Kwenye kitabu cha GIVE AND TAKE kilichoandikwa na Adam Grant, mwandishi ametushirikisha aina tatu za watu inapokuja kwenye ushirikiano.

Aina ya kwanza ni wachukuaji (takers), hawa ni wale wanaochukua zaidi ya wanavyotoa ili kujinufaisha wao wenyewe zaidi. Hawa hujali maslahi yao kabla ya maslahi ya wengine. Hupata wanachotaka lakini baadaye sifa zao huharibika na kupoteza walichopata.

Aina ya pili ni wabadilishanaji (matchers), hawa ni wale ambao wanaamini kwenye nipe nikupe, wanatoa kadiri ya wanavyopokea. Hawa hujali sana usawa na hawakubali kutoa zaidi wala kupokea zaidi. Mafanikio ya watu hawa huwa siyo makubwa kwa sababu ya ukomo wanaojiwekea kwenye watu wanaoshirikiana nao.

Aina ya tatu ni watoaji (givers), hawa ni wale ambao wanatoa zaidi ya wanavyopokea, huwa wanatoa zaidi bila kujali wanapokea nini. Hawa huweka maslahi ya wengine mbele kama wanavyoweka maslahi yao. Wanaweza kuchelewa kupata mafanikio, lakini huyapata kwa uhakika na hudumu nayo.

Katika makundi haya matatu, mwandishi ametuonesha kwa mifano na tafiti kwamba kama tunataka kupata mafanikio makubwa na tutakayodumu nayo, basi tunapaswa kuwa watoaji.

Lakini maswali ambayo wengi wanajiuliza ni wanawezaje kuwa watoaji? Vipi wengine hawatajinufaisha kupitia utoaji?

Mwandishi ameyajibu maswali hayo kwenye kitabu.

Kwenye kuwa mtoaji, mwandishi ameshirikisha misingi minne ya utoaji ambayo ni MTANDAO, USHIRIKIANO, KUTATHMINI na KUSHAWISHI.

Kuhusu wengine kujinufaisha na utoaji wako mwandishi ametushirikisha jinsi ya kukabiliana na changamoto kubwa tatu za utoaji ambazo ni kuchoshwa na utoaji, kuepuka wanaotaka kujinufaisha na utoaji wako na mazoea yaliyopo kwenye mazingira au hali fulani zinazokusukuma uwe ambavyo hutaki kuwa.

Na mwisho, mwandishi ametupa hatua tunazoweza kuanza kuchukua kwenye utoaji na tukawanufaisha wengine pamoja na kujinufaisha sisi wenyewe.

Kuna fursa nyingi kwa watoaji kufanikiwa.

Hofu kubwa iliyopo kwa watoaji, hasa kwenye kazi na biashara ni kuzidiwa na wengine, kuwanufaisha wengine huku wao wakibaki bila kitu.

Hii siyo kweli, kazi nyingi za sasa zinahitaji ushirikiano wa watu kama timu na siyo ushujaa wa mtu mmoja. Inapokuja kwenye timu, anayefanikiwa siyo shujaa anayejiangalia yeye, bali yule anayetoa thamani kubwa zaidi kwenye timu, na hapo ndipo watoaji wanapokuwa na fursa kubwa ya kufanikiwa.

Unachopaswa kujua ni kwamba hakuna juhudi inayopotea, unaweza kufanya jambo la kutoa sasa na usipate majibu, lakini baadaye likakupa fursa nzuri na kubwa zaidi.

Muhimu ni kuzingatia misingi ya utoaji tuliyojifunza na kuziepuka changamoto zinazowarudisha wengi nyuma kwenye utoaji.

Watoaji waliofanikiwa huwa wanaishi kwa msingi huu; kadiri wanavyotoa zaidi, ndivyo wanavyofanikiwa zaidi. Lakini pia wamekuwa wakipima mafanikio yao siyo kwa wanachopata, bali wanachotoa na jinsi kinavyowanufaisha wengine. Jenga maisha yako kwenye msingi huu na utakuwa na mafanikio makubwa.

Maana tofauti za mafanikio.

Kwa wachukuaji (takers) mafanikio ni kupata zaidi ya wengine, wanajipima kufanikiwa pale wanapokuwa wamewazidi wengine.

Kwa wabadilishanaji (matchers) mafanikio ni usawa, kupata kadiri ya unavyotoa, wanajipima mafanikio yao kwa kile wanachopata ukilinganisha na walichotoa.

Kwa watoaji (givers) mafanikio ni kutoa zaidi kwa wengine, wanajipima kufanikiwa pale utoaji wao unapokuwa na manufaa kwa wengine.

Kama tunataka kubadili mazingira ya kazi au biashara, basi tunapaswa kuchochea maana ya mafanikio ambayo ni bora, maana waliyonayo watoaji.

Utamaduni wa kila eneo una nguvu ya kuwajenga na kuwabadili watu. Mtu anapoingia kwenye mazingira ambayo ni ya ushindani, anakuwa mshindani, anapoingia kwenye mazingira ya ushirikiano, anaonesha ushirikiano.

Ni wajibu wetu kukuza aina ya mafanikio inayopimwa kwa utoaji na hii itawasukuma wengi kuwa watoaji.

Hata motisha mbalimbali tunaotoa kwa wengine, unabeba ujumbe ndani yake, kwamba watu wananufaika kwa kufanyaje. Tukitoa motisha pale watu wanapokuwa watoaji, hiyo ndiyo tabia inayojengeka.

Mafanikio bila kuwaangusha wengine.

Inapokuja kwenye mafanikio, wengi wanaamini kwamba ili wafanikiwe basi wanapaswa kuwashusha wengine. Ili wewe uwe juu, lazima wengine wawe chini. Kile unachohitaji ili kufanikiwa, lazima ukichukue kwa wengine.

Huu ni mtazamo uliopitwa na wakati, mtazamo unaowafanya watu kuwa wachukuaji na mafanikio wanayopata kuanguka.

Kupitia utoaji, tumeona unaweza kujenga mafanikio yako huku pia ukiwawezesha wengine nao kufanikiwa. Unafanikiwa wewe na wengine pia na hilo linayafanya mafanikio yako kudumu, kwa sababu hakuna anayekuwa ameumia kwa kufanikiwa kwako.

Watoaji wanaofanikiwa, huwa wanafika kwenye kilele cha mafanikio bila kumwangusha yeyote. Badala ya kuangalia uhaba, wao hutengeneza utele, badala ya kuona mkate ni mdogo hivyo wapate wao na kuwanyima wengine, wamekuwa wanatengeneza mkate mkubwa zaidi.

Kwa wachukuaji, mafanikio ni pata potea (zero-sum), lakini kwa watoaji, mafanikio ni kupata kwa pamoja (positive-sum).

Anza kutoa unachofurahia.

Kama umejigundua kwamba wewe siyo mtoaji kwa asili, unaweza kubadilika na kuwa mtoaji kwa kuanza kutoa kile ambacho unafurahia kutoa na hakikugharimu wewe. Na toa kitu hicho kwa wale wenye uhitaji nacho na kinayafanya maisha yao kuwa bora zaidi.

Kwa kufanya hivi, utaanza kuona jinsi utoaji wako, wa kitu kidogo unavyobadili maisha ya wengine na hapo utapata hamasa ya kuendelea kutoa zaidi.

Angalia ni kitu gani unapendelea zaidi wewe na ambazo kwako siyo kigumu kufanya, kisha angalia wale waliokwama kwenye kile kilicho rahisi kwako na wasaidie kujikwamua.

Unaweza kuanza na kitu kidogo, lakini utakavyoona wengine wananufaika, utasukumwa kuendelea kutoa zaidi. Utakapoanza kupata matunda mazuri kwenye utoaji wako, utasukumwa kutoa zaidi, siyo kwa sababu unategemea kupata, ila kwa sababu unasukumwa kutoa, na hilo litapelekea upate zaidi.

Hatua za kuchukua ili uwe mtoaji.

Tumejifunza mengi kupitia kitabu hiki, kuanzia manufaa ya utoaji, misingi ya utoaji na kuepuka changamoto za utoaji. Ili kuyafanya maisha yako kuwa bora na kufanikiwa zaidi kwenye utoaji, mwandishi ametushirikisha hatua mbalimbali za kuchukua. Zisome hapa na chagua zile unazoweza kuzitekeleza.

1. Jipime ili kujua kama wewe ni mchukuaji, mtoaji au mbadilishanaji, mwandishi ameandaa maswali yatakayokupa mrejesho sahihi, yanapatikana kwenye tovuti hii; www.giveandtake.com ingia na ujifanyie tathmini.

2. Tengeneza mtandao wa watoaji ambapo kila mtu anakuwa tayari kutoa kile kilicho ndani ya uwezo wake kwa wengine, bila kuangalia anapata nini.

3. Wasaidie watu kufanya kazi inayoendana na uwezo ulio ndani yao. Kama wewe ni mwajiri au kiongozi, wajue watu wako vizuri na wasaidie kuweza kutumia uwezo wao kwenye kazi wanazofanya au kufanya kazi zinazoendana na uwezo wao.

4. Anzisha mashine ya upendo, hii ni njia ya kuwasaidia watoaji kutambulika na kusifiwa, kitu kitakachowasukuma wengine kua watoaji pia.

5. Tumia kanuni ya MSAADA WA DAKIKA 5, kama mtu anakuomba umsaidie kitu na kitakuchukua chini ya dakika tano, msaidie. Pia mara kwa mara toa kwa wengine kile kinachotumia chini ya dakika 5, mfano kuwatambulisha watu wawili ambao wanaweza kushirikiana au kujibu ushauri ambao mtu amekuomba.

6. Jifunze na tumia mawasiliano yasiyo ya nguvu kwa kuwa msikilizaji badala ya mwongeaji, mwomba ushauri badala ya kujisifu na kuwa tayari kujifunza badala ya kuona unajua kila kitu.

7. Jiunge na jumuia ya watoaji. Mitandaoni na hata kwenye maisha ya kawaida, kuna jumuia mbalimbali za watu ambao wako tayari kusaidiana kwa kila hali. Tafuta jumuia ya aina hiyo ujiunge nayo na uingie kwa mtazamo wa kuwa mtoaji na siyo mchukuaji tu.

8. Fanya zoezi la utoaji, kila siku jisukume kutoa kitu kwa ajili ya wengine, hata kiwe kidogo kiasi gani. Ukifanya hivyo kwa mwezi mzima bila kuacha hata siku moja, utajijenga kuwa mtoaji.

9. Toa mchango wa fedha kwa wenye uhitaji wa kuanzisha miradi mbalimbali. Kuna watu wana mipango ya kuanzisha miradi mbalimbali lakini wamekwama kifedha. Unapokutana na watu wa aina hii, wape mchango wa fedha ili waweze kukamilisha ndoto zao.

10. Omba msaada kwa wengine. Pale unapokwama, usione ni vibaya kuomba wengine wakusaidie, usione kama unawapa mzigo, badala yake unapata nafasi ya kuwajua watoaji ambao unaweza kushirikiana nao zaidi.

Alhamisi ya utoaji (Giving Thursday).

Kutokana na maarifa haya mazuri tuliyoyapata kwenye kitabu cha GIVE AND TAKE, tunakwenda kuwa na huduma ya Alhamisi ya utoaji (Giving Thursday) kwenye KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa huduma hii, kila siku ya alhamisi inakuwa siku maalumu ya utoaji kwenye kundi la wasap la KISIMA CHA MAARIFA.

Kwenye siku hiyo, kila mwanachama anashirikisha kitu kinachoweza kuwa na manufaa kwa wengine, iwe ni uzoefu fulani alioupata, fursa aliyoiona au kitu alichojifunza au kukutana nacho na kinachoweza kuwanufaisha wengine pia.

Pia kwa mwenye swali au aliyekwama na anataka kupata ushauri, anauliza moja kwa moja kwenye kundi na wanachama wengine wanamshauri na kumpa majibu yanayoweza kumsaidia kutoka pale alipokwama. Majibu yanaweza kuwa ya ushauri, hatua za kuchukua au kumpa mtu connection itakayomsaidia kutoka alipokwama.

Msingi mkuu kwenye huduma hii ya Alhamisi ya utoaji ni kushirikishana MAARIFA, RASILIMALI na CONNECTION za kuwezeshana kupiga hatua zaidi. MAARIFA yanajumuisha ujuzi na uzoefu alionao mtu. RASILIMALI zinajumuisha vitu alivyonavyo mtu na vinavyoweza kuwa msaada kwa mwingine. CONNECTION inahusisha mtandao alionao mtu, anaoweza kuutumia kuwasaidia wengine.

Huduma hii inaanza mara moja na itakuwa kila siku ya alhamisi kwa siku nzima. Kama bado hujawa mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA, karibu sasa uwe mwanachama ili uwanufaishe wengine, huku pia ukinufaika. Kupata maelezo ya kuwa mwanachama tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253.

Karibu kwenye Soma Vitabu App.

Rafiki, nikukumbushe kama bado hujawa na app yetu mpya ya SOMA VITABU basi uchukue hatua sasa kuweka app hiyo kwenye simu au tablet yako.

Kuna zawadi mbalimbali nitazitoa kwa upande wa vitabu kwenye app hiyo, hakikisha unakuwa na app ili usivikose vitabu vizuri.

Kuweka app, fungua kiungo hiki; www.bit.ly/somavitabuapp

Kama unakwama kwenye kuweka au kutumia app, angalia maelezo kwenye video kwa kufungua kiungo hiki; https://bit.ly/somavitabufull au kwa kusoma hapa; www.kisimachamaarifa.co.tz/somavitabuapp

Karibu sana rafiki yangu tuendelee kuwa pamoja kwenye safari hii ya kushirikishana maarifa sahihi ili tuweze kupata mafanikio makubwa. Kama hujawa mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA chukua hatua sasa na kama hujawa na SOMA VITABU APP pia chukua hatua sasa.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania