Siku yako [leo] inatabiri hatma ya maisha ya kila siku na hili hutokea kadri unavyoitumia siku moja huenda ndivyo unavyozitumia siku nyingine.

Mwandishi Som Bathla ni mbobevu katika kushirikisha uzoefu wake ni kwa vipi mtu anavyoweza kuitumia siku moja kubadili maisha yake. Siku inapaswa kuongozwa na kutawaliwa na mtu vizuri ili izae maongozo mazuri ya kila siku ya maisha. Pia Som Bathla anashirikisha katika kitabu hiki juu ya mifumo mbalimbali ya ufikiri inayosaidia mtu aweze kutumia kutawala siku na kuyaumba maisha bora na imara kila siku.

Kila mtu anatamani kuona siku yake ikiwa bora na ajione akiwa na uwezo wa kutawala siku na kuumba hali anazozifurahia. Mwandishi anasema lazima uwe na vitu kama vitatu ili kuweza kuwa na siku zinazokuwa bora. Mosi uwe na mfumo mzuri wa fikara, uwezo wa kuchukua hatua na tatu uwe na mtizamo wa juu kuhusu vitu na maisha. Kwa pamoja haya mambo matatu ndio yaumbayo siku inayovutia na mtu kujiona ana utoshelevu mkubwa. Hili linaweza kuwa na matunda ambapo kila siku mtu anajiwekea lengo la kufanya katika udogo udogo wenye uendelevu. Huwezi kupata matokeo makubwa ikiwa unaanza na kuacha au unaanza na kuishia njiani.

Siku bora hunaambatana na siku inayoisha na alama ya uzalishaji wa kitu, mjengo wa nidhamu na kuweka fokasi. Utajisikia vibaya kama una shughuli zako iwe ni biashara inaisha hujapata mteja au hujafanya mauzo. Siku kama hii humfanya mtu ajisikie vibaya na kuona siku yake ina mikosi. Amka kila siku kwa kunia kuzalisha kitu iwe ni faida katika biashara, kuongeza wigo wa kutoa thamani au kugusa jamii kwa jambo la kuivusha jamii. Uzalishaji katika siku unachangiwa na watu ambao wana misingi ya nidhamu ya muda, pesa na kazi. Hili linaimarishwa na mtu au kampuni yenye kuweka fokasi katika jambo husika. Nidhamu na fokasi ni sura pacha au ni nyuso mbili za shilingi moja.

Fikara [kiwango cha uelewa kuhusu mambo/uzoefu/maarifa au imani fulani zitokanazo na makuzi au malezi fulani] zinaathiri sana namna utakavyoiendesha siku nayo ikakupa matokeo utakayo. Hii itoshe kusema ukianza vibaya katika mjengo wa fikara basi hutaweza kuidhibiti siku au kuitawala. Fikara ni mbegu inayooteshwa katika maisha yetu ya kila siku. Mbegu mbovu huzalisha matokeo mabovu na ndivyo fikara zinazokosa maarifa sahihi zinamwongoza mtu kushindwa kutawala siku yake. Mwandishi anashirikisha mifumo 5 mikubwa ambayo mtu yeyote anaweza kujifunza na kuitumia ili kupata uwezo wa kuongoza siku yake izalishe matokeo yanakufurahiwa.

Mfumo wa kwanza ni “Kufikiri kunakolenga kuja na majibu” Yeye anaita kwa kingereza “Solution Oriented Mindset”. Jamii zetu nyingi zimekuzwa katika kulalamika pasi kuwa na mapendekezo ya majibu au maoni ya kuboresha. Hili ndilo linalofanya watu wawe na siku zinazoisha hawajafanya jambo lolote lile lenye matokeo mazuri. Ili siku iwe bora lazima mtu ajifunze kugundua kuwa kwa kila changamoto inayokuja au matatizo ni fursa ya kupanua uwezo wa kufikiri na kubuni mambo. Isingekuwa changamoto au matatizo yaliyopo basi kusingekuwa na magunduzi au biashara duniani. Changamoto ni chakula cha akili na akili inayokosa changamoto hudumaa. Jifunze kutolalamika bali kufikiri na uje na mapendekezo au njia ya utatuzi wa jambo husika.

