Watu wengi wamekuwa wanapitia msongo wa mawazo kwenye maisha yao na wasijue nini chanzo.
Wanajikuta wamezama kwenye msongo huo na kushindwa kuondokana nao kwa sababu hawajui chanzo.
Kuna sababu kubwa mbili, ya kwanza ni kulazimisha mambo, kutaka mambo yawe tofauti na yalivyo au nje ya uwezo wako, sababu hii hatutaijadili sana leo.
Sababu ya pili na ambayo tutaijadili kwa kina leo ni kujidanganya.
Watu wengi wamekuwa wanaingia kwenye msongo pale ambapo hawawezi kujidanganya tena, pale ambapo uhalisia umekuwa wazi kiasi kwamba huwezi tena kujidanganya.
Iko hivi rafiki, maisha huwa yanatupa viashiria mbalimbali, lakini huwa tunavipuuza na kujidanganya kwamba mambo ni mazuri.
Baadaye mambo yanaharibika kiasi kwamba huwezi tena kujidanganya ni mazuri, na hapo ndipo mtu anapata msongo na kujiambia mambo yamebadilika kabisa.
Ukweli ni kunakuwa hakuna chochote kilichobadilika, ila hawawezi tena kujidanganya kwa sababu ukweli uko wazi mno.
Inaweza kuwa ni mahusiano ambayo hayaendi vizuri, lakini mtu anajidanganya na kutokuangalia uhalisia, inafika hatua mahusiano yamevunjika ndiyo uhalisia unakuwa wazi na mtu hawezi kujidanganya tena na hapo anakuwa na msongo.
Au inaweza kuwa ni biashara ambayo inasua sua, haiendi vizuri, lakini mtu anajidanganya mambo siyo mabaya, au siku siyo nyingi mambo yatabadilika, japo hakuna hatua za tofauti anazochukua. Kinachotokea ni biashara kufa na hapo uhalisia unakuwa wazi na mtu hawezi tena kujidanganya.
Kama unataka kujiepusha na msongo, acha kabisa kujidanganya, uone uhalisia kama ulivyo, usijiridhishe juu juu, angalia uone uhalisia na pata picha ya matokeo ya baadaye kama mambo yataenda kama yanavyoenda sasa. Usijidanganye kwamba mambo siyo mabaya sana, kama kuna kitu hakipo sawa, kichukulie hatua mara moja, ukiendelea kujidanganya na kusubiri, kuna siku utaumbuka na hapo utakaribisha msongo utakaokusumbua zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,