“Stop letting yourself be distracted. That is not allowed. Instead, as if you were dying right now… Stop allowing your mind to be a slave, to be jerked about by selfish impulses, to kick against fate and the present, and to mistrust the future.” — Marcus Aurelius

Upo kwenye vita na adui yako mkuu ni usumbufu unaokuzunguka.
Kuna watu wanatumia gharama kubwa kuhakikisha wananasa umakini wako.
Kila habari, tangazo, mitandao ya kijamii na mengine yanayoendelea, yanalenga kunasa umakini wako.

Kama unayataka mafanikio makubwa na utulivu kwenye maisha yako, jukumu la kwanza ni kushinda vita hii ya usumbufu.
Kulinda sana umakini wako na kuhakikisha unakwenda kwenye yale mambo yaliyo muhimu pekee.
Kumbuka ni vita, hivyo zoezi hilo halitakuwa rahisi.
Na kama ambavyo nimekuwa nakueleza, umakini wako ni faida kubwa kwa watu wengine, ndiyo maana wanatumia kila gharama kuunasa.

Ni wakati sasa wa kulinda mno umakini wako, ili uwe faida kwako.

Dalili za kwamba umeshindwa vita hiyo ya usumbufu ni hizi;
👉🏽Unaposema huna muda wa kusoma vitabu lakini unajua kila habari inayoendelea.
👉🏽Unapolalamika hupati muda wa kuanzisha biashara ya pembeni wakati kila siku hukosi kuingia kwenye mitandao ya kijamii na kufuatilia maisha ya wengine.
👉🏽Unaposema huna muda wa kuweka juhudi zaidi kwenye kile unachofanya, wakati unabishana na wengine kuhusu mambo ya michezo, siasa na mengineyo.

Ukishajikuta uko bize, kila siku unaianza na kuimaliza ukiwa umechoka kweli kweli, lakini yale ambayo ni muhimu kwa ukuaji wako binafsi, mafanikio yako na hata utulivu wako wa ndani hupati muda wa kuyafanya, umeshashindwa hii vita.

Kila siku mpya unayoianza ni siku ya mapambano, siku ambayo maadui zako wamejipanga kweli kweli kunasa umakini wako.
Hivyo ianze kila siku ukiwa na mkakati wa kushinda hiyo vita, uwe tulivu na mwenye umakini ili uweze kutekeleza yale muhimu kwako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu hakuna anayekosea, soma hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/12/15/2176

Rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr Makirita Amani.