Ukiangalia dunia, unaweza kujikuta una maswali mengi sana.
Ukiangalia maji ya bahari, utashangaa jinsi ambavyo mawimbi yanatengenezwa, jinsi kubwa na kujaa kunavyotokea. Unaweza kujiuliza hii bahari ina shida gani? Kwa nini isingekuwa tu tulivu muda wote?
Ukiangalia ardhi, nako pia unaweza kuwa na maswali mengi. Kuna maeneo yana milima na mengine yako tambarare, huku mengine yakiwa mabonde. Unaweza kujiuliza kwa nini ardhi yote isilingane, kwa nini milima na mabonde?
Ukiuangalia mwaka, ndiyo unaweza kushangaa kabisa, kuna misimu mbalimbali ndani ya mwaka mmoja, kama kiangazi, masika, kipupwe na vuli. Kulingana na shughuli zako, unaweza kupendelea msimu fulani kuliko misimu mingine, na unaweza kujiuliza kwa nini mwaka mzima usiwe msimu unaotaka wewe.
Kitu muhimu sana tunachopaswa kujua ni kwamba asili inaendesha mambo yake kwa mipango yake, haiangalii sisi tunataka nini, bali inaangalia kipi sahihi kwa dunia na maisha kuendelea kuwepo. Kama bahari ingekuwa tulivu tu, kuna viumbe hawatakuwa na maisha. Kama ardhi ingekuwa milima au mabonde pekee, kuna maisha yangeshindikana. Na kama msimu ungekuwa masika tu au kiangazi tu, kuna maisha yangefikia ukingoni.
Kitu kingine muhimu cha kujifunza ni kujiandaa kukabiliana na hali tofauti kwenye maisha. Siyo kila wakati mambo yatakwenda kama ulivyopanga, hivyo unapaswa kuwa na maandalizi ya kukabiliana na hali tofauti na ile uliyozoea.
Bahati haina shida, ardhi haina shida, misimu haina shida na wala dunia haina shida, bali mwenye shida ni wewe kama utashindwa kuendana na vitu hivyo vizuri na kuweza kuvitumia vyema kupata unachotaka. Jifunze kuitumia asili kama ilivyo, kupata kile unachotaka, badala ya kusubiri asili iwe kama unavyotaka wewe ndiyo upate unachotaka.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante kocha ukweli Asili inafanya mambo kwa utaratibu Wake,mfano mdogo tu,tarehe mbili nikiwa naendelea na utaratibu wangu wa kawaida nikifurahia kumaliza mwezi na kuanza mwezi mwingine,pamp yangu ya Kisima ikaharibika, ndipo niliendelea kujua ni nini maana ya mfuko wa dharula, maana nimetumia laki tatu kuirudisha katika utaratibu wake wa kawaida, muhimu kama familia hatukusumbuka na maji bali Mimi akili na fikra ndio ziliumia kufanya kazi.
LikeLike
Vizuri Sana Beatus kwa hilo uliloweza kujifunza kwa pampu kuharibika.
Usingekuwa na dharura ungejikuta unaingia kwenye madeni ambayo yangekutesa.
LikeLike
Asante sana kocha kwa somo zuri,hutuwezi pingana na asili kwani ndio maisha halisia.
LikeLike
Asante sana kocha somo hili bora kabisa. Kwa kweli asili haijali yeyote bali inaendelea kujiendesha kwa utaratibu wake.
LikeLike