Mfumo wa pili ni “Kuifunza akili kuona kumbe inawezekana” Yeye anaita kwa kingereza “Possibility Thinking Mindset”. Watu huona mambo yanawezekana mpaka pale watu watakaojitokeza kubadili yaloonwa hayawezekani yanawezekana. Hili linatuamsha kuwa kumbe inawezekana kufanikiwa kama wengine walivyofanikiwa. Si wakati wa kungoja wengine wafanye ndipo tuone inawezekana ila ni mwaliko wa wote kuifunza akili kuona inawezekana. Akili ukiishawishi na kuiaminisha kuwa jambo fulani liwalo na liwe nitafanikiwa basi kweli hutoa nafasi ya mtu kupata au kuona uwezekano wa mambo kutokea. Msukumo huu unavyouweka katika maisha ya kila siku kuwa inawezekana ndivyo unavyopata msukumo mkubwa zaidi kuchukua hatua, kuthubutu, kujaribu na kufanikiwa.

Mfumo wa tatu ni “Kuifunza akili ione na kutambua vitu katika wakati uliopo” Yeye anaita ni “Consciousness Oriented Mindset”. Tunakosa fursa nyingi maishani na kusema mambo ni magumu kwa sababu hatujaifunza akili ione ama kutambua ni rasimali ngapi zimetunguka sasa. Kukosa kuona huku ndiko kunakofanya mtu mara baada ya kupata matatizo basi anapoteza kabisa matumaini kuwa ndivyo itakuwa hivyo siku zote. Ukiweka angalau dakika chache na kujifunza kuangalia wakati uliopo una nini au una kitu gani kiko katika uwezo wako ndivyo unajitengenezea nafasi ya kuwa na siku bora. Jifunze kuangalia ulipo una vitu gani vinavyoweza kukusaidia mbali na kufikiria jana au yajayo usoweza kuwa na udhibiti nayo.

Mfumo wa nne ni “Kuifunza akili ifikiri katika uharaka na kasi”, Yeye anaita ni Speed Loving Mindset). Dunia inakoelekea ni kufikia dunia inayoenda kasi kwa kila kitu na kwa uharaka. Magunduzi ya ndege za angani, simu, umeme yana mlengo mmoja wa kurahisisha utendaji wa vitu na vitu vifanyike kwa haraka. Hili linatoa tahadhari kubwa kwa kila mtu kuifunza akili iende na kasi hii ya mambo yaendavyo. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yanaendelea kufupisha kupatikana kwa vitu. Hili mwandishi anatualika tujifunze kuwa na akili ya upesi na uharaka katika kufanya vitu au kutumia nafasi. Muda unavyokimbia ndivyo wale ambao hawakimbii na kasi ya mambo watajikuta wakiaachwa nyuma.

Mfumo wa tano ni “kuifunza akili iwe ina uanafunzi maisha yote” Mwandishi anaita ni mfumo uitwao “Lifetime learning Mindset”. Dunia ya sasa inaenda kasi na mambo mengi yanabadilika na yanataka watu wajifunze kutokana na mabadiliko. Licha kuwa Dunia inabadilika katika mifumo na mambo bado watu wengi wakishajifunza kitu kimoja basi hawajitoi tena kuendelea kujifunza. Hili ni anguko ambalo hutokea katika biashara za watu ambao wanafikiri kukaa kwao katika biashara kwa muda mrefu basi hawastahili kujifunza mambo mapya. Inakadiriwa kuwa kila mwaka kuna ongezeko la maarifa mapya na katika miaka 2 hadi 3 maarifa ya mambo yalokuwepo yanakuwa yameanza kupitwa na wakati. Mtu asipojifunza au kuwa mwanafunzi wa kila siku wa maisha basi kuna changamoto ya kuona yupo sayari mpya na yeye ni mtu mgeni.

Huwezi pata matokeo pekee kwa kujua hii mifumo na usichukue hatua ya kufanya kitu. Kuna umuhimu mkubwa wa kutumia hii mifumo yote katika umoja kuleta matokeo bora katika siku moja na siku nyingine maishani. Chochote kile unachotaka kukianza na kiwe sehemu ya maisha basi kuna umuhimu wa kuandika au kuchagua mambo 3 ulojifunza kwa siku husika na kuendelea kuyafanya.

Mwandishi nampenda pale anaposema jipe nafasi kila siku ya kusherehekea ushindi mdogo mdogo unaopata. Hili lina uzito mkubwa mno kukupa hamasa ya kuendelea kufanya kitu tena na tena. Chukua mfano, ulijipa ahadi kuwa kila siku utakuwa unasoma kurasa 10 za kitabu. Basi ukiweza jipe hongera mwenyewe kila siku na hili ndivyo litakavyokupa msukumo wa kufanya jambo kwa kuitafuta hali ile ya uzuri wa furaha uloipata baada ya kufanya kitu fulani.

Kibaiolojia unapopata ushindi fulani wa jambo baada ya kulifanya na kujisikia vizuri ni matokeo ya kemikali kubwa ya furaha inaitwa “Dopamini”. Kemikali hii ni kemikali zawadi ambayo hutoka pale mtu anapofanya kitu na kujisikia hali ya raha au utoshelevu fulani. Kumbukumbu inayejengeka kutokana na matokeo ya hii kemikali ndio inayompa mtu awe na msukumo wa kurudia jambo tena na tena. Watu wanaofanikiwa huendelea kufanikiwa kwa kusukumwa na matokeo ya kemikali hii zawadi. Tengeneza ushindi wa hatua ndogo ndogo kila siku ili uendelee kuipata hii zawadi maishani mwako na uzidi kupata matokeo bora kila siku.

Siku kuendelea kuwa bora lazima uwe na mahusiano mazuri na watu wa karibu yako na wale wanaokuzunguka iwe kuanzia nyumbani, shuleni, ofisini na mitandaoni. Mahusiano yakiwa mabovu na wale wanaotuzunguka ni rahisi siku kuharibika na tukapoteza utawala wa siku zetu. Pesa haiwezi nunua mahusiano ila isipokuwa muda unaowekeza kujenga mahusiano. Mahusiano mazuri huimarisha siku iwe nzuri. Pata picha asubuhi umeamka na tayari umepata ugomvi na watu lazima kwa namna moja siku utaona imeanza vibaya. Mitaani wanasema leo siku ina ndege mbaya.

Mwandishi anasisitiza jambo muhimu la msingi sana lingine nalo ni “Chuki”. Anasema usiruhusu chuki itawale ndani yako maana itakuharibu wewe, wanaokuzunguka na siku yako. Msamaha ni uimara maishani na ndio unasaidia watu waendelee kuishi katika kupendana. Hisia hasi zote mbali na chuki, hasira, wivu zina nguvu kubwa ya kuibomoa siku na siku iwe mbaya.

Mwisho siku yako inapoisha ni muhimu kupata “Usingizi”. Usingizi mzuri ni matokeo ya jinsi ulivyoishi vizuri katika siku yako moja. Siku ikienda vizuri, umekaa vizuri na watu, umeongeza thamani, umeshinda jambo fulani, umepata fursa fulani ni wazi unapoenda kulala unapata kulala usingizi bora na wenye afya.

Matatizo mengi ya watu kukosa usingizi yanahusishwa na siku kwenda vibaya, kugombana na watu, siku imeisha hujafanya kitu, hofu, msongo wa mawazo na kadhalika. Siku iishapo vizuri huambatana na kujikuta ukiwa na msisimuko wa furaha, shukrani na kuona utoshelevu. Himizo kubwa la mwandishi ni kwenda kutawala siku zetu na kuumba yale ambayo tutafurahia kuyaona ianzapo siku na iishapo siku. Unapoweza kudhibiti siku yako moja ndivyo unavyoweza kutawala siku nyingine vizuri.

Dkt. Raymond Nusura Mgeni

raymondpoet@yahoo.com

+255 676 559 211.

[Kwa maswali, maoni, ushauri na mirejesho tumia mawasiliano hapo juu ]