Nguvu ya asili ipo kwenye msimamo na kurudia rudia.
Hakuna chochote ambacho asili inafanya mara moja na kuacha, bali hurudia kwa muda mrefu na hapo ndipo matokeo makubwa hutengenezwa.
Chukua mfano wa tone la maji, moja pekee haliwezi kuleta madhara yoyote, lakini tone hilo linapojirudia mara nyingi, linaweza kuvunja mwamba mkubwa.
Hivi pia ndivyo safari ya mafanikio ilivyo, hakuna kitu utakachofanya mara moja na kisha kikaleta mafanikio makubwa na ya kudumu.
Bali mafanikio ni matokeo ya msimamo na kurudia rudia, kufanya kitu kwa muda mrefu bila ya kuacha.
Lakini hili limekuwa gumu kwa wengi kwa sababu kubwa mbili;
Moja hawajui kama inachukua muda na ni kitu endelevu, hivyo wanatumia muda mwingi kutafuta njia za mkato za mafanikio, za kufanya kitu mara moja kisha kupata mafanikio ya kudumu.
Mbili wanachoka haraka, kwa kuwa hawajui inahitaji muda, wengi huingia kwenye kitu kwa pupa, wanatumia vibaya nguvu zao na kuishia kuchoka haraka, hivyo hawawezi kuendelea kwa muda mrefu.
Wewe umepata bahati ya kujua hili, kwamba inahitaji msimamo na marudio ya muda mrefu, hivyo jipange vyema.
Jipe muda na fanya kwa kurudia rudia, chagua kitu ambacho unaweza kukifanya maisha yako yote na siyo unachotaka kufanya muda mfupi halafu uachane nacho.
Na muhimu zaidi, pangilia nguvu zako vizuri, usizitawanye hovyo, jua hizi ni mbio ndefu na siyo fupi. Unaweza kujisukuma ukakesha siku moja, lakini ukajikuta unalala siku mbili baadaye bila kufanya chochote. Sasa ni bora kupangilia vizuri muda wako, ili kila siku uweze kupiga hatua fulani kwenye kile unachofanya.
Kwa chochote unachofanya, jua sehemu kubwa ya mafanikio iko kwenye msimamo na kurudia rudia, hivyo kuwa tayari kurudia kufanya na kwa muda mrefu na usipoteze muda na nguvu zako kwa mambo yasiyochangia kukufikisha uendako, hasa njia za mkato.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Ni kweli kocha ,sehemu kubwa ya mafanikio ipo kwenye msimamo na kurudia rudia. Mafanikio ni mbio ndefu na siyo fupi. Nilichojifunza hapa ni kujenga tabia ya kuchukua hatua kuhusu jambo fulani kila siku bila kujali unajisikia kufanya au laa. Kwa mfano miongoni kwa malengo yangu mwaka huu 2020/2021 ni kujenga skills kuwa profit advisor na kutengeneza wateja angalau 20. Kwahiyo ili nijenge skills za kuwa profit advisor lazima nisome kitabu kinaelezea jinsi ya kutoa value hiyo hivyo nimejiwekea utaratibu wa kusoma kitabu angalau nusu saa kisha kufanya zoezi kuhusu nilichofanya angalau saa moja, na kwa upande wa kutengeneza wateja wapya ishirini nimenunua kozi jinsi ya kutangaza kwenye mitandao ya kijamii na kuwaleta wateja tarajiwa kwenye platform yangu ,kwahiyo nahitaji kutenga muda wa angalau nusu saa nisome jinsi ya kunasa wateja kwenye internet na kufanya mazoezi angalau saa moja, haya ndo mambo nayopaswa kufanya kila siku na kukazana kuwa bora.
LikeLike
Vizuri Hafidhi kwa mpango huu utakaoiwezesha biashara yako kukua.
Nenda kautekeleze kama ulivyopanga, kwa kila siku kuchukua hatua bila kuacha.
Kila la kheri.
LikeLike