Unajichelewesha sana pale unapotaka kupatia kwa mara ya kwanza.

Yaani unataka uanze biashara yako ya kwanza na hiyo iwe na mafanikio makubwa.

Au kazi yako ya kwanza iwe ndiyo kazi inayokufikisha kwenye mafanikio makubwa.

Unajidanganya.

Hakuna mtu yeyote ambaye amewahi kupatia au kupata kila alichokuwa anataka kwa kufanya kitu mara ya kwanza.

Bali watu wote wamepata kile walichokuwa wanataka baada ya kujaribu na kushindwa kwenye vitu vingi na tofauti tofauti.

Hivyo kuwa huru, jiondoe kwenye kifungo cha kutaka kupatia mara ya kwanza.

Badala yake kuwa kwenye mtazamo wa kujaribu vitu vingi uwezavyo, jifunze, boresha au badili na songa mbele.

Angalia kila kitu unachofurahia leo, hakikuanza kama kilivyo.

Gari la kwanza halikuwa bora kama magari unayoona leo, kompyuta ya kwanza ilikuwa kubwa inayojaa kwenye chumba kikubwa. Simu ya kwanza haikuwa kama simu uliyonayo leo.

Maisha ni kuanzia pale ulipo, kupiga hatua moja na kisha kuboresha hatua hiyo kadiri unavyokwenda kwa kupiga hatua nyingine nyingi zaidi.

Kila unapotaka kuahirisha kitu kwa sababu hujawa tayari jikumbushe hili, hakuna aliyewahi kupatia kwa mara ya kwanza, hivyo anzia hapo ulipo, fanya na utaendelea kuboresha kadiri unavyokwenda.

Kumbuka sheria ya mwendo, kilichopo kwenye mwendo kinaendelea na mwendo na kilicho simama kinaendelea kusimama. Wewe anzisha mwendo, ili uendelee na mwendo na mwendo huo utakufikisha kwenye kile unachotaka, baada ya kupita kwenye vile usivyotaka.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha