2677; Kutenganishwa na fedha zako.
Jana mtu wa karibu sana alinipigia simu akinieleza ametapeliwa kiasi fulani cha fedha alichokuwa nacho.
Ni wiki moja kabla alinipigia simu akinieleza kiasi cha fedha alichopata na akiwa hana uhakika afanye nini.
Ushauri wangu kwake ulikuwa rahisi, nilimwambia hiyo fedha asikimbilie kuitumia kwa namna yoyote ile.
Atulie kwanza wakati anafikiria nini afanye.
Na pia nilimtaka asijionyeshe kama ana fedha, yaani mtu yeyote asijue kama ana fedha hizo, maisha yake yaendelee kama vile hana fedha hizo alizopata.
Wakati ananipigia jana nilimuuliza ni kiasi gani ametapeliwa, akanijibu ni nusu ya alichokuwa nacho.
Nikamuuliza nusu nyingine imeenda wapi, akanijibu alishaanza kutumia.
Kitu kikubwa nilichojifunza kwenye hili ni rahisi sana kuwatenganisha watu na fedha zao.
Nguvu kubwa sana inatumika kuhakikisha watu wanatenganishwa na fedha zao.
Kuanzia matangazo ya biashara, watu wenye uhitaji, matapeli na hata fursa mpya zinazokuja kwako pale unapokuwa na fedha.
Hii vita ni kali, kuishinda siyo rahisi, maana maadui ni wengi na wana silaha kali za ushawishi.
Kuna njia kuu mbili za kuweza kujilinda na hatari hii ya kutenganishwa na fedha zako.
Njia ya kwanza ni usiwe na fedha.
Yaani hapa hakikisha huwi na fedha ambazo zipo zipo tu.
Kwa kila kipato unachoingiza, tenga fedha ya matumizi ya msingi tu. Nyingine yote iende kwenye akaunti maalumu ambapo huwezi kuitoa.
Huko inajikusanya baadaye unaiwekeza.
Yaani muda wote kaa umefulia, huwezi kutenganishwa na fedha ambazo huna.
Njia ya pili ni usiwaonyeshe watu una fedha.
Usiwe rahisi kutabirika una fedha au huna. Yaani wakati wote kuwa kwa namna ile ile, ambayo watu hawajui kama una fedha au huna.
Wengi huwa hawaliwezi hili, wakiwa na fedha kila mtu anajua wana fedha.
Ukiwa na tabia ya kutabirika kama una fedha, unakaribisha wale wenye hila za kukutenganisha na fedha zako.
Hakuna kitu kinachowapa watu hao nguvu kama pale wanapokuwa na uhakika kwamba una fedha.
Epuka hilo kwa kuhakikisha hali yako ya kifedha haijulikani au kutabirika na yeyote.
Hatua ya kuchukua;
Muda wote kaa ukiwa umefulia, kwa kila kipato chako cha ziada kiweke kwenye gereza ambapo huwezi kukitoa kisha kipeleke kwenye uwekezaji.
Usiwaambie wala kuwaonyesha watu kwamba una fedha. Mara zote onekana umefulia ili kuwakatisha tamaa wale wanaotaka kukutenganisha na fedha zako.
Tafakari;
Kama hutazipenda fedha zako, wapo watakaozipenda zaidi na kwa mapenzi hayo makubwa waliyonayo watakutenganisha nazo.
Inapokuja kwenye swala la fedha, kuwa na tahadhari kubwa, kila mtu anatafuta njia ya kukutenganisha na fedha zako.
Kocha.
Ok Noted coach
Fedha iliyo ipo ipo tu ni rahisi kuipoteza,mwisho unakuja kushtuka imeshapungua sana ndo akili inakaa sawa.
Nisiwe mrahisi kutabirika wakati gani nina fedha wakati gani sina fedha hili litaepusha mengi yanayowafanya watu wanitenganishe na fedha yangu.
LikeLike
Kabisa.
LikeLike