Wahamasishaji, washauri, viongozi wa dini na watu wengine ambao watu wanawaamini na kuwatumia kama mwongozo kwao katika kufanya maamuzi mbalimbali, wamekuwa wanaonekana ni watu wenye uwezo fulani wa juu kuliko wengine.

Kuonesha hilo, wale wenye mafanikio makubwa kwenye kuwashawishi wengi wafuate kile wanachowaambia, wamepewa jina la guru, ikiwa ni neno la Kihindi linalomaanisha mwalimu wa kiroho.

Lakini kwa sasa neno guru limekuwa linatumika kwa yeyote anayeonekana kuwa na ubobezi wa hali ya juu kwenye maarifa, ushawishi na kuwafanya wengine wawaamini na kufanyia kazi kile wanachoshauri au kuelekeza.

Maguru hawa wamejijengea imani kubwa, kiasi kwamba wafuasi wao wanaamini hawawezi kufanya bila ya kuongozwa na maguru hao.

Hivi ndivyo hata dini nyingi zimeweza kushikilia watu wengi, kwa kuwaaminisha kwamba nje ya dini au imani hizo, wao si chochote.

Hivyo pia ndivyo viongozi wabinafsi na wanaotaka kukaa kwenye madaraka kwa muda mrefu wanavyofanya, kuwaaminisha watu kwamba bila ya wao, hawawezi kuwa na maisha mazuri.

Leo nakwenda kukupa uhuru wako, na utaamua mwenyewe unautumiaje, au kama utaendelea kurudi kwa hao maguru ni juu yako.

Hakuna tofuati kati yako wewe na guru yeyote unayemuamini na kumfuata. Uwezo wa kufanya makubwa tayari uko ndani yako, na unaweza kufanya makubwa kama anavyofanya guru unayemkubali kwenye kila eneo la maisha yako.

Ndani yako tayari unacho kila unachohitaji ili uweze kufanya makubwa, ni wewe kujua kile kilicho ndani yako na kuanza kukitumia.

Kitu pekee ambacho guru anakijua na wewe hukijui ni hiki; guru anajua humhitaji yeye ili ufanikiwe, wanajua una uwezo wa kufanikiwa bila hata ya uwepo wao. Lakini kwa kuwa wanataka kunufaika na wewe, hawakuambii hivyo, wanahakikisha unaamini bila wao huwezi, ili uendelee kuwa chini yao, ufanikiwe kwa kilicho ndani yako lakini sifa uwape wao.

Sikuambii uache kuamini watu wengine, waamini utakavyo, sisemi uache kuwafuata wengine, wafuate. Ninachokuambia hapa ni hiki, usifikiri nguvu ya wewe kufanya makubwa na kufanikiwa iko kwa mtu mwingine yeyote. Nguvu hiyo iko ndani yako. Wengine wanaweza kuichochea, lakini lazima ianze kuwaka ndani yako.

Kwa kujua hili, unakuwa huru kuchagua kuishi maisha unayoyataka wewe na siyo yale unayopangiwa na yeyote, hata awe guru kiasi gani. Kwa sababu unajua maisha yako ni yako, na nguvu zote ziko ndani yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha