Pope Alexander aliwahi kunukuliwa akisema maarifa kidogo ni hatari kwa yule anayeyapata hivyo mtu anapaswa kuyanywa kwa kina maji ya chemchem ya maarifa au asiyaonje kabisa.
Wengi wamekuwa hawaelewi nukuu hiyo na ndiyo maana wanarudia makosa ambayo yamekuwa yakifanyika kwa miaka mingi.
Mara zote wale wanaojua kitu juu juu huwa ndiyo waongeaji sana, huwa ndiyo wanajiona ni wajuaji na wale wasiojua kitu hicho basi ni wajinga kabisa. Lakini wale wanaojua kitu kwa kina, kwanza wanajua ni jinsi gani hawajui na pili wanakuja kujua yote ni upuuzi (absurd) hivyo hawawashangai sana wasiojua.
Hii ipo hata kwenye imani, wale walioshikilia imani fulani juu juu ndiyo huwa hatari, huona wale wote ambao hawaamini kwenye kile wanachoamini wao wanapaswa kuadhibiwa kabisa. Wale walio na imani ya kina wanajua yalipo madhaifu ya imani yao na kwa nini wamechagua kuishikilia licha ya madhaifu hayo na hawawezi kuwahukumu wale wasioamini wanachoamini.
Funzo hapa ni kuwa makini na maarifa kidogo unayoyapata yasikufanye unajua zaidi kuliko wengine, kwamba wao ni wajinga na wewe tu ndiye mwerevu. Tafuta kujua zaidi na utaanza kuwaonea wivu wale wasiojua unayojua wewe, maana kadiri unavyojua ndivyo unavyoona mengi usiyojua. Hivyo fanya kujua kuwa wajibu wako na siyo kuhukumu wengine kwa ujuaji wako, kama mtu atapenda kujifunza msaidie, kama hataki usimlazimishe.
Kadhalika kwenye imani, tambua kile unachoamini wewe siyo sahihi zaidi ya wanachoamini wengine. Kinachowatofautisha watu kwenye vile wanavyoamini ni namna vinaendana na kile kilicho ndani yao. Kwa kuwa hujui kilicho ndani ya mtu, huwezi kumhukumu kwa kile anachoamini. Epuka kujiona wewe ni mtakatifu zaidi kwa sababu ya unachoamini na wale wasioamini hicho siyo watakatifu kama wewe. Ukiijua imani yako kwa kina, utawaonea wivu wale ambao hawajaijua kama wewe, maana utakuwa umejua vitu vinavyokutikisa na kukuweka njia panda, lakini vinakusaidia kuibeba imani hiyo kweli au kuachana nayo.
Kwenye jambo lolote lile, wale wanaojua juu juu ndiyo huwa wasumbufu kwa wengine. Lakini wale wanaojua kwa kina, hawana hata muda wa kuwasumbua wengine, maana wanajua ni kwa kiasi gani bado wanapaswa kujua.
Usikimbilie kuwasumbua wengine kwa chochote ulichokijua kwa juu juu, jipe muda na kuzama kwa kina zaidi, utaona jinsi ilivyo upuuzi kujisumbua na wengine.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante Sana kwa makala yenye maneno tafakarishi sana,kwanza nimeirudia mara nyingi kuisoma na nitairudia tena na tena, pia nimeinukuu kwenye daftari langu kubwa la mafunzo yangu,pia imenikumbusha”barua ya#07Tatizo ni huyo Ng’ombe wako aliekondeana”pia katika kitabu cha UNA NGUVU YA KUTENDA MIUJIZA CHA DR AMAN MAKIRITA,sura ya sita ukurasa wa 138,ukimsoma kamanda David Goggis ktk tangazo la vita,na anavyoelezea,jinsi tunavyotumia uwezo mdogo chini ya %40 ktk kazi zetu,lakini pia ktk kitabu hicho sura ya nne ukrsa wa 101,nukuu ya mwanasaikolojia Abraham Maslow skis email”pale zana pekee inayoonyesha nayo ni nyundo”kila kitu kinageuka kuwa msumari, tunahitaji kujifunza zaidi,kama ambavyo hatujui tunaendelea kujifunza basi nasi tusiwabeze au kuwadharau wasiojua.
LikeLike
Vizuri sana Beatus.
LikeLike