Wale wanaofanya makubwa kwenye maisha yao siyo kwamba wana tofauti kubwa sana na wanaoshindwa kufanya makubwa. Bali wanajitambua zaidi kuliko wengine.

Na katika kujitambua kwao, wanazijua rasilimali muhimu za kulinda ili waweze kufanya makubwa. Hizo ni rasilimali ambazo zikipotea huwa zina madhara makubwa ya kumzuia mtu asipige hatua. Rasilimali hizi unapaswa kuzilinda kila siku, kwani mchango wake kwenye maisha yako unategemea na jinsi unavyozitumia kila siku.

Rasilimali ya kwanza ni umakini wa akili yako. Hii ni rasilimali inayokuwezesha kupangilia na kutekeleza majukumu yako ya kila siku. Usipoilinda rasilimali hii, wengine wataiteka na kuitumia kwa manufaa yao. Kwa sasa kila mtu anawinda umakini wako, hivyo unapaswa kuulinda sana kwa kuuweka kwenye mambo muhimu pekee.

Rasilimali ya pili ni nguvu ya mwili, hii ndiyo inayokuwezesha kukamilisha majukumu yako ya kila siku. Mwili unapokuwa na nguvu, unaweza kuchukua hatua muhimu kwenye maisha yako, usipokuwa na nguvu huwezi kufanya chochote. Usipolinda nguvu zako, zitapotea kwa kuhangaika na yasiyo muhimu na hapo utashindwa kufanya makubwa. Peleka nguvu zako kwenye yale muhimu pekee.

Rasilimali ya tatu utashi wako, hii inakuwezesha kufanya maamuzi sahihi kwenye maisha yako. Utashi ndiyo unakusaidia kuchagua kilicho sahihi pale unapokuwa njia panda au unapokuwa umekwama. Utashi wako hupungua pale unapotumika kufanya maamuzi yasiyo sahihi. Hivyo ulinde na kuutumia kwenye maamuzi muhimu pekee.

Rasilimali ya nne ni kipaji halisi ulichonacho, kile kinachotoka ndani yako kweli na siyo cha kuiga. Hiki ndiyo kina nguvu kubwa ya kukusukuma wewe kufanya yale ambayo hakuna mtu mwingine anayeweza kufanya. Kipaji kinakutofautisha na wengine, hivyo kilinde, maana wengi watakushawishi uachane nacho na kufanya yanayofanywa na wengine.

Rasilimali ya tano ni muda wako wa siku, hii ni rasilimali inayowezesha rasilimali hizo nyingine kufanya kazi. Bila muda huwezi kufanya chochote na muda wetu una ukomo huku mambo ya kufanya yakiwa mengi. Linda sana muda wako, ukishapotea haurudi na mambo mengi yanauwinda.

Ukizilinda vizuri rasilimali hizi tano, kwa kuzipangilia vizuri na kuhakikisha hazipotezwi kwa yasiyo muhimu, utaweza kufanya makubwa sana kwenye maisha yako bila ya kujali unaanzia wapi sasa.

Uzuri ni kwamba rasilimali hizi zipo ndani ya kila mtu, bila kujali umri, jinsia wala elimu, wale wanaojitambua na kulinda rasilimali hizi, wanafanya makubwa na kufanikiwa. Wale wasiojitambua na kuzilinda, wanaishia kuwa kawaida. Chagua kilicho sahihi kwako kulinda rasilimali hizo au kuzitawanya hovyo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha