Biashara ndiyo njia ya uhakika ya kufika kwenye utajiri na mafanikio makubwa kwenye maisha. Hiyo ni kwa sababu unapomiliki biashara yako, hakuna anayekuwekea ukomo wowote.

Lakini biashara ni ngumu kuanzisha, ngumu kufanya na ngumu kuikuza ifike kwenye ngazi za kukupa mafanikio makubwa.

Huu ni ukweli ambao wengi wanaotaka kuingia kwenye biashara hawapendi kuusikia, wanaingia kichwa kichwa na kuishia kuanguka vibaya.

Tafiti nyingi zilizofanywa kwenye biashara zinaonesha wazi kwamba katika biashara 10 zinazoanzishwa, ndani ya miaka miwili 8 zinakuwa zimekufa kabisa. na mbili zinazosalia, moja ndiyo inakuwa na mafanikio baada ya miaka mitano.

Kama biashara ingekuwa ni shule au fani ya kusomea, basi ndiyo inayoongoza kwa wanafunzi wengi kufeli. Na wengi wa wanaofeli ni kwa sababu wanakataa kuuangalia ukweli, wanajidanganya na wanapokutana na uhalisia, wanaanguka vibaya.

Kupitia makala za USHAURI WA CHANGAMOTO, nimekuwa natoa ushauri kwa changamoto mbalimbali ambazo watu wamekuwa wanapitia kwenye maisha na zinawakwamisha kufanikiwa.

Sehemu kubwa ya changamoto ambazo watu wamekuwa wanaomba ushauri ni kwenye biashara. Kuna changamoto ambazo zimekuwa zinaombewa sana ushauri, na nimeshazijibia huko nyuma. Lakini leo nazikusanya kwa pamoja na kuzijibia tena.

Karibu ujifunze hatua sahihi za kuchukua kwenye changamoto hizi zinazokwamisha biashara nyingi.

Moja; MTAJI.

Changamoto kubwa inayofanya nishindwe kufikia malengo ni mtaji, nina uwezo wa kufanya shughuli za kilimo, biashara, ufugaji, ili niweze kufanya kazi hizo mojawapo nilihitaji mtaji wa milioni moja, nifanyeje ili niipate? – Isaya E. B.

Nataka kuanzisha duka la Mangi yaani mchele, unga, juisi, maji, sukari nk ila nina mtaji wa laki 500, nikipiga mahesabu hayaji kabisa kuifanya hiyo ila naipenda tu ndio changamoto yangu naomba kusaidiwa. Ahsante sana. – Odilia K.

Mtaji ni changamoto ambayo imekuwa inatajwa sana. Kuna njia mbalimbali za kupata mtaji wa kuanzisha biashara.

Lakini njia kuu ambayo huwa nashauri kwa wale wanaoanzia chini kabisa ni kujiwekea akiba zako mwenyewe. Hapa unahitaji kuwa na shughuli nyingine ha kufanya inayokuingizia kipato na sehemu ya kipato hicho kuiweka akiba. Kama una ajira kila mwezi tenga angalau asilimia 10 ya mshahara wako na iweke mahali ambapo huwezi kuitumia. Kama huna ajira, tafuta shughuli ya kufanya, hata kama ni vibarua vya kutumia nguvu zako, fanya chochote halali kinachokuingizia kipato na kisha sehemu ya kipato hicho weka akiba kama mtaji wa kuanza biashara unayotaka.

Mbili; Muda.

Muda wa kuendesha biashara umekuwa changamoto kwa wengi. Hapa kuna wale ambao biashara inawategemea kwa kila kitu na kuna wale ambao wana shughuli nyingine wanayofanya na biashara ni kitu cha ziada.

Kwa wale ambao biashara inawategemea kwa kila kitu, weka vipaumbele vyako vizuri. Jua yale majukumu muhimu kwako kufanya ambayo hakuna mwingine anaweza kuyafanya vizuri na hayo ndiyo yape kipaumbele cha kwanza. Kwa majukumu mengine, tafuta watu wa kukusaidia kuyafanya. Jua huwezi kufanya kila kitu, hivyo chagua kufanya yaliyo muhimu na yenye tija.

Kwa wenye shughuli nyingine na biashara kwa pamoja, kwanza chagua biashara ambayo inaendana na muda unaoweza kupata. Kisha igawe siku yako moja kwenye siku mbili, moja ni masaa ya kazi na mbili ni masaa ya kuwa kwenye biashara. Kama unavyoheshimu masaa ya kuwa kwenye kazi, heshimu hivyo pia masaa ya kuwa kwenye biashara. Mfano kama unaingia kazini saa moja asubuhi na kutoka saa tisa mchana, hiyo ni siku yako ya kazi. Hapo sasa unahitaji siku ya biashara ambayo inaweza kuwa kuanzia saa 10 jioni mpaka saa 4 usiku. Lazima uheshimu siku hiyo ya biashara kama unavyoheshimu ya kazi na kupangilia vizuri muda wako kwa vipaumbele.

Tatu; wateja.

Changamoto ya kutowapata wateja wangu. – E. Komba

Utafutaji wa masoko simudu sana, nifanyeje? – Ajok A. M.

Biashara ni wateja, biashara nyingi hufa pale zinapokosa wateja wa uhakika. Wengi huingia kwenye biashara kwa mtazamo potofu, kwamba ukishafungua biashara basi wateja wataona na kuja wenyewe. Hilo siyo sahihi. Kwa zama tunazoishi sasa, wateja wamevurugwa, wana usumbufu mwingi kiasi kwamba wanaweza kuwa wanapita mbele ya biashara yako kila siku na hawajui kama upo.

Hivyo unapaswa kuwatafuta wateja, unapaswa kuwa na mkakati wa masoko ambao unaufanyia kazi. Kwanza kwa kujua ni thamani gani unayotoa kwenye biashara yako, kisha kujua wateja wa aina gani unaowalenga, kujua wanapatikana wapi na kisha kuwafuata kule waliko na kuhakikisha wanajua kuhusu uwepo wa biashara yako.

Hili ni eneo unalopaswa kulifanyia kazi hasa, la sivyo biashara yako haiwezi kukua. Biashara inakua pale inapoongeza wateja wapya kila wakati.

Nne; mauzo.

Mitandao imerahisisha watu kutangaza biashara zao, watu wanapost sana picha mitandaoni na wateja wanajua kweli kwamba watu hao wanafanya biashara gani. Lakini inapokuja kwenye kununua, wateja wengi hawanunui. Wanaweza kuulizia bei, wakaomba hata punguzo lakini mwisho wa siku hawanunui. Biashara nyingi zinaathirika na hili, wateja wanafika na kuulizia lakini hawanunui.

Unapaswa kuwa na mkakati wa mauzo, unaowashawishi na kuwasukuma wateja kununua kila wanapofika kwenye biashara au kuulizia. Kutoa pesa huwa kunauma, hivyo usifikiri mteja atakuja kwako na kukupa fedha kirahisi. Ana matumizi mengi na pesa zake, lazima umeshawishi kweli kwamba kukupa wewe pesa hizo kuna manufaa makubwa kwake kuliko kwenda kuzitumia kwingine.

Kwa kile unachouza, jua maumivu ya wateja wako yako wapi na jinsi gani unachouza kinatuliza maumivu yao. Kisha wanapofika kwenye biashara yako, tonesha vidonda vyao, wafanye wayasikie maumivu yao kisha onesha jinsi kile unachouza kinavyotuliza maumivu hayo. Huo ndiyo unakuwa mkakati wako wa mauzo.

Tano; Mzunguko wa fedha.

Mimi nafanya biashara ambayo kwa sasa ina miaka 2 changamoto kubwa ni madeni yaani kila mtaji ukipungua nakopa hela na hizo hela zinanitesa kuzirudisha. – Asifiwe A. M.

Kuna usemi wa Kiswahili ambao ni maarufu sana kwa biashara ndogo ndogo, msemo huo ni ‘chuma ulete’. Dhana ni kwamba mtu kwenye biashara yake anauza sana, tena sana, lakini haoni pesa zinaenda wapi. Hapo mtu anashawishika kwamba kuna watu wanaiba fedha kwenye biashara kwa njia za kishirikina. Lakini hilo siyo kweli, hakuna anayeweza kuiba fedha kwenye biashara zako kwa njia za kishirikina. Ataiba wazi wazi kama mwanya upo au uzembe wako utaleta hasara.

Kutokujua mzunguko wa fedha wa biashara ni kikwazo kwa biashara nyingi kukua. Wengi huwa wanafurahia kununua na kuuza, lakini hawajui kuhusu mapato na matumizi.

Huhitaji kuwa mhasibu kuweza kukokotoa mzunguko wa fedha kwenye biashara yako, unachohitaji kujua ni vitu viwili, pesa kiasi gani inaingia kwenye biashara na kiasi gani imetoka. Ili biashara iwe na afya, lazima pesa inayoingia iwe kubwa kuliko inayotoka.

Tunza vizuri kumbukumbu za kila unachofanya kwenye biashara kisha kokotoa kila siku, kila wiki na kila mwezi. Pesa ya biashara wacha ikae kwenye biashara na usiitoe kwa matumizi binafsi. Na muhimu zaidi, jua faida kiasi gani unatengeneza na sehemu ya faida hiyo unapaswa kuirudisha kwenye mtaji wa biashara.

Sita; gharama za biashara.

Gharama za kuendesha biashara imekuwa kitu ambacho wafanyabiashara wengi hawafuatilii na kudhibiti, hivyo zinakua na kumeza kila faida inayopatikana.

Lazima uzijue gharama za msingi za kuendesha biashara yako na kuzidhibiti zisikue kadiri faida ya biashara inavyoongezeka.

Saba; wasaidizi.

Nimefungua biashara ya dawa kwa kutegemea mke wangu ana fani hiyo lakini mambo yamekua tofauti kutokana na kutojali hiyo biashara nakuona haina msingi na kuiacha kusimamia ipasavyo sijui nifanye nini na mimi sina ujuzi wa kuuza dawa lakini anataka aone na mimi nakaa dukani na kuuza. – Ayubu J. M.

Msimamizi wa biashara pindi ninapokuwa kazini, na nina mchumba napata wasiwasi kidogo kumuachia biashara. Samson J. B.

Kupata wasaidizi sahihi kwenye biashara imekuwa changamoto kubwa. Kuna watu wengi wanatafuta kazi za kufanya, ila ukiwapa kazi hawawezi kuzifanya vizuri. Kila mfanyabiashara ambaye amewahi kuajiri anajua jinsi ilivyo vigumu kupata watu sahihi wa kuajiri.

Kitu kikubwa unachopaswa kuzingatia katika kupata wasaidizi wazuri kwenye biashara yako ni kuangalia kwanza tabia kabla ya ujuzi. Unaweza kumfundisha mtu yeyote yule ujuzi, lakini huwezi kumfundisha tabia. Hivyo anza na tabia. Na tabia za kuangalia ni tatu; UADILIFU, AKILI NA NGUVU.

Mwekezaji bilionea Warren Buffett ana msingi wake amekuwa anautumia kwenye kuajiri ambapo anasema huwa anaangalia UADILIFU, AKILI na NGUVU na kama mtu hana sifa ya kwanza, basi hizo mbili zitakuwa hatari.

Tumia sifa hizo katika kutafuta watu sahihi wa kukusaidia kwenye biashara yako.

Nane; ushindani.

Ushindani wa biashara umekuwa mkali kwa sababu ni rahisi mno kuingia kwenye biashara katika zama hizi kuliko kipindi cha nyuma. Hivyo biashara yoyote unayoifanya, kuna wengine wanaweza kuifanya pia, na wakiona unanufaika, wataifanya.

Hata kama umekuja na biashara mpya kabisa, ikiwa na mafanikio kuna wengine nao wataanza kuifanya.

Kukabiliana na ushindani usishindane, badala yake jitofautishe. Kwa biashara yoyote ile unayofanya, angalia jinsi ya kujitofautisha na wengine wote wanaoifanya. Kuwa na kitu ambacho wewe tu ndiye unayeweza kukifanya, ambacho mteja hawezi kukipata sehemu nyingine isipokuwa kwako.

Ushindani wa moja kwa moja kwenye biashara una gharama kubwa na utakuangusha, achana nao na jitofautishe. Weka upekee na utofauti wako kwenye biashara, toa huduma zilizo bora na wape wateja sababu ya kuacha wengine na kuja kwako.

Tisa; taratibu za kisheria.

Usajili, leseni na kodi ni taratibu muhimu za kisheria ambazo kila mfanyabiashara anapaswa kuzifuata. Kipindi cha nyuma watu walikuwa wanaweza kufanya biashara bila kujali taratibu hizo na wasisumbuliwe. Lakini sasa mambo yamebadilika, kila aina ya biashara sasa ina mifumo ya usajili, leseni na kulipa kodi.

Jua kwa biashara unayofanya ni usajili wa aina gani unapaswa kuwa nao, leseni gani unapaswa kuwa nazo na utaratibu wa kulipa kodi kulingana na mzunguko wa biashara yako. Usikwepe mambo haya, yatakuwa kikwazo kwa biashara yako.

Kumi; kuikuza zaidi biashara.

Kwanza nitoe shukurani kwako kocha katika ukocha wako tangu nianze pata mafunzo nashukuru sana biashara yangu imekuwa Kila jamaa na marafiki zangu wakifika kwa biashara mambo ni mazuri . Changamoto yangu ni biashara imekua inaniomba kuajili kijana nashindwa nianzie wapi nashindwa mpaka kusafiri kufuata bidhaa duka linanitegemea nianzie wapi? – Joseph M.

Kuna wafanyabiashara wengi ambao wanaanzia biashara chini kabisa, wanapambana na biashara zinapata mafanikio fulani. Lakini baada ya kufika ngazi fulani ya mafanikio, biashara haikui tena. Miaka nenda rudi biashara inakuwa pale pale. Huku mwanzilishi akichoka na asiweze kupambana kama awali na hilo kupelekea biashara kuanza kuanguka.

Ili biashara iweze kukua zaidi, isiwe na kikomo, lazima uitengenezee mfumo wa kuweza kujiendesha bila ya kumtegemea mwanzilishi wake. Hivyo wakati bado biashara yako ni ndogo, tengeneza mfumo. Kila unapopiga hatua, hakikisha biashara inakutegemea wewe kidogo na kutegemea mfumo zaidi.

Unapofanikiwa kuwa na mfumo wa biashara ambayo inaweza kujiendesha yenyewe bila ya wewe kuwepo kabisa, unakuwa umefikia mafanikio ya juu kabisa na yasiyo na ukomo. Hiki ni kitu kinachojengwa kwa muda, hivyo anza nacho mapema.

Hayo ndiyo majibu ya changamoto kumi zinazokwamisha biashara nyingi. Kujifunza kwa kina kuhusu biashara na jinsi ya kupata wazo, kukuza mtaji, kudhibiti mzunguko wa fedha na taratibu za kisheria, soma kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA BIASHARA. Kitabu hicho ni mwongozo kamili ambao kila mfanyabiashara anapaswa kuwa nao.

Kama bado hujapata nakala yako ya kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA BIASHARA, wasiliana sasa na 0752 977 170 na utatumiwa au kuletewa kitabu ulipo.

Kama nilivyoanza makala hii, nakusisitiza tena, biashara ndiyo njia ya uhakika ya kufikia mafanikio makubwa na utajiri, lakini siyo rahisi. Unapokuwa na mwongozo sahihi unapunguza ugumu, zingatia haya uliyojifunza hapa pamoja na kusoma kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA BIASHARA na utaweza kufanikiwa sana kupitia biashara.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania

Rafiki, karibu upate na kusoma vitabu vizuri vya maendeleo binafsi na mafanikio kwa lugha ya Kiswahili. Pakua na weka app ya SOMA VITABU na upate maarifa sahihi. Kwa maelezo zaidi fungua; https://amkamtanzania.com/somavitabuapp