2612; Kushughulika na watu.
Changamoto na migogoro mingi unayokutana nayo kwa watu wengine vinatokana na wewe kusahau jambo hili la msingi kabisa.
Kwamba binadamu ni viumbe wa kihisia na siyo viumbe wa kimantiki.
Kwamba wanafanya maamuzi yao kwa hisia na kisha kuyahalalisha kwa mantiki.
Na kubwa kabisa ni kwamba hisia huwa hazidumu, zinapita kama upepo.
Na zaidi, hatuwezi kuzielezea hisia zetu kwa usahihi.
Ndiyo maana mara nyingi unapowauliza watu kwa nini wamefanya kitu fulani, watakupa sababu ambayo haina hata mashiko, kwa sababu hawawezi kuelezea hisia walizokuwa nazo.
Je hakuba kabisa tumaini kwetu wanadamu kwa sababu ni viumbe wa kihisia?
Jibu ni hapana, tumaini lipo.
Ndiyo maana kuna sheria na tararibu mbalimbali tunazolazimika kuzifuata, lengo ikiwa ni kuzuia hisia zetu zisilete madhara mabaya.
Hata nchi inakuwa na katiba na sheria, ambazo zinapaswa kufuatwa na kila mtu bila kujali nafasi yake.
Pale mtu anapokwenda kinyume na hayo, madhara hutokea.
Sasa unaweza kuona kwa nini unapitia changamoto nyingi kwenye biashara yako pale unapoajiri watu wengine kuliko ulivyokuwa peke yako.
Ni kwa sababu ya hisia za watu.
Na unapokuwa huna utararibu, sheria na misingi mbalimbali inayopaswa kufuatwa na kila mtu, unakuwa umejiweka mahali pagumu sana.
Hatua ya kuchukua;
Kwenye mambo yote unayoshughulika na watu wengine, weka wazi kabisa misingi, sheria na taratibu zinazopaswa kufuatwa na kila mtu.
Bila ya hayo mambo yataendeshwa kwa hisia na migogoro haitakoma.
Kadhalika kwenye maisha yako binafsi, jiwekee misingi, sheria na taratibu ambazo utazisimamia mara zote bila kujali hisia unazokuwa nazo.
Hiyo ndiyo njia pekee ya kuvuka udhaifu wetu binadamu.
Tafakari;
Hisia zinazosukuma kufanya makubwa, ndiyo hizo hizo zinazokuwa kikwazo kikubwa kwetu kama hatuna mkakati mzuri.
Usikubali kupotezwa na hisia zako, badala yake zitumie kwa manufaa makubwa kwako.
Kocha.