Kama biashara haikui basi inakufa, na siyo kwamba inabaki pale pale.
Hivyo ni wajibu wako kama mfanyabiashara kuhakikisha kila wakati biashara yako inakua zaidi ya ilivyokuwa.
Biashara nyingi zinakufa kwa sababu wanaozifanya hawajui wanafanya nini. Wao wanafikiri wako kwenye biashara, ila ukweli hawapo kwenye biashara, wanasindikiza wengine wanaofanya biashara.
Kama unataka kweli kuwa kwenye biashara, uendeshe biashara ambayo inakua na kufanikiwa, lazima uwe na mkakati unaoufanyia kazi.
Siyo tu unaamka kila siku, unafungua biashara, unanunua, unauza na kufikiri mafanikio yatakuja. Unapoendesha biashara kwa njia hiyo na ikafa, unaishia kutafuta sababu za kujiridhisha, kwamba uchumi siyo mzuri, kwamba kuna chuma ulete, kwamba ushindani ni mkali, kwamba mtaji wako ni mdogo na mengine.

Kwenye makala ya leo ya ushauri wa changamoto, nakwenda kukushirikisha njia tano za uhakika za kuchukua ili kuiboresha biashara yako na kuikuza. Ukizijua njia hizi, ukazifanyia kazi na kujipima kila mwezi, hakuna namna biashara yako itashindwa kukua.
Kabla hatujaona njia hizo, tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye hili.
Ushauri ninaoomba ni kitu gani kinaweza kuiboresha biashara yangu? – Teresia Dominic Sekwa
Ushauri aliouomba mwenzetu Teresia niushauri ambao kila mfanyabiashara mdogo na wa kati anauhitaji sana, kwa sababu wengi wamekuwa wanafanya biashara kwa mazoea, kitu kinachopelekea biashara zao kufa bila ya wao kujua.
Hapa kuna njia tano za kukuza biashara yako na kuiwezesha kufanikiwa. Njia hizi zinatokana na namba muhimu unazopaswa kuzifuatilia na kuzijua kuhusu biashara yako, maana hizo ndiyo zinapima uhai na ukuaji wa biashara yako.
NJIA YA KWANZA; MTAJI UNAOZUNGUKA.
Mtaji unaozunguka kwenye biashara ndiyo damu ya biashara, huu ukipungua biashara inakosa uhai na kufa. Hivyo kila wakati lazima ujue ni mtaji kiasi gani unaozunguka kwenye biashara.
Hakikisha matumizi unayoondoa kwenye biashara, iwe ni binafsi au ya biashara hayagusu kabisa mtaji.
Pia kwa kila faida unayopata kwenye biashara, asilimia fulani unapaswa kuirudisha kwenye mtaji.
Kila wakati tumia njia mbalimbali kukuza mtaji, ukianza na vyanzo vyako vingine vya fedha, kurudisha faida, kupata fedha kutoka kwa wadau mbalimbali na pale unapokidhi kuchukua mkopo.
Kila wakati lazima uwe na mkakati unaofanyia kazi wa kukuza zaidi mtaji unaozunguka kwenye biashara kwa sababu kama mtaji haukui, biashara haiwezi kukua.
Hatua ya kuchukua; kila wiki na kila mwezi kokotoa kiwango cha mtaji unaozunguka kwenye biashara na kuwa na mkakati wa kukuza mtaji huo. Jiwekee lengo la mtaji huo kukua kwa angalau asilimia 20 kila mwaka na litekeleze.
NJIA YA PILI; MAUZO.
Mauzo ndiyo njia pekee inayoleta fedha kwenye biashara yako, bila mauzo hakuna fedha na hivyo biashara haiwezi kwenda.
Unapaswa kuwa na mkakati mzuri wa mauzo kwenye biashara yako, kwa kujua kile unachouza na wateja unaowalenga kisha kuwa na njia ya kuwashawishi wateja hao kununua kile unachouza.
Kitu kimoja unachopaswa kujua ni kwamba watu hawapo tayari kutengana na fedha zao kununua unachouza. Lakini pia wanakutana na kelele nyingi za kuwashawishi watengane na fedha zao.
Lazima wewe uwe na sababu ya mashiko kwa nini wanunue unachouza na kwa nini wanunue kwako. Hivyo jua mahitaji yao na jinsi kile unachouza kinavyowasaidia na washawishi kwa njia hiyo.
Kingine muhimu kwenye mauzo ni usisubiri wateja waje kwenye biashara, watafute, wafuate walipo, tangaza, wasiliana nao kwa njia mbalimbali kuwashawishi waje kwenye biashara yako.
Hatua ya kuchukua; tengeneza mpango wa mauzo wa biashara yako, unaoanza na kile unachouza, tatizo ambalo kinatatua, wateja unaowalenga, walipo, jinsi unavyowafikia na jinsi ya kuwashawishi. Kisha jiwekee kiwango cha mauzo utakachojisukuma kufanya kila siku, wiki na mwezi na jisukume kukifia huku ukijipima.
NJIA YA TATU; WATEJA.
Wateja ndiyo wanaonunua kile unachouza na wanaoleta fedha kwenye biashara. Hivyo unapaswa kuwa na njia ya kuwavutia wateja na kwenda nao kwa muda mrefu.
Unapaswa kujua wateja ulionao sasa na kutengeneza wateja wapya kwa biashara yako.
Tengeneza mahusiano mazuri na wateja wako kwa kuwasiliana nao mara kwa mara ili wajione wakiwa sehemu ya biashara yako.
Hatua ya kuchukua; jua idadi ya wateja ulionao sasa na kuwa na njia za kupata wateja wapya. Kila mwezi jipime kwa wateja uliowahudumia, wapya na wa zamani. Kuwa na mawasiliano ya wateja wako na wasiliana nao mara kwa mara ili wawe karibu na biashara yako.
NJIA YA NNE; GHARAMA ZA BIASHARA.
Kuna gharama mbalimbali unazoingia katika kuendesha biashara yako. Inaweza kuwa ni pango la eneo unalifanyia biashara, kodi ya serikali, wafanyakazi wanaokusaidia, usafiri na matumizi mengine.
Hili ni eneo ambalo usipokuwa nalo macho utajikuta unauza sana lakini hela huioni, kwa sababu inamezwa na matumizi makubwa.
Na kwa wafanyabiashara wengi wadogo, mahitaji binafsi pia yamekuwa yanaingia moja kwa moja kwenye biashara na hivyo kuibebesha mzigo mzito.
Hatua za kuchukua; zijue gharama zako za msingi za kuendesha biashara na zidhibiti sana zisikue. Mahitaji yako binafsi usichukue moja kwa moja kwenye biashara, badala yake jilipe kiasi fulani kutoka kwenye biashara.
NJIA YA TANO; FAIDA.
Faida ndiyo matokeo ya mwisho ya biashara inayoendeshwa vizuri, kama biashara ni mtihani, basi faida ni ufaulu. Unakuwa umefaulu kuendesha biashara yako pale unapoweza kuzalisha faida.
Na faida halisi ni pale unapochukua mauzo kisha ukatoa manunuzi/uzalishaji na gharama zote za kuendesha biashara.
Unapaswa kukazana kutengeneza faida kwenye biashara yako na sehemu kubwa ya faida hiyo kurudi kwenye biashara kama ukuaji wa mtaji. Kwa njia hiyo utaweza kuikuza sana biashara yako.
Hatua ya kuchukua; jiwekee kiwango cha faida unachotaka kufikia kila mwezi, kisha kokotoa gharama zako za biashara kwa mwezi na jua mauzo kiasi gani yatakufikisha kwenye faida hiyo. Hapo sasa jisukume kufikia mauzo hayo, kwa kukuza wateja zaidi.
HATUA YA MSINGI KABISA.
Hatua tano ulizojifunza hapa, zinafanya kazi vizuri kama utaweza kuzifanyia kazi na zitakupa matokeo makubwa mno.
Lakini matokeo yake siyo ya haraka, ni jambo linalohitaji muda, ujuzi wa kina, uvumilivu, msimamo na ung’ang’anizi.
Kitu kikubwa ninachokushauri ni uwe na mwongozo mzuri unaoutumia kuendesha biashara yako.
Na hapa nakushauri uwe na kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA BIASHARA ambacho nimekiandika, kimejadili kwa kina hatua hizo tano na nyingine muhimu kama kutoa huduma bora kwa wateja, kusimamia vizuri mzunguko wa fedha na kuikuza zaidi biashara.

Kama upo kwenye biashara, unapaswa kuwa na kitabu hiki, maana ndiyo rejea kuu kwako katika safari ya biashara.
Kama bado huna kitabu hicho, jipatie nakala yako sasa, piga simu 0752 977 170 na utaletewa kitabu kama upo Dar es salaam au kutumiwa kama upo mkoani.
Biashara ni sayansi na sanaa kwa wakati mmoja, huwezi kufanikiwa kwa mazoea, lazima uwe na misingi na miongozo sahihi unayoifuata. Anza na hii mitano na jifunze mingine kutoka kwenye kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA BIASHARA na utaendesha biashara yenye mafanikio makubwa.
Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani
TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.
Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania
Rafiki, karibu upate na kusoma vitabu vizuri vya maendeleo binafsi na mafanikio kwa lugha ya Kiswahili. Pakua na weka app ya SOMA VITABU na upate maarifa sahihi. Kwa maelezo zaidi fungua; https://amkamtanzania.com/somavitabuapp