Mambo mengi yanayokukasirisha kwenye maisha, hayana maana kabisa. Hivyo hasira unazojipa ni kupoteza muda na nguvu zako kwa hisia ambazo hazina manufaa.

Chukua mfano unapita njiani, ukakutana na mbwa ambaye baada ya kukuona akaanza kubweka. Je utamkasirikia mbwa huyo? Utasema kwa nini akuone wewe na aanze kubweka?

Kama utafanya hivyo, utawashangaza wengi, kwamba umkasirikie mbwa kwa kuwa mbwa? Maana mbwa huwa wanabweka, sasa cha kukukasirisha wewe ni nini?

Sasa tuje kwa watu, kile ambacho watu wanakifanya, ndivyo walivyo, siyo kusudi wala bahati mbaya, wanapofanya kitu, wanatuonesha wao ni watu wa aina gani.

Hivyo kumkasirikia mtu kwa sababu ya kitu alichofanya, hata kama kimekuumiza siyo sahihi, haina manufaa kwako. Chukua mfano wa mtu uliyemuamini na akakusaliti, kukuangusha au kukuumiza. Utakasirishwa sana na hilo na kuona amefanya makusudi.

Ninachotaka nikuambie ni kimoja, kama mtu huyo siyo mgonjwa wa akili, basi jua hajafanya makusudi, amefanya hivyo kwa sababu ndivyo alivyo. Kukasirisha hakutambadilisha na hakutabadili kilichofanyika. Badala yake shukuru kwamba umemjua mtu huyo kwa undani na usirudie makosa ya mwanzo.

Huna sababu ya kukasirishwa na jambo lolote analofanya au kusema mtu, kwa sababu kukasirika kwako hakutakuwa na msaada wowote. Mtu anasema na kufanya kile kilicho ndani yake, kama mbwa anavyobweka kwa sababu ni mbwa. Kumkasirikia mtu kwa alichofanya au kusema, haitakuwa na tofauti na kumkasirikia mbwa kwa kubweka.

Mara nyingi watu wanahitaji huruma yako, maana wengine hawapendi kuwa vile wanavyokuwa, ila yale waliyopitia kwenye maisha yao yamewajenga hivyo. Huenda na wewe ungepitia waliyopitia, ungekuwa kama walivyo wao.

Hivyo mtu anapofanya kitu kinachokukwamisha, kukuangusha au kukuumiza, usikasirike. Badala yake chagua kama mtu huyo anahitaji huruma yako na umsaidie kuwa bora zaidi au unahitaji kumfuta kabisa kwenye maisha yako kwa sababu juhudi zako za kumsaidia hazitazaa matunda.

Usipoteze nguvu zako kwa hisia ambazo hazina matokeo yoyote yatakayokusaidia. Peleka nguvu hizo kufanya mambo yenye tija.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha