Wazazi ambao walipitia magumu wakati wa utoto wao, hupambana ili watoto wao wasipitie magumu kama waliyopitia wao.
Wanafanya hivyo kwa nia njema, lakini kama tulivyoona kwenye ukurasa wa jana, nia njema huja kuzalisha matokeo yasiyo mazuri.
Katika kumzuia mtoto asipitie magumu, mzazi anaondoa kabisa kila nafasi ya kushindwa na hivyo mtoto hakosi au kushindwa chochote katika utoto wake.
Akifanya makosa mzazi anakuwa wa kwanza kumsaidia kutoka kwenye makosa yake. Akitaka kitu chochote kile mzazi anahakikisha anakipata. Anaona asipompa mtoto kila anachotaka, ataonekana siyo mzazi bora.
Kufanya hivyo haiwasaidii watoto, bali inawapotosha, inawapa picha isiyo sahihi kuhusu ulimwengu. Inawafanya waone kwamba ulimwengu unapaswa kuwasikiliza wao, na kuwapa kila wanachotaka.
Lakini hivyo sivyo ulimwengu unavyofanya kazi, hakuna anayepata kila anachotaka na kwa wakati anaotaka mara zote, hayupo. Hata raisi wa taifa kubwa duniani, hapati kila anachotaka kwa namna anayotaka na kila mara.
Kwenye maisha kuna kupata na kukosa, ambavyo vinakwenda pamoja, kupata kitu kimoja maana yake umekosa kingine. Kwenye maisha kuna kushindwa, unaweza kufanya kila unachopaswa kufanya na ukashindwa.
Na la muhimu zaidi maisha hayana usawa, unaweza kuwa upande sahihi na bado ukapata matokeo mabaya huku wale unaowaona wako upande usiyo sahihi wakipata matokeo mazuri.
Mtoto aliyekuzwa kwa kulindwa, anayekua akiwa na picha ya dunia kumtumikia yeye na matakwa yake, anakosa maandalizi muhimu ya kukabiliana na ulimwengu halisi na inampelekea kushindwa vibaya.
Watoto wanahitaji kushindwa, tena tangu wakiwa wadogo, wanahitaji kukosa baadhi ya vitu wanavyotaka, wanahitaji kukasirika, kuhuzunika na kuwa na wasiwasi, hivyo ndivyo maisha yalivyo.
Tusiwalinde sana watoto kwenye vitu hivyo, hatuwasaidii kwa kufanya hivyo, bali tunawafanya wawe dhaifu katika kukabiliana navyo.
Waswahili waliposema asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu walikuwa sahihi sana, ulimwengu hauna huruma na hauangalii nani ni nani, wenyewe unakwenda kwa mipango yake na asiyeelewa hilo atapata adhabu mpaka akome.
Kama ulipitia magumu kwenye utoto wako na ukapambana kufanikiwa, jua magumu hayo yalikuwa na mchango kwako kufanikiwa. Siyo lazima mtoto wako naye apitie magumu yale yale, lakini hakikisha kuna magumu anakabiliana nayo.
Huenda wewe ulikosa ada ya shule au mahitaji muhimu ya shuleni, haimaanishi na mwanao naye akose ada ya shule, lakini siyo lazima kila sherehe ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwake ifanyike shuleni au kwa ukubwa nyumbani kwa sababu kila mwanafunzi mwenzake anafanya hivyo.
Watoto wanahitaji kujua pale wanapokosea na kujua kuna gharama ya kukosea, hivyo wanapokosea na wasiadhibiwe wanajifunza kwamba dunia inawasujudu wao, kitu kisichokuwa sahihi, kwa sababu watakapotoka kwenye mikono yako inayowafunika, dunia itawaadhibu vya kutosha. Waandae mapema ili dunia isije kuwataabisha zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante Sana kocha kwa makala nzuri juu ya kulea watoto wetu ktk makuzi mazuri, lakini wote tumetokea kwenye utoto na hadi sasa tunaona dunia inavyotufundisha,kutuadhibu na kutujenga ktk uimara wa aina yake.
LikeLike
Ni kweli Beatus,
Tusiwazuie watoto kupitia yale tuliyopitia.
LikeLike
ukurasa muhimu na muhimu kwa kila mtu kuusoma juu ya malezi jinsi tunavyowalea watoto ukurasa umeshiba sana.kocha una mpango wa kutoa toleo la pili la kitabu cha hizi kurasa za maisha na kuuza kwa wengi kwan kuna maarifa sana yanayojibu changamoto nyingi kwenye jamii kupitia hizi kurasa.
LikeLike
Asante Hendry,
Ndiyo, nitazikusanya kurasa hizi kuwa vitabu.
LikeLike
Asante kocha,hili ni mhimu sana hata kwa sisi tulio katika maandalizi ya kuingia katika majukumu ya familia.Linatutahadharisha juu mambo mhimu sana kuzingatia
LikeLike
Karibu Alex
LikeLike