2447; Hakuna Kuchelewa.
Safari ya mafanikio huwa haina kuchelewa. Wakati wowote ambapo mtu unaamua unayataka mafanikio, ndiyo wakati sahihi kwako kuyafanyia kazi na kuyapata.
Wapo ambao huona kwa sababu umri umekwenda na wamechelewa kujitambua kwenye eneo la mafanikio basi hawawezi tena kupata mafanikio makubwa.
Hiyo siyo kweli, kama tu unaweza kufikiria mafanikio makubwa, basi ipo ndani yako kuweza kuyapata mafanikio hayo.
Na jingine muhimu kabisa ni kila ambacho umewahi kupitia kwenye maisha yako ni rasilimali muhimu na unayoweza kuitumia kwenye safari ya mafanikio.
Hata kama umekuja kujitambua kimafanikio umri ukiwa umeenda, hujachelewa. Kila ambacho umepitia kwenye maisha yako mpaka ulipofika sasa, ni rasilimali ambazo ukiweza kuzitumia vizuri, utafanya makubwa.
Kuna mengi umefanya kwenye maisha yako na kushindwa au kutokupata mafanikio makubwa. Huo ni uzoefu mzuri ambao ukiutumia utaweza kufanya makubwa.
Kuna watu umejuana nao katika safari ya maisha yako ambao ni mtandao mzuri kwako kufanikiwa.
Kuna maeneo mbalimbali ambayo umepita na yamekupa mwanga mkubwa kwenye uelewa wako.
Zote hizo ni rasilimali muhimu sana kwenye safari yako ya mafanikio.
Unachohitaji ni kuzileta pamoja na kuweza kuzitumia kwa namna bora ili uweze kufanikiwa.
Kuianza safari ya mafanikio ukiwa na miaka 60, siyo sawa na anayeianza akiwa na miaka 30.
Kwenye miaka hiyo 60 hujachelewa, kwani kuna mengi unayokuwa umepitia ambayo mwenye miaka 30 hajapata nafasi ya kuyapitia.
Muhimu ni wewe kujua kila ambacho umeshapitia kwenye maisha yako ni rasilimali na unapaswa kuitumia vyema ili kupata mafanikio unayoyataka.
Safari ya mafanikio haina kuchelewa, wakati wowote unapokuwa tayari kuianza ndiyo wakati sahihi kwako.
Tumia kila ambacho umepitia kwenye maisha yako kama rasilimali muhimu kwenye hiyo safari na kwa hakika utafanikiwa.
Hatua ya kuchukua;
Jiulize ni maeneo gani ambayo unajiona kama umechelewa. Tambua leo kwamba hujachelewa, ila ulikuwa kwenye maandalizi muhimu.
Kaa chini na orodhesha kila uzoefu ambao umeshapitia kwenye maisha yako mpaka sasa na tumia kila uzoefu kama rasilimali ya kufika kwenye mafanikio unayotaka.
Iendee safari ya mafanikio ukitumia kila rasilimali uliyonayo na safari yako haitakuwa ndefu kama ya yule asiyekuwa na rasilimali kama zako.
Tafakari;
Wanasema mwanafunzi akiwa tayari, mwalimu huonekana. Siyo kwamba mwalimu hakuwepo, alikuwepo muda wote, ila kwa mwanafunzi kutokuwa tayari, hakuweza kumuona.
Kadhalika unapokuwa tayari kwa mafanikio ndiyo wakati sahihi kwako kuianza safari ya mafanikio. Hakuna kuchelewa, kwani kila ambacho umepitia yalikuwa ni maandalizi ya safari hiyo muhimu. Tumia yote uliyopitia kama rasilimali muhimu kwenye safari hiyo ya mafanikio.
Kocha.
Asante kocha
LikeLike
Karibu
LikeLike
Asante Sana kocha
LikeLike