Unaweza kujipa sababu nyingi kwa nini umenunua kitu, kwamba unakipenda, kwamba unakithamini lakini zote hizo ni sababu za juu juu tu.

Sababu halisi kwa nini umenunua kitu, ni kwa sababu thamani unayoipata ni kubwa kuliko gharama unazolipia. Yaani thamani yake ni kubwa kuliko bei.

Chukua mfano, unataka kununua gari, ukaenda kwa wauzaji wa magari, umeshachagua ni aina gani ya gari umepata. Kwa gari ile ile, yenye sifa zile zile na ubora ule ule, kwa wauzaji wawili uliotembelea, kuna mmoja bei yake iko juu mwingine bei yake iko chini. Utanunua kwa yupi?

Jibu liko wazi, kama hakuna tofauti nyingine yoyote, utanunua kwa anayeuza bei ya chini, kwa sababu msukumo wako wa kufanya manunuzi ni kupata thamani kubwa kuliko bei unayolipia.

Kitu kikubwa cha kujifunza hapa ni kwamba, wateja wako wanatumia kigezo hicho hicho katika kufanya maamuzi ya kile unachowauzia. Hawatanunua mpaka wahakikishe kwamba thamani wanayoipata ni kubwa kuliko fedha wanayolipa.

Hivyo una kazi mbili kubwa, ya kwanza ni kuhakikisha unaweka thamani kweli kwenye kile unachouza au kufanya, kwa namna ambayo mtu mwingine hawezi kuweka. Hata kama unauza bidhaa au huduma inayouzwa na wengine, wewe weka thamani ya ziada, ambayo itafanya uwe tofauti.

Kitu cha pili ni kuhakikisha mteja anajua thamani kubwa iliyopo, ambayo ni kubwa kuliko bei anayotakiwa kulipia. Mteja hatajua mwenyewe na kwa zama hizi za usumbufu, hana muda wa kujisumbua kujua, ni wajibu wako kuhakikisha mteja anaielewa thamani halisi, kwa kumweleza manufaa yote atakayoyapata kwa kununua kile unachouza, huku ukisisitiza yale ambayo hawezi kuyapata kwa wengine.

Sisi binadamu huwa tunafanya maamuzi yetu kwa ubinafsi, kuangalia maslahi yetu kwanza na siyo kwa huruma ya yule ambaye anataka tufanye kitu fulani. Hivyo kwa kazi au biashara unayofanya, acha kutegemea huruma na gusa maslahi ya watu. Acha kuwataka watu wanunue kwa kukuonea huruma na anza kuwaonesha thamani kubwa watakayoipata na hapo watakimbilia kununua wenyewe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha