Moja ya vitu vikubwa sana nilichojifunza kwenye kitabu cha THE PYSCHOLOGY OF MONEY kilichoandikwa na Morgan Housel kuhusu maamuzi ya kifedha ni kwamba hakuna anayedhani hayuko sahihi.

Kila maamuzi ya kifedha ambayo anayafanya mtu, yako sahihi kwa upande wake na kwa hali anayokuwa nayo wakati anafanya maamuzi hayo.

Hili ni jambo la kawaida mno, lakini sikuwa nimelijua na kulitazama kwa undani wake.

Huwa tunawashangaa wengine pale wanapofanya maamuzi ya aina fulani, kwa kuona wanakosea au hawajui wanachofanya, lakini ukweli ni kwamba kwa upande wao wako sahihi kabisa.

Chukua mfano wa mtu anayecheza bahati nasibu ya kununua tiketi kwa shilingi elfu 2, ambapo zawadi ya ushindi ni mamilioni ya fedha, lakini nafasi ya kushinda ni finyu mno.

Lakini bado watu masikini wananunua tiketi hizo za bahati nasibu, licha ya kwanza nafasi ya kushinda ni ndogo mno.

Watu wamekuwa wakiwashangaa kwa maamuzi hayo, ni mpaka tafiti zilipoonesha kwa nini watu huwa wanafanya hivyo. Kwa tafiti zilizofanywa, zinaonesha kwamba watu wanaocheza bahati nasibu hizo siyo wanategemea kushinda zawadi, ila wanachonufaika nacho ni kile kipindi wanachonunua tiketi na kusubiria matokeo.

Katika kipindi hicho wanakuwa na matumaini kwamba huenda wakashinda bahati nasibu hiyo. Ni matumaini hayo ndiyo wanayonufaika nayo kwenye kucheza bahati nasibu hizo. Ndiyo maana hata wakishindwa, bado wanacheza tena na tena na tena.

Kwa kuelewa hivi unaweza kuona kwa nini watu wengi wanacheza bahati nasibu ambazo uwezekano wa kushinda ni mdogo, wanachonufaika nacho ni yale matumaini wanayokuwa nayo kwa muda mfupi.

Tunapaswa kuacha kuwashangaa watu kwa maamuzi ya kifedha wanayoyafanya, wengi wanaamini wako sahihi na ndiyo maana wanayafanya.

Kama tunataka kuwasaidia watu kufanya maamuzi sahihi kifedha, lazima tujue kwanza saikolojia zao. Bila kujua hilo, tutawashangaa, tutawasema vibaya na tutawalazimisha wawe kama tunavyotaka sisi, lakini hawatafanya hivyo.

Unaweza kumshauri mtu vizuri sana kuhusu fedha, lakini akaenda kufanya maamuzi ya tofauti mpaka ukamshangaa. Jua tatizo siyo ushauri wako, bali tatizo ni kile kilicho ndani yao inapokuja kwenye fedha.

Hili pia linapaswa kuwa msaada kwetu, kwa tabia za kifedha tulizonazo ambazo zinatukwamisha, tunapaswa kujichunguza tabia na hisia tulizonazo kifedha. Kama tunataka kubadili tabia hizo, lazima kwanza tubadili tabia na hisia tulizonazo.

Kujifunza zaidi kwenye kitabu cha The Psychology Of Money, soma uchambuzi wake kwa kubonyeza hapa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha