Kuna watu wamekuwa wanachagua wao wenyewe kufa, kwa kukikaribisha kifo kabla hata ya muda wake.

Na hawafanyi chochote ambacho ni hatari ili kujiua, bali wanafanya kila ambacho wanategemewa kufanya na matokeo yake kuwa kifo cha mapema.

Njia ambayo imekuwa inatumiwa na wengi kuchagua kufa bila ya kujua ni kustaafu. Pale mtu anapochagua kupumzika na asifanye tena kazi, mwili wake unajua hauna tena mahitaji na hapo unakaribisha kifo.

Tafiti nyingi zimekuwa zinaonesha watu wengi hufa ndani ya miaka mitano tangu kustaafu kazi zao. Pamoja na sababu nyingine zinazoweza kuchangia, lakini kubwa zaidi ni mwili kuona hauna tena kazi.

Unapokuwa unafanya kazi, roho yako inajua bado unahitajika na hivyo inausukuma mwili ili uendelee kuwa imara kupambana na kazi. Unapostaafu kazi, roho inajua kazi imeisha na hivyo haiusukumi mwili, kitu kinachopelekea mwili kudhoofu, inakuwa rahisi kukaribisha magonjwa na hauwezi kupambana nayo.

Hivyo moja ya njia za kuepuka kufa haraka ni kuhakikisha hustaafu kazi au biashara unayoifanya, kuendelea kuifanya maisha yako yote.

Lakini siyo kila aina ya kazi au biashara itakupa nafasi ya kuishi muda mrefu, bali ile ambayo unapenda kuifanya ambayo inatokana na kusudi la maisha yako.

Kama kazi au biashara unayoifanya huipendi na inakupa msongo, kuendelea kuifanya ni kuchagua kuyafupisha maisha yako. Lakini kama ni kitu unachopenda kufanya, ambacho upo tayari kukifanya kwa muda mrefu bila kuchoka, basi unapaswa kuendelea kukifanya kila siku unapokuwa hai.

Ndiyo maana ni muhimu sana ujue kusudi la maisha yako na uchague kitu cha kufanya kukamilisha kusudi hilo, ambacho utakifanya maisha yako yote.

Wengi hupuuza hili, hasa wanapokuwa na kazi au biashara zinazowalipa sana japo hawazipendi. Wakijiambia wanafanya kazi au biashara hizo kwa muda tu, wapate uhuru wa kifedha kisha wastaafu na kupumzika. Wanafanya kweli, wanazipata fedha, ila wanapostaafu na kupumzika, maisha yao nayo yanaporomoka haraka.

Hata kama utaazimika kustaafu kazi au biashara unayoifanya, kwa sababu zozote zile, hakikisha una kitu chako unachoweza kuendelea kukifanya siku zote za maisha yako, ambacho hakuna namna utalazimika kustaafu, mpaka uchague mwenyewe.

Kama bado hujawa na kitu cha aina hii, anza kukifanyia kazi mapema. Anza kujiangalia mwenyewe, jisikilize nini kinatoka ndani yako, jaribu vitu mbalimbali na utakutana na kile kinachokuvutia zaidi na unachokitumia kutoa mchango kwa wengine, kisha kitengeneze kwa namna utaweza kukifanya kila siku. Na ukiwa na njia ya kulipwa kukifanya, basi inakuwa bora zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha