2605; Kujua Hujui.
Akili ni kujua.
Hekima ni kujua hujui.
Mwanafalsafa Socrates, mtu anayechukuliwa kuwa na hekima sana kuwahi kuishi hapa duniani aliulizwa swali, kwa nini wewe una hekima sana?
Majibu yake; kwa sababu najua sijui.
Jibu fupi lakini limebeba maana kubwa sana.
Ukiamini unajua, huna tena nafasi ya kujifunza.
Na kwenye dunia yenye mengi kuliko unavyoweza kujua, utakuwa umeanza kuanguka.
Ukiamini kwamba hujui, unakuwa mnyenyekevu na kuendelea kujifunza kwa umakini.
Na hilo linakupa fursa ya kujifunza mengi zaidi.
Kadiri unavyojifunza mengi, ndivyo pia unavyokuwa na hekima.
Hatua ya kuchukua;
Pale unapojiambia tayari unakijua kitu, ndiyo wakati wa kuweka umakini mkubwa wa kujifunza kitu hicho.
Hata kama ni marudio, wewe jifunze kwa umakini, kuna vingi utavijua ambavyo hukuwa unajua kwamba hujui.
Tafakari;
Unapojifunza kitu kwa mara ya pili, au mara nyingine yoyote haiwi marudio, bali inakuwa fursa mpya zaidi ya kujifunza. Maana hauwi mtu yule yule aliyejifunza kitu hicho kwa mara ya kwanza.
Wanasema hakuna mtu mmoja anayeweza kuvuka mto mara mbili, maana kwa mara ya pili hawi mtu yule yule na mto hauwi ule ule.
Kadhalika hakuna mtu mmoja anayeweza kusoma kitabu mara ya pili, maana mara ya pili hawi mtu yule yule na kitabu hakiwi vile vile.
Kocha.