Tasnia ya mauzo imekuwa inachukuliwa kama isiyo ya uaminifu, ambapo wauzaji hutumia kila mbinu kumshawishi mtu kununua kitu ambacho hakihitaji.
Ni kweli kuna wauzaji wengi wenye mtazamo huo, ambao kwao wanachojali ni kuuza na kupata fedha, bila kujali anayenunua kitu hicho kina manufaa kwao au la.
Wauzaji hawa huwa wanajisifia kabisa kwamba wanaweza kuuza kitu chochote kwa mtu yeyote. Na hiyo ni dalili tosha kwamba watu hao siyo wauzaji, bali matapeli.
Kuna watu wenye vipaji vya ushawishi, ambao wakiongea kitu, unajikuta unawaamini na kufanya wanachokushawishi. Lakini baadaye unapokuja kutulia, unagundua maamuzi uliyofanya siyo sahihi kwako.
Kama una kipaji au mafunzo na mbinu za mauzo unaweza kuwashawishi watu wanunue unachouza hata kama hakina manufaa kwao. Lakini utakuwa umejijengea kikwazo kikubwa, watu hao hawatanunua tena kwako, tena watajifunza kukukwepa, wakikuona wanakimbia kabisa ili usije kuwahadaa tena.
Njia bora ya kuuza siyo kutumia mbinu na ulaghai kuwashawishi watu wakubali kile unachouza. Njia bora kabisa ni kuwahudumia wengine, kuwa mtu unayejali wengine na kuona maumivu waliyonayo, kisha kuwapa kile ambacho kinawaondolea maumivu hayo.
Njia bora ya mauzo ni yenye utu, ambapo unajiweka kwenye viatu vya mteja wako, ambapo unajua kwa undani mahitaji yake na una suluhisho lenye manufaa kwake.
Unapomshawishi kununua, siyo tu kwa sababu unataka pesa, lakini pia unajua una kitu chenye manufaa kwake. Na siyo kwa nadharia, bali kwa uzoefu wako binafsi, kwa sababu wewe pia ni mtumiaji mzuri wa kile unachomshawishi mtu mwingine anunue.
Kwa kujiweka upande wa kutoa huduma, kwa kuweka utu wako kwenye kile unachofanya, utakuwa na ushawishi mzuri, watu sahihi watanunua kwako na watanufaika, kitu kitakachowafanya waendelee kununua na hata kuwakaribisha wengine kununua.
Kwenye kila jambo huwa kuna njia mbili, moja rahisi na yenye matokeo ya haraka na moja ngumu na matokeo yake yanachelewa. Kwenye mauzo, kutumia ulaghai ni rahisi na matokeo yake ni ya haraka, lakini hayadumu. Kutoa huduma ni kugumu na matokeo yake yanachukua muda, ila yanadumu.
Chagua njia ipi unataka kutumia, lakini kama unataka mafanikio makubwa na ya kudumu, kwa chochote unachofanya, kwa chochote unachouza, jiweke upande wa kutoa huduma.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,