2486; Machaguo mengi.

Tuna bahati kubwa ya kuishi kwenye zama ambazo tuna machaguo mengi kwenye kitu chochote tunachofanya.

Hulazimiki kuchukua chochote kilichopo, bali una uhuru wa kuchagua kile unachotaka.

Tulidhani katika zama hizi za machaguo mengi wengi wangekuwa na furaha na mafanikio kutokana na uhuru mkubwa uliopo wa kuchagua.

Lakini mambo yamekuwa kinyume, watu wamekosa furaha na hata mafanikio kutokana na wingi wa machaguo.

Kwanza watu wanatumia muda mwingi kuchagua kuliko kufanya. Hilo limezalisha tabia sugu ya kuahirisha mambo au kusubiri mpaka kila kitu kiwe sawa.

Pili watu hawakai kwenye kitu kimoja kwa muda mrefu. Hata baada ya kutumia muda mwingi kuchagua, bado inakuwa rahisi kubadilika pale wanapoona kuna chaguo jingine bora zaidi. Kwa kushindwa kuwekeza muda na juhudi za kutosha kwenye kitu kimoja, wengi wanashindwa kufanikiwa.

Tatu watu wanachoka kwenye kuchagua kabla hata hawajaanza kufanya. Na wanachoka zaidi kwenye kuanza na kuacha mambo mengi bila ya kuweka juhudi kwenye machache.
Nguvu ile ile ambayo ingewekezwa sehemu moja ingezalisha matokeo mazuri, inaishia kutawanywa kwenye mambo mengi na kukosa ufanisi.

Kuwa makini na machaguo mengi yaliyo mbele yako, ni rahisi sana machaguo hayo kuwa kikwazo kwako kupiga hatua.
Jipe mkakati wa kufikia maamuzi mapema na kukaa na maamuzi hayo bila kuyabadili mara kwa mara.

Hatua ya kuchukua;
Kwenye machaguo mengi yaliyo mbele yako, pata utulivu na isikilize nafsi yako maana hiyo inajua nini hasa unachotaka.
Ukishaisikiliza nafsi yako, fanya maamuzi kisha kaa kwenye maamuzi hayo mpaka upate matokeo badala ya kubadili maamuzi hayo kila mara.

Tafakari;
Uhuru ni sumu kubwa kwa mtu asiyejua anachotaka na asiyekuwa na nidhamu binafsi. Maana ataishia kuhangaika na mengi yasiyo na tija kwake, kitu ambacho kinakuwa kikwazo kwake kufanikiwa.
Usifurahie tu uhuru, jiulize je unajua unachotaka? Na je una nidhamu binafsi ya kutosha kukomaa kwenye kitu mpaka kilete matokeo mazuri?

Kocha.