Sikiliza hapa;
Rafiki yangu mpendwa,
Maamuzi yote tunayofanya kwenye maisha yetu huwa ni kwa ajili ya kuboresha hali tulizonazo. Kila tunachofanya, ni kwa sababu tunaamini tutakuwa bora zaidi kwa kukifanya kuliko kutokukifanya.
Hata pale tunapofanya kitu ambacho kinakuwa na madhara, bado tunakuwa tumeamini kwamba tutakuwa bora zaidi kwa madhara hayo kuliko kutokufanya. Hivyo ndivyo akili zetu binadamu zinapofanya maamuzi, hasa katika hali ya mazoea.
Kuna vitu viwili ambavyo ndiyo tunavitaka sana na vinavyosukuma maamuzi yetu yote; Uhuru na Furaha. Mambo yote tunayokazana kufanya ni kwa sababu tunataka kuwa huru zaidi na tunataka kuwa na furaha.
Unaweza kushangaa, kama uhuru na furaha ndiyo vitu vinavyotusukuma, mbona maamuzi yetu mengi yanaishia kutunyima vitu hivyo? Ukichunguza maamuzi yote ambayo umekuwa unafanya, unaona kabisa matokeo yake yamekunyima uhuru na furaha unayokuwa unataka.
Na hapo ndipo tatizo letu binadamu lilipo. Pale tunapofanya mambo yetu kwa mazoea, badala ya kufikiri kwa usahihi, tunaishia kupata matokeo ambayo siyo bora kwetu. Tunafanya tukiwa na nia njema kabisa, lakini kwa sababu namna tunavyofanya siyo sahihi, matokeo tunayokuja kupata yanakuwa siyo sahihi.
Kwenye barua hii tunaenda kuangalia jinsi ambavyo tumekuwa tunajitengenezea matatizo mengi na ambayo yanatukwamisha kwenye malengo makuu mawili ya uhuru na furaha. Na tutajifunza kitu kimoja ambacho kinaweza kuondoa sehemu kubwa ya matatizo hayo, ili tuweze kuwa na uhuru na furaha kwenye maisha yetu.

1. Mara Zote Tunataka Tusichokuwa Nacho
Ikiwa huna chombo chochote cha usafiri, ukimwona mwenye baiskeli utasema ukipata baiskeli maisha yako yatakuwa nafuu.
Unakazana na kupata baiskeli, unaona maisha yako yamekuwa nafuu. Lakini unapoona wenye pikipiki, unaona wewe unatumia nguvu nyingi na huwezi kubeba mzigo au mtu. Unaona ukiwa na pikipiki, maisha yako yatakuwa nafuu.
Unakazana na kupata pikipiki, na kweli hutumii tena nguvu nyingi. Lakini unapoona wenye magari unaona wewe haupo salama kwenye pikipiki. Unaona ukiwa na gari maisha yako yatakuwa nafuu.
Unapata gari, labda ndogo, unaona unahitaji kubwa zaidi. Baadaye utahitaji ndege, boti n.k.
Hivyo ndivyo akili yetu sisi binadamu inavyokuwa. Kuna kitu tunakuwa tunakitaka sana, tunakazana kukipata, lakini tukishakipata, tunaangalia ambacho hatuna.
Hilo siyo tatizo lako binafsi, au kukosa shukrani, ni asili yetu binadamu. Na iko hivyo kwa maana kubwa, iliwaaidia watangulizi wetu kuhakikisha wanakuwa salama kwenye mazingira ambayo hayakuwa na usalama.
Kabla ya kuja kwa maendeleo makubwa tunayoyaona sasa, maisha ya wanadamu yalikuwa duni sana. Kuridhika na kitu chochote ilikuwa ni hatari. Hivyo akili zetu zimeumbwa kuangalia nini ambacho hatua na huo kuwa ndiyo wajibu wetu, kuhakikisha tunakazana kukipata.
Pamoja na kwamba ni asili yetu, hatupaswi kuyaendesha maisha yetu kwa namna hiyo. Hasa pale kutaka tusichokuwa nacho kunapotufanya tutengeneze matatizo yanayotukwamisha kupata uhuru na furaha.
2. Umeshapata Kila Ulichosema Kitakupa Uhuru na Furaha
Ulipokuwa mtoto, ulikuwa unapangiwa kila kitu na wazazi. Uliona ukiwa mtu mzima na kujipangia mambo yako mwenyewe, utakuwa huru na mwenye furaha. Sasa umekuwa mtu mzima, vipi uhuru na furaha?
Ulipokuwa shuleni, uliona ukishahitimu na kupata kazi au biashara, utakuwa na maisha mazuri na kuwa na furaha. Sasa umeshatoka shuleni, una kazi/biashara, vipi uhuru na furaha?
Ulipokuwa na kipato kidogo, uliona ukikuza kipato chako utakuwa huru na mwenye furaha. Umekuwa unaongeza kipato chako, vipi uhuru na furaha?
Rafiki, naweza kuorodhesha maengi ambayo tayari yameshatokea kwenye maisha yako, lakini kile ulichotarajia hakijaenda hivyo.
Kama ambavyo tumeona, kila tunachofanya ni kwa ajili ya uhuru na furaha. Na hapo ulipo sasa, ni wewe umejifikisha hapo. Kwa hatua ulizochukua huko nyuma, ndiyo umefika hapo ulipo. Kwa maana nyingine, hapo ndipo ulitaka kuwepo.
Swali ni je umepata uhuru na furaha kama ulivyokuwa unatarajia? Katika hali ya kawaida na kwa walio wengi, uhuru na furaha bado ni vitu vinavyoonekana kuwa mbali. Na hiyo ni kwa sababu mambo mengi yanafanywa kwa mazoea na siyo kwa kufikiri kwa usahihi.
Yote uliyofanya mpaka sasa ni sahihi kabisa, lakini hayakupi matokeo uliyotarajia, kwa sababu hayaendani na matokeo hayo. Ndiyo maana utaona, kwenye matokeo hayo hayo uliyonayo wewe na hayajakuridhisha, kuna mwingine anatamani sana angekuwa nayo. Au kuna mwingine tayari anayo na yanamridhisha.
Wengi sana wamekuwa wanakazana kuongeza mwendo kwenye safari ya maisha, wakati uelekeo wao unakuwa sahihi. Hilo ndiyo linafanya wapate matokeo, lakini wasiridhike nayo. Kwa sababu matokeo hayo hayaendani na wao moja kwa moja.
Na mtego mkubwa kwenye hili unaanzia kwenye jamii, ambayo inawashawishi watu wafuate mkumbo, kwa kuiga yale ambayo wengi wanayafanya wakidhani ndiyo sahihi.
Tunapaswa kutambua na kuvuka huo mtego ili tuweze kuepuka na kutatua matatizo mengi ambayo tunajitengenezea sisi wenyewe.
3. Suluhisho La Tatizo Ni Tatizo
Robert Kiyosaki amewahi kusema; “Kuna matatizo mawili ya fedha, kutokuwa nazo za kutosha na kuwa nazo nyingi.” Kauli hii ina ukweli sana, na siyo kwenye fedha tu, bali kwenye kila kitu. Unapokuwa huna kitu ni tatizo, na unapotatua tatizo hilo na ukawa na hicho kitu nalo linakuwa tatizo.
Endelea kusoma suluhisho hilo kwenye #BaruaYaKocha hapa; #BZK077; Suluhisho La Sehemu Kubwa Ya Matatizo Yako, Taka Ulichonacho