Kwenye moja ya mahojiano yake na watu mbalimbali waliofanikiwa, mwandishi James Altucher alikuwa anamhoji mchekeshaji na mfanyabiashara Bryon Allen ambaye alianza ujasiriamali akiwa na umri wa miaka 12.

Alipokutana na wachekeshaji maarufu, aliona hicho ndiyo kitu anachotaka kufanya kwenye maisha yake na hapo alijipa kauli ya kishujaa na iliyompa msukumo mkubwa wa kufanyia kazi ndoto yake.

Alisema; “Hiki ndiyo kitu nitakachokwenda kukifanya kwa maisha yangu yote, sitajali iwapo nitalipwa au la. Nipo tayari kufanya bure, nipo tayari kulala nje na nipo tayari kula nyasi, ila hiki ndiyo nitakachofanya maisha yangu yote.”

Habari njema ni kwamba Bryon hakulala nje, wala hakula nyasi, bali alikuwa bilionea, kwa sababu kauli hiyo ilimfanya aache kuhangaika na mambo mengine na kuweka nguvu zake kwenye kile alichochagua.

Swali kwako rafiki yangu, ni kitu gani ambacho umekichagua kufanya maisha yako yote, ni kipi unaweza kutumia kauli hiyo ya kishujaa?

Shirikisha kwenye maoni hapo chini, kile ambacho umechagua kukifanya maisha yako yote, na kisha weka nguvu zako na umakini wako kwenye kitu hicho.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha