2451; Kuna mahali pana breki.
Kama gari ina uwezo wa kwenda kwa kasi ya mpaka kilomita 200 kwa saa, ila ikawa inaenda kwa kasi ha kilomita 100 kwa saa, sababu zinaweza kuwa mbili.
Moja ni mafuta hayajakanyagwa kiasi cha kufika kasi hiyo ya juu.
Mbili ni breki zinakuwa zimekanyagwa na hivyo kuwa kikwazo kufikia kasi hiyo ya juu.
Hivyo pia ndivyo maisha yetu yalivyo.
Kama hupati matokeo makubwa unayojua unaweza kuyapata, sababu zinaweza kuwa mbili.
Moja ni huweki juhudi za kutosha ili kuweza kuzalisha matokeo hayo.
Na mbili ni kuna mahali unaweka breki na hiyo inazuia usipate matokeo unayotaka.
Wale wanaosema wamefanya kila kinachopaswa kufanyika ila bado hawapati matokeo, tatizo linakuwa kwenye breki.
Kuna breki fulani mtu anakuwa amejiwekea au ameruhusu wengine wamuwekee na hiyo ndiyo kikwazo cha mafanikio makubwa.
Breki zinaweza kuanzia ndani ya mtu, kutokana na fikra na hisia anazoweza kuwa nazo mtu.
Breki za ndani ni ngumu sana kuvunja kwa kuwa ni vigumu mtu kujua kwamba amejiwekea breki.
Na pia breki zinaweza kutoka nje ya mtu, kwa kuanzia kwa wale wanaomzunguka mtu, hasa anaoshirikiana nao.
Breki hizo huja kwa mfumo wa ukatishaji tamaa au ukwamishwaji unaosababishwa na wengine.
Tambua kama hupati unachotaka licha ya kuweka kila aina ya juhudi, kuna breki ndiyo kikwazo kwako.
Zijue breki hizo na ziachilie ili uweze kufanya makubwa.
Hatua ya kuchukua;
Fikiria kile ambacho unataka sana kukipata kwenye maisha yako na juhudi zote ambazo umekuwa unaweka ili kukipata. Kama juhudi ni kubwa ila matokeo ni madogo, tafuta ni wapi penye breki. Anzia ndani yako, kwenye mtazamo, fikra na hisia ulizonazo juu ya jambo hilo. Na pia nenda nje, ukiangalia wote unaoshirikiana nao kwenye jambo hilo kama kweli wanachangia lifanikiwe au wanakuwa kikwazo.
Bila kujua penye breki na kuziachilia, kuweka juhudi zaidi haisaidii.
Tafakari;
Kukanyaga mafuta zaidi ili kuongeza mwendo wa gari huku pia umekanyaga breki ni kupoteza nguvu bila ya manufaa yoyote. Kadhalika kuweka juhudi ili ufanikiwe wakati una vikwazo kwa mafanikio hayo ni kujihangaisha bure. Achilia kwanza breki ili juhudi unazoweka ziwe na tija.
Kocha.
Asante Sana kocha.
LikeLike
Karibu.
LikeLike