“Seek to learn constantly while you live; do not wait in the faith that old age by itself will bring wisdom.” —SOLON
Unakula chakula kila siku,
Hukubali siku ipite hujaulisha mwili wako,
Na kwa siku ambayo huna namna ya kulata chakula, utapambana kwa kila namna kuhakikisha unakipata.
Hukuna siku umewahi kujiambia hujala siku nzima kwa sababu umekosa muda, kwa sababu uko bize.
Hata kama umetingwa kiasi gani, unapofika wakati wa kulisha mwili, kila kitu kinasimama na unaulisha kwanza mwili wako.
Lakini sasa inapokuja kwenye kulisha akili yako, yaani kujifunza, sababu huwa haziishi.
Ni rahisi sana kupata sababu za kutokulisha akili yako kuliko kutenga muda na kuilisha.
Utajiambia huna muda, uko bize na mengine mengi.
Unakubali siku ipite hujasoma au kujifunza chochote, halafu siku nyingine tena, na nyingine tena, ukija kustuka mwaka umeisha na hakuna ulichojifunza.
Unapokuwa tayari kulisha mwili na siyo akili, je unamaanisha tumbo lako ni muhimu kuliko akili yako?
Watu wengi wanaogopa utapiamlo wa mwili kwa sababu unaonekana, huku wakiwa na utapiamlo mkubwa wa akili kwa kuwa hawawezi kuuona haraka.
Usikubali kuendelea na zoezi hilo la kutengeneza utapiamlo wa akili yako.
Akili yako ni muhimu sana, kwa sababu bila akili imara, mwili utaumia.
Hivyo hakikisha kila siku unajifunza kitu kipya, kitu kinachokufanya uwe bora zaidi ya ulivyokuwa na uweze kupiga hatua zaidi.
Hii ni kila siku, usijiruhusu kujiambia kwamba huna muda au uko bize.
Unapofika wakati wa kulisha akili yako, kuwa makini kama unapofika wakati wa kula,
Acha kila kitu na lisha akili yako.
Njia rahisi ya kufanya hivyo ni kutembea na kitabu popote unapokuwa na kila unapopata muda, fungua na soma kurasa chache.
Kwa kiwango cha chini kabisa, soma kurasa 10 kwa siku, usishuke chini ya hapo.
Soma kurasa 4 unapoamka au kabla/wakati unapata kifungua kinywa.
Soma kurasa 3 mchana, kabla/wakati/baada ya chakula cha mchana.
Soma kurasa 3 usiku, baada ya kula au kabla ya kulala.
Jijengee utaratibu huo kila siku na utaona manufaa yake pale akili yako inapoanza kuwa na afya bora.
Kama hujifunzi kila siku, ni bora ujiambie ukweli,
Acha kujifanganya kwamba huna muda,
Wewe jiambie tu ukweli kwamba HUTAKI KUJIFUNZA
Kwa sababu unapotaka kitu, unapokuwa na nia ya kweli, hukosi njia ya kukifanya.
Jifunze kila siku, maarifa hayaji kama ajali, na pia umri hauleti hekims wenyewe, hekima unaipata kupitia kujifunza na kuweka kwenye matendo yale unayojifunza.
Unakwenda kujifunza nini leo?
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania
Nakushkru Sana kocha kwa tafakari hii ya leo,sitaendelea kutengeneza utapiamlo tena, muhimu nitaendelea kuzidisha zaidi ya pale nilipokuwa, nimefanya hili kwenye mazoezi maambo ni mazuri,sasa kwa hili la kuongeza maarifa naenda kuongeza nguvu zaidi.ubarikiwe sana kocha wetu
LikeLike