Nakumbuka sherehe za zamani ambapo watu walikuwa wanapakuliwa na kupelekewa chakula pale walipokaa. Haikujalisha unapenda au hupendi nini, chakula kilipakuliwa sawa kwa wote na kisha kusambazwa kuwapelekea walipo.

Lakini sherehe za siku hizi zimebadilika kabisa, hakuna tena wa kukupakulia chakula na kukuletea ulipo, bali unapaswa kwenda eneo la chakula na kujipakulia mwenyewe au kuchagua upakuliwe nini. Hilo linampa mtu uhuru wa kuchagua, kama hupendi pilau, huchukui na kadhalika.

Hivyo ndivyo mafanikio yalivyo, hayakufuati pale ulipo, bali wewe unapaswa kuyafuata mafanikio yalipo.

Na ili kufanikiwa unapaswa kuchukua hatua mbili muhimu ambazo umekuwa unazichukua kwenye kupata chakula kwenye sherehe.

Hatua ya kwanza ni kuingia kwenye mstari. Wakati wa kupata chakula kwenye sherehe, huwa kuna mstari wa kuelekea eneo la chakula. Ili upate chakula lazima utoke pale ulipokaa na kujiunga na mstari unaoelekea kwenye chakula. Hutapata chakula kwa kuendelea kukaa pale ulipo.

Kwenye mafanikio lazima uchague nini unataka kufanya, ni eneo lipi unalotaka kufanikiwa na wapi unapotaka kufika. Huwezi kubaki hapo ulipo sasa na kutegemea ufanikiwe, lazima uwe na sehemu nyingine unayotaka kufika na huo ndiyo unakuwa mstari wako uliochagua.

Hatua ya pili ni kukaa kwenye mstari na kupiga hatua kuelekea kwenye chakula. Ukishaingia kwenye mstari hupati chakula hapo hapo, bali mstari unasogea taratibu kuelekea kwenye chakula. Unapaswa kuwa na uvumilivu na kupiga hatua hizi kuelekea kwenye chakula. Hutapata chakula kama utaona mstari ni mrefu na kurudi kukaa.

Kwenye mafanikio, baada ya kuchagua nini utafanya, unapaswa kuchukua hatua kila siku ili kufika kule unakotaka kufika. Haitatokea haraka wala kwa miujiza, itahitaji muda na kazi, hivyo kuwa tayari kuweka vitu hivyo, huku ukiwa na uhakika kwamba mstari wako unasogea kuelekea kwenye mafanikio.

Naamini wakati unasoma hapa umejiona kwenye moja ya mstari ambao umewahi kuwepo kupata chakula, iwe ni kwenye sherehe au mgahawa. Tumia picha hiyo hiyo kuona ni mstari gani wa mafanikio uliopo, ni hatua zipi unazopiga ili kuyafikia mafanikio.

Wakati mwingine unapokuwa kwenye mstari huwa unachungulia mbele kuona ni umbali kiasi gani umebakisha kufika kwenye sehemu ya chakula, kadhalika jipime kwa hatua unazopiga na ona ulikotoka, ulipo sasa na kule unakofika, hilo litakupa msukumo wa kuendelea kubaki kwenye mstari na kupiga hatua kuelekea kwenye lengo.

Ingia na kaa kwenye mstari wa mafanikio yako, kisha piga hatua kila siku kuyafikia mafanikio yako, kuna ugumu gani hapo? Watu huhangaika na mambo mengi magumu lakini hawaingii na kukaa kwenye mstari wowote na ndiyo maana hawapigi hatua kubwa. Wewe umeshajua, fanya kilicho sahihi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha