ugumu wa kazi au kukosa ujasiri wa kumkabili mtu mwingine kuhusiana na kazi hiyo.
SOMA; Hatua Nne Za Kuizuia Simu Janja Yako Isikuzidi Wewe Ujanja.
Nimalize ujumbe huu wa leo kwa ukweli ambao unapaswa kuujua kuhusu matatizo na changamoto mbalimbali kwenye maisha.
- Maisha yako ni mwendelezo wa matatizo na changamoto, hakuna wakati ambao hautakuwa na tatizo au changamoto.
- Suluhisho la tatizo moja, huwa ni chanzo cha tatizo jingine. Hivyo kwa kila tatizo unalotatua, jiulize ni tatizo gani jingine ambalo umetengeneza, na tatua hilo pia, ambapo utazalisha tatizo jingine na kuendelea.
- Unapotatua tatizo au changamoto moja, inayokuja inakuwa kubwa kuliko ile ya awali, hivyo kutatua matatizo ni kukua zaidi.
- Usipotatua tatizo au changamoto unaendelea kubaki kwenye ngazi hiyo hiyo, yaani kama maisha ni shule, basi matatizo ni mtihani wa kutoka darasa moja kwenda darasa jingine. Ukifaulu unapanda darasa, usipofaulu unarudia darasa.
- Kuyakimbia matatizo hakuyapunguzi, badala yake kunayakuza zaidi, kila unapogundua kuna changamoto au tatizo, likabili kwa wakati huo.
- Pale unapochukua hatua sahihi kwenye tatizo au changamoto lakini haikutatuka, basi una njia ya mwisho ya kutumia, ambayo ni kuuachia muda ufanye kazi yake. Muda ni mwalimu na tiba nzuri, lakini usikimbie tatizo kwa kuuachia muda, badala yake fanya sehemu yako, halafu uachie muda sehemu yake.
Usifukie kichwa chako kwenye mchanga pale unapokutana na matatizo au changamoto, badala yake kuwa imara na pata ujasiri wa kuyakabili matatizo na changamoto hizo na utaweza kuzitatua.
Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.
Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania