Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Kama mpaka sasa bado hujanielewa vizuri, ni kwamba nina aleji na kitu kimoja tu hapa duniani, kushindwa. Nimekuwa naamini, bila ya shaka yoyote ile kwamba kila kitu kinawezekana. Ndiyo, kila kitu. Lakini sasa naboresha imani hiyo, kwa sababu kuna kitu kimoja nimegundua hakiwezekani, ambacho ni kushindwa.
Hivyo imani yangu ni mpya ni kila kitu kinawezekana isipokuwa kushindwa. Ndiyo, kushindwa ndiyo kitu pekee ambacho hakiwezekani kabisa. Naweza nisipate matokeo ambayo nilikuwa nayataka, lakini hayo ni matokeo, siyo kushindwa. Siwezi kushindwa kamwe, hiyo ndiyo imani kuu na msimamo wangu ambao hauwezi kuyumbishwa na chochote.
Na kama kuna kitu kimoja ambacho nakazana kukuambukiza, kupitia barua hizi ni hiyo imani na huo msimamo. Ukishaweza kuamini na kusimamia hivyo, bila kuyumbishwa na kitu chochote, mafanikio makubwa ni yako.
Na tuwe tu wakweli, hii siyo shughuli rahisi. Umezungukwa na ushahidi mwingi wa kushindwa. Sababu na visingizio vya kushindwa tayari unavyo, ni wewe tu uchague unataka kutumia ipi itakayokufariji zaidi na kukuokolea muda wa kujieleza sana.
Inanikumbusha kichekesho kimoja nimewahi kukisoma kwenye kitabu kinachohusu usimamizi wa wafanyakazi. Meneja mmoja alikuwa na tatizo sugu la uchelewaji wa wafanyakazi na kila mtu aliyechelewa alikuwa na maelezo mengi ya kutoa. Ili kuokoa muda akaorodhesha sababu zote ambazo watu wamekuwa wanatoa na kubandika ukutani. Mtu alipochelewa alimwambia nitajie namba ya sababu yako na uende. Inachekesha kama wewe siyo meneja mwenye wafanyakazi wachelewaji.
Sawa, hiyo siyo mada ya barua hii, ni mfano tu wa kukupa msisitizo jinsi ambavyo sababu za kushindwa tayari zipo, ni wewe uchague. Na utaona kwa nini wengi wanashindwa, wakati kushindwa ni kitu ambacho hakipo. Kwa sababu ya urahisi wa kupatikana kwa sababu, watu wanachukua hizo ili wasiwe na maelezo mengi ya kutoa.
Kuamini tu kwamba kushindwa hakuwezekani haitoshi kukupa mafanikio makubwa. Imani inahitaji matendo, na barua hizi zimejikita kukupa matendo, yenye ushahidi, ambayo ukiyafanya unapata matokeo.
Kwenye barua hii tunaenda kuangalia mkakati rahisi sana wa Rockerfeller, ambao unaweza kumpa mtu yeyote matokeo makubwa kwenye jambo lolote analofanya.

1. Mkakati Wa Rockefeller Unaoleta Matokeo Makubwa.
John D Rockefeller ni mmoja wa watu matajiri sana kuwahi kuwepo hapa duniani. Aliweza kujenga utajiri wake mkubwa kwenye sekta ya kusafisha na kusafirisha mafuta, kupitia kampuni ya Standard Oil.
Rockefeller hakufikia mafanikio hayo makubwa kwa kurithi au kusaidiwa. Alizaliwa kwenye familia masikini, kwa baba ambaye alikuwa mganga tapeli. Hakuwa na uwezo mkubwa darasani, alikuwa mzito kuelewa kwa haraka na hivyo ilimlazimu kujifunza kwa juhudi sana.
Kwa uzito wake kwenye kujifunza, hakuhangaika sana na elimu ya juu. Badala yake alipata kozi fupi ya ukarani na uhasibu na akiwa na miaka 16 aliingia mtaani kutafuta kazi. Kwa sababu hakutoka familia tajiri na wala hakuwa na koneksheni, zoezi la kupata kazi halikuwa rahisi.
Ili kuhakikisha anatimiza hilo, alitengeneza mkakati ambao uliweza kumpa kazi yake ya kwanza na akawa anaendelea kutumia mkakati huo hata alipoingia kwenye biashara.
Mkakati wa Rockefeller ulikuwa hivi; Aliorodhesha biashara zote kubwa zilizokuwa kwenye mji aliokuwepo ambapo aliona ni sehemu sahihi kwake kuanzia kazi. Kisha akaanza kutembelea biashara moja baada ya nyingine.
Alifika kwenye kila biashara na kuulizia kukutana na bosi, na alipompata na hata kutokumpata, aliongea na yeyote aliyeweza kumsikiliza. Maelezo yake yalikuwa mafupi; “Naelewa uhasibu, ningependa kupata kazi.” Alipoambiwa hapana, ambacho ndiyo alisikia kutoka kwa wote, alienda kwenye biashara iliyofuata kwenye orodha yake.
Alifanya hivyo kwa biashara zote alizoorodhesha mpaka orodha ilipoisha, kisha akarudia tena awamu ya pili. Akarudi kwenye kila biashara na kutoa maelezo yake, akapokea hapana mpaka orodha ikaisha. Akarudia tena awamu ya tatu na siku moja akafika kwenye biashara iliyokuwa na uhitaji wa karani, akapewa nafasi ya kujaribu kazi na akaifanya kwa weledi mkubwa. Akaajiriwa siku hiyo hiyo.
Kwa maisha yake yote, Rockefeller alikuwa akiisherekea siku hiyo ya tarehe 26 Septemba, aliyoiita siku ya kazi. Aliisherekea kuliko hata siku yake ya kuzaliwa, kwa sababu ndiyo siku iliyofungua milango ya mafanikio yake makubwa.
Wakati Rockefeller anafanyia kazi mkakati huu alikuwa na miaka 16 tu, na hakuna na namna nyingine bali kupata kazi kama sehemu ya yeye kuanzia.
Tunauona hapo mkakati wa Rockefeller, ambao kila mtu anaweza kuufanyia kazi na kupata matokeo. Mkakati huo una hatua nne;
Moja; jua kwa hakika kile unachotaka, ambacho huna mbadala bali kukipata.
Mbili; tengeneza orodha ya hatua za kuchukua ili kupata unachotaka.
Tatu; fanyia kazi orodha yako mpaka upate matokeo unayotaka, bila kuacha.
Nne; pata matokeo unayotaka.
Rafiki, hebu niambie tu wewe mwenyewe, ni kwa namna gani mkakati kama huo, ukifanyiwa kazi kwa uhakika utashindwa kuleta matokeo? Na je ni mara ngapi umekuwa na mkakati rahisi kama huo na kuufanyia kazi kwa uhakika?
Kitu kimoja kitakachokushangaza sana ni kwamba mkakati huu ulifanyiwa kazi na kuleta matokeo mwaka 1855, lakini ni mkakati unaoweza kufanya kazi nyakati zozote zile. Licha ya maendeleo makubwa ya kiteknolojia ambayo yameshatokea, bado mkakati huo unaweza kumpa matokeo mazuri mtu yeyote atakayeufanyia kazi.
Kabla hujasema umepambana sana na hujapata matokeo, onyesha orodha yako unayofanyia kazi na tuambie umefanyia kazi mara ngapi. Ukiangalia kwa upande huo, utaona mwenyewe kuna kazi hujafanya kwenye kupata matokeo unayotaka.
Kwenye #BaruaYaKocha nimekushirikisha mambo mengine manne ya kufanyia kazi mkakati huo wa Rockefeller, pamoja na mifano ya jinsi yeye mwenyewe alivyoutumia kupata matokeo.
Soma barua hiyo hapa; #BZK075; Mkakati Huu Wa Rockefeller Utakupa Matokeo Makubwa Kwenye Jambo Lolote Unalofanya.