Kama kuna kitu ambacho mwaka 2020 umetufundisha basi ni uwezo mdogo ambao sisi binadamu tunao kwenye kutabiri mambo yanayoweza kutokea.

Dunia imekumbwa na mshangao mkubwa mwaka huu 2020 baada ya kujikuta ikifungwa kwa sababu ya kirusi ambacho hakuna aliyedhani kwamba kingeleta madhara makubwa kama ilivyotegemewa.

Hakuna mtabiri hata mmoja ambaye aliweza kuona kirusi hiki kikija mwaka 2020, wengi walikuwa wanatabiri kutakuja kirusi, lakini hawakujua lini na wala ukubwa wa madhara yake hawakuweza kutabiri.

Lakini sisi binadamu, ni kama tuna laana ya kukimbilia kutabiri na kuamini utabiri wetu japo kuwa siyo sahihi. Mara baada ya COVID – 19 kutangazwa kuwa janga la kidunia, tulikimbilia tena kutabiri.

Watu mbalimbali, wenye taaluma zinazohusu afya na magonjwa, uchumi na mambo ya kijamii walianza tena kutabiri. Safari hii ilikuwa ni utabiri kwenye madhara ya kiafya na kiuchumi, idadi ya watu watakaofariki na jinsi uchumi utatikisika. Wapo walioenda mbali zaidi na kusema huu ndiyo mwisho wa dunia.

Lakini sehemu kubwa ya yaliyotabiriwa hayajatokea, idadi kubwa ya vifo iliyotegemewa haijatokea na japo madhara ya kiuchumi yanaendelea kuwa makubwa, siyo kwa kiasi ambacho ilikuwa inatabiriwa.

Pamoja na kila utabiri kwenda tofauti na ilivyotabiriwa, bado watu wanaendelea kutabiri na bado tunaendelea kuamini kwenye utabiri huo. Lakini kitu pekee tunachoambulia kwenye tabiri hizi ni kujiumiza tu, maana mengi hayatokei.

Utabiri ni uongo.

Nassim Nicholas Taleb ni mwanahisabati na mwandishi ambaye amekuwa akiwapinga sana wale wanaotabiri. Kwenye vitabu vyake mbalimbali amekuwa anaonesha jinsi ambavyo watabiri hawana mchango wowote, kwa sababu wanayotabiri na yanayotokea ni vitu tofauti kabisa.

Kwenye kitabu chake cha Fooled By Randomness, ameonesha jinsi ambavyo watu wanadanganywa na matukio yanayotokea kwa bahati tu, kisha kuyatumia kutabiri yajayo na kuishia kushindwa vibaya.

Kwenye kitabu chake kingine kinachoitwa Black Swan anaeleza jinsi baadhi ya matukio ambayo hayatabiriki yanavyotokea, halafu yakishatokea watu wanajifanya kuyaelezea kama vile ilikuwa lazima yatokee, au yalikuwa yanatabirika.

Cha kuchekesha sasa, baada ya COVID – 19 kutokea, kila mtu aliona ni Black Swan, lakini yeye Taleb alikataa na kusema COVID haina sifa za Black Swan. Unaweza kusoma chambuzi za vitabu hivyo viwili ambazo zipo kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA, kwa kufungua; https://www.t.me/somavitabutanzania

Taleb na wengine wamekuwa wanaona jinsi utabiri ulivyo uongo. Na iko hivyo kwa sababu historia huwa inatengenezwa na matukio ya kushtukiza, huku utabiri ukifanywa kwa matukio yaliyopo sasa.

Hapo ndipo utabiri unapotudanganya, kwa sababu kila anayetabiri, anaangalia kilichopo sasa, kisha kuona kitaendaje kwa siku zijazo. Ndiyo maana mwanzo wakati watu wengi wanakufa kwa COVID watabiri waliona hali itaendelea kukua, lakini hawakujua kuna vitu vingi visivyoonekana vinavyoweza kuathiri hali ya mambo.

Hivyo kama unataka kupangilia maisha yako vizuri, kama unataka kupiga hatua unazotaka, unapaswa kuwa makini sana na tabiri nyingi zinazofanywa.

Na uelewe hapa hatuzungumzii utabiri wa wale wanaobahatisha tu, kama watu wanaotoa utabiri wa unajibu na sayansi nyingine za aina hiyo. Bali hapa tunazungumzia utabiri unaofanywa na watu wenye utaalamu na ubobezi wa hali ya juu kwenye maeneo yao.

Kama ni afya basi tunazungumzia utabiri unaofanywa na wataalamu wa afya, ambao wametumia miaka yao yote kujifunza na kuelewa eneo hilo. Kama ni utabiri wa uchumi basi tunazungumzia wachumi ambao wamebobea kwenye eneo hilo.

Lakini pamoja na ujuzi, ubobezi na uzoefu mkubwa walionao kwenye maeneo yao, bado wataalamu hawa wanakosea kwenye utabiri wao, kwa sababu wanatabiri kwa kuanza na mambo yalivyo sasa.

Ni utabiri upi utakaokusaidia kwenye maisha yako?

Kama tulivyoona, utabiri wa wataalamu ni wa uongo na umekuwa na upotoshaji mkubwa, je unawezaje kupanga mambo yako na kuchukua hatua zitakazokuwezesha kufanikiwa zaidi?

Kuna aina moja tu ya utabiri unaopaswa kuufanya mwenyewe na kuuishi kila siku. Utabiri huo ni huu kwamba kuna mabadiliko yanakuja, kwamba kila unachofanya sasa, kitaondoka na kupotea kabisa, hivyo kila mara uwe na maandalizi sahihi ya kuweza kukabiliana na mabadiliko hayo.

Kama umeajiriwa, kila siku ishi kwa kufikiri kesho unaweza kuamka na ajira yako isiwepo, kisha jiulize maisha yako yataendaje?

Kama unafanya biashara, kila siku ishi na utabiri kwamba kesho biashara hiyo haitakuwepo kabisa, halafu ona maisha yako yataendaje katika hali hiyo.

Utabiri huu unakufanya uwe na njia mbadala za kukabiliana na maisha yako ili chochote kinachotokea, isiwe mshangao kwako, badala yake iwe ni kitu ulichotegemea na kinachofuata ni kuchukua hatua ulizokuwa umepanga.

Kwa kuishi kwa namna hii, hutatikiswa na chochote, hutababaishwa na utabiri wa wengine na maisha yako yataendelea kwenda vizuri bila ya kutegemea nini kinaendelea.

Zawadi ya kukuwezesha kutabiri vyema.

Rafiki yangu mpendwa, unajua ninavyokupenda wewe, na jinsi kazi zangu zote zinavyolenga kukuwezesha wewe kupiga hatua, kwa sababu hiyo ndiyo njia pekee ya mimi kupiga hatua pia.

Miaka mingi iliyopita, niliandika kitabu kinachoitwa JINSI YA KUNUFAIKA NA MABADILIKO YANAYOTOKEA, kwenye kitabu hicho nimeeleza jinsi mabadiliko yanavyokuja wakati hatutajiandaa na namna tatu watu wanakabiliana nayo.

Leo nakupa wewe zawadi ya kitabu hiki, upate nafasi ya kukisoma, ili ujiandae na mabadiliko mengi na makubwa yanayokuja. Kama COVID ilikukuta kwa mshangao, basi usikubali tena mabadiliko yoyote yakushangaze.

Kitabu kitakufundisha jinsi ya kunufaika na mabadiliko, kwa kuyawahi, kwa wewe kubadilika kabla mabadiliko hayajafika, na yanapofika, wewe unakuwa mbele ya wengine.

Kitabu hiki huwa kinauzwa kwa bei ya elfu tano (5,000/=) lakini siku hii ya leo, tarehe 30/09/2020 nimechagua nikupe kitabu hiki. Ndiyo, nakupa tu, ukisome na uchukue hatua sahihi.

Kwa siku ya leo tu, tarehe 30/09/2020 utakipata kitabu kwa kuchangia tsh elfu moja tu (1,000/=) hii ni ada ya kukamilisha muamala ili kitabu uweze kukipata, ndiyo maana nakuambia nimekupa kama zawadi kwako rafiki yangu.

Kitabu kinapatikana kwenye APP ya SOMA VITABU na malipo yanafanyika ndani ya APP, hivyo usitume fedha, wewe ingia kwenye app kwa kufungua; http://bit.ly/somavitabuapp kisha nenda kwenye kitabu, kifungue, kisha nunua, chagua mtandao wako wa simu, ingiza namba ya siri na kamilisha muamala. Baada ya hapo omba uthibitisho kwa kuingiza namna uliyotumia kulipia na hapo utapata kitabu hiki kizuri nilichokupa zawadi.

Nikutakie kila la kheri kwenye kupata maarifa sahihi, yatakayokuwezesha kuwa mbele ya mabadiliko ili usibabaishwe na watabiri wanaowayumbisha wengi. Pata zawadi yako leo hii, maana ni ya siku moja tu. Na muhimu zaidi, ipate zawadi ndani ya APP ya soma vitabu.

Kama unapata changamoto kwenye kupakua na kutumia app, soma maelekezo na kuangalia video kwa kufungua hapa; https://amkamtanzania.com/somavitabuapp

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania