Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Barua hii imekuja na kichwa kikali, kwamba ‘nitakuua’, kwa sababu inafika mahali ambapo ni lazima tuambiane ukweli kuhusu hii safari ambayo tupo. Ni lazima tujue kama kweli tupo kwenye safari tukimaanisha au tupo tukifurahia. Lazima tujue kama wote tupo kwenye hii safari kama sehemu ya kazi au kuna ambao tupo kama sehemu ya utalii.

Naandika haya siyo kwa kulalamika, wala ishara ya kukata tamaa. Bali ni kwa ajili ya kunyoosha mambo yakae sawa, kuchora mstari ambapo mtu anapaswa kuchagua anakaa upande upi. Ni kuhakikisha aliye ndani yupo ndani kweli na hakuna wasiwasi juu yake. Na asiye na uhakika basi anakaa nje mpaka pale anapopata uhakika.

Rafiki, tunaletwa pamoja na kitu kimoja tu, NJAA YA MAFANIKIO MAKUBWA. Na japo mafanikio yana maana tofauti kwa kila mtu, kuna mambo matatu ambayo ni lazima yatokee kwako kwa kuwa ndani ya hii Jumuia ya Washirika Wa Mafanikio.

Ni lazima UJENGE TABIA NA NIDHAMU sahihi, ambazo zinayafanya maisha yako kuwa huru na ya furaha. Kwa namna unavyoishi isiwe kikwazo kwako kuwa na maisha ya mafanikio unayotaka.

Ni lazima UJENGE UTAJIRI NA UHURU WA KIFEDHA, kwa namna ambayo maisha yako yanaweza kwenda bila kuathiriwa na chochote. Kiasi halisi kinaamuliwa na aