Pale unapoongea au kuwasiliana na mtu mwingine kwa njia yoyote ile, akasema kitu kisha jibu likaja haraka kwenye akili yako, kuwa makini kabla hujatoa jibu hilo.

Maana majibu mengi ambayo huwa yanakuja haraka huwa siyo sahihi, ni majibu ambayo yanakuwa hayajaangalia swala zima bali yamesukumwa na kile kilichoshika hisia zako kwenye swala hilo.

Hivyo jifunze kujipa muda kabla ya kutoa majibu yako kwenye jambo lolote lile.

Jinsi ya kufanya hivyo;

Kwa maongezi ya kuongea ana kwa ana au kuongea kwa simu, kwanza jifunze kutokumkatisha mtu akiwa anaongea, mwache mtu aongee mpaka amalize. Kisha akimaliza kuongea, epuka kukimbilia kumjibu, badala yake hesabu mpaka tano kabla hujatoa majibu yako. Ikiwezekana hesabu zaidi kama haitachelewesha, lakini hakikisha hukimbilii kutoa majibu yanayokuja kwenye akili yako.

Kwenye mawasiliano yanayohusisha ujumbe wa kuandika, iwe ni ujumbe wa simu, barua pepe au kupitia mitandao, kabla hujajibu ujumbe uliotumiwa, rudia tena kuusoma, na mara hii soma ujumbe na zuia hisia zako zisiingie. Ukisharudia kusoma, andika majibu yako, lakini usiyatume. Yaache kwa muda angalau saa moja au hata siku nzima kulingana na uzito wa jambo, kisha soma tena na ndipo utume. Kama ni mawasiliano ya kujibizana hapo kwa hapo, tumia mbinu kama ya maongezi.

Kwa kujichelewesha kujibu na kurudia kusoma majibu yako kabla hujayatoa, utaona jinsi ambavyo majibu yaliyokuja kwenye akili yako kwa haraka yalivyokuwa ya hisia na ambayo yataleta tafsiri mbaya kwa mtu mwingine. Pia utaona majibu uliyokuwa nayo mwanzo hukuwa umeelewa vyema upande wa pili.

Kingine muhimu, jambo lolote linaloibua hisia kali ndani yako, iwe ni hisia chanya kama ya furaha au hasi kama ya hasira, chelewa zaidi kujibu. Hakikisha unajipa muda mpaka hisia hizo zitulie, kisha kurudi kwenye swala husika kabla ya kutoa majibu yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha