Unahangaika na mambo mengi ambayo hayana mchango wowote kukufikisha kule unakotaka kwenda.
Kila siku unapata mawazo ya kuanza na kujaribu vitu vipya, ambavyo unaviona vitakuwa bora zaidi.
Lakini ambacho hufikirii kabla hujaanza kitu kipya ni kwamba muda na nguvu zako vina ukomo. Kwa siku una saa 24 tu na haziongezeki, kila siku unaianza ukiwa na kiwango fulani cha nguvu na kadiri unavyofanya vitu nguvu hizo zinapungua.
Hivyo kwa kila kitu kipya unachokubali kuanza kufanya, kuna kitu cha zamani ambacho inabidi uache au upunguze kukifanya. Sasa unapokuwa mtu wa kujaribu vitu vipya kila wakati, hupati nafasi ya kufanyia kazi vile ambavyo ni muhimu kwako.
Kulinda muda na nguvu zako, anza kusema hapana kwa mambo yote mapya ambayo unashawishika kufanya lakini hayachangii kufika kule unakotaka kufika. Utapata mawazo mengi na kuona ni ya kibunifu, lakini kwanza angalia yana mchango kiasi gani kwako kufika kule unakotaka kufika.
Wakati mwingine kitu kipya unachotaka kufanya kinaweza kuwa kinachangia kufika unakotaka, lakini mchango wake ni mdogo na inapunguza muda wa wewe kufanya kile ambacho ni kikuu zaidi.
Mfano kama unataka kuwa mwandishi bora, kazi kubwa kwako ni kuandika, mengine yote ni ya ziada. Baada ya kuandika, kazi nyingine kubwa ni kutafuta wasomaji wa kazi zako. Sasa wengi wamekuwa wanakimbilia kwenye njia za kutafuta wasomaji, mfano mitandao ya kijamii na nyinginezo, lakini wanasahau kazi ya msingi ambayo ni kuandika.
Hivyo hapo lazima uwe makini, unaweza kupata wazo zuri la kuwafikia wasomaji wengi, labda kutumia muda zaidi kwenye mitandao ya kijamii kujadiliana na wale unaotaka wawe wasomaji, lakini muda huo inabidi uupunguze kwenye kuandika na hata kusoma. Hivyo hata kama utapata wasomaji, hutakaa nao kwa muda kwa sababu huna kilicho bora kwao.
Ni bora kuweka juhudi kwenye uandishi, ukatoa kazi iliyo bora, ukaipeleka kwa wachache ulionao, watakusaidia kuwafikia wengi zaidi.
Huo ni mfano mmoja kwenye uandishi, lakini unaweza kuangalia kwenye maeneo mengine na utaona hali inayofanana na hiyo. Mfano kwenye kazi za taaluma mbalimbali, watu husisitizwa sana umuhimu wa kujenga mtandao wao, wanaweka nguvu nyingi kwenye kujenga mtandao kuliko wanazoweka kwenye kufanya kazi bora.
Kwa chochote unachofanya, iwe ni kazi, biashara au huduma yoyote unayoitoa, jua lile jukumu la msingi kabisa unalopaswa kulifanya ili kufika unakotaka kufika, kisha lipe kipaumbele hilo. Kabla hujakubali kufanya jukumu jipya, angalia kwanza kunaathiri vipi ufanyaji wa jukumu hilo kuu. Kama inapunguza muda au nguvu unayoweka kwenye jukumu hilo kuu, usifanye.
Njia pekee ya kupata muda zaidi na kutumia nguvu zako kwa usahihi ni kusema hapana kwa chochote ambacho hakichangii wewe kufika kule unakotaka kufika. Na usiwe na huruma kwenye hili.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Nitalinda muda na nguvu zangu kwa kuyakataa mambo yote mapya yasiyo na mchango wowote wa kunifikisha kule ninapotaka kufika.
Asante sana kocha.
LikeLike
Safi sana.
LikeLike