2498; Jenga Mtaji Wa Biashara.

Kuna changamoto moja kubwa ambayo naiona kwa watu wengi walio kwenye biashara ndogo, hasa za huduma.

Watu hawa wamekuwa wanaendesha biashara zao bila ya kuwa na mtaji. Wanasubiri wateja wawalipe na kisha kutumia kile wanacholipwa na wateja.
Halafu wanasubiri tena kupata wateja au kukipwa tena na wateja.

Hali hii ni mbaya na inamweka mtu kwenye wakati mgumu na kumfanya awe na tamaa, hivyo kulazimika kukubali kila aina ya kazi. Kwa sababu hana fedha na ana uhitaji wa fedha, hawezi kukataa kazi inayokuja mbele yake.

Kwa watu wanaofanya biashara za huduma, ambapo wateja wanawalipa wafanye kitu fulani, hudhani hawahitaji kuwa na mtaji, kwa sababu gharama zote zinatoka kwa mteja.

Lakini hiyo siyo sahihi, kila biashara inapaswa kuwa na mtaji, ili iweze kufanya mambo yake vizuri na mtu usisukumwe na tamaa na kuchukua kazi ambazo siyo sahihi.

Wakati mwingine hata kwenye biashara za bidhaa, mtu anaweza kutoa fedha ya mtaji na kufanyia mambo mengine ya nje ya biashara kabisa.
Hilo limekuwa linasababisha biashara iyumbe na kushindwa kusimama imara yenyewe.

Unapaswa kutenga kabisa mtaji wa biashara yako ni kiasi gani, kisha kuuweka kwenye biashara na kutokuuingilia.
Kadhalika kwa biashara ya huduma, hata kama hakuna unachonunua wewe, kuwa na mtaji wa kuiendesha kiasi kwamba wakati wote hutegemei kwanza malipo ya mteja ndiyo uweze kufanya kazi au kulipa gharama za biashara.

Hatua ya kuchukua;
Kwa biashara yoyote unayofanya, tenga kabisa kiasi cha mtaji unaopaswa kuwa kwenye biashara hiyo ili iweze kujiendesha vizuri bila ya kukupa tamaa ya kuhangaika na kila kazi.
Na ukishaweka mtaji kwenye biashara, acha kuuingilia kwa matumizi mengine binafsi au nje ya biashara.
Unahitaji kujijengea nidhamu ya hali ya juu sana kwenye eneo hili la fedha za biashara, la sivyo biashara itakuwa kitu kigumu sana kwako.

Tafakari;
Biashara ni mtaji. Biashara isiyo na mtaji siyo biashara, ni hobi tu na hobi haiwezi kukua na kukupa manufaa makubwa.

Kocha.