2771; NA, NA, NA.

Ugumu au ufahisi wa kufanya jambo lolote unategemea sana na wingi wa NA kwenye mambo unayoyahitaji.

Kadiri NA zinavyokuwa nyingi, ndivyo inavyokuwa vigumu zaidi kufanya kitu.

Kwa mfano ukijiambia ukifika stendi ya basi utapanda basi linalokwenda Arusha, hapo unakuwa na uwanja mpana wa kuchagua na hivyo kukamilisha kirahisi.
Lakini ukijiambia unataka ukute basi NA iwe nyekundu NA iwe inaendeshwa na mwanamke, machagua yanakuwa machache au hayapo kabisa.

Unajionea hapo jinsi ambavyo kuwa na NA nyingi kunavyofanya kitu kiwe kigumu kufanya.

Hivyo kama unataka kufanya kitu, ondoa NA na uweke AU.
AU inaongeza uwanja wa machaguo na unakuwa na fursa nyingi zaidi za kufanya.

Kama unataka kujijengea tabia yoyote ile, jiwekee masharti rahisi ya kufanya. Ondoa NA zote unazojiwekea ambazo zinakuwa kikwazo.

Kwa mfano kama unataka kujenga tabia ya kuandika au kufanya mazoezi kila siku, jiambie ukiamka unaandika/unafanya mazoezi. Hilo linakupa uwanja mpana wa kutekeleza kile ulichopanga.
Lakini ukiweka NA nyingi, kwamba ukiamka NA ukiwa unajisikia vizuri NA ukiwa na vifaa NA hali ya hewa ikiwa nzuri basi utaandika/kufanya mazoezi.
Wingi huo wa NA unapunguza uwezekano wa kitu kufanyika kwa sababu inakuwa vigumu kwa masharti unayokuwa umeweka kutimia.

Badala ya kusubiri mpaka kila kitu kiwe sawa ndiyo ufanye, wewe fanya kwa kutumia chochote kinachopatikana kwa wakati huo.

Hatua ya kuchukua;
Ni NA ngapi umejiwekea kwenye kufanya kile muhimu kwako kufanya kila siku ili kufanikiwa?
Punguza hizo NA ili ujiondolee vikwazo ulivyojitengenezea na vinavyokuzuia usiweze kufanya kila siku kama unavyopaswa kufanya.

Tafakari;
Dunia haiwezi kuwa kama vile tunavyotaka sisi. Hivyo kujiwekea vigezo na masharti mengi yanayopaswa kutimia ndiyo uweze kufanya ni kujizuia kufanya.
Kufanya ndiyo kinapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza kwako, hivyo usikubali chochote kukuzuia kutekeleza hilo.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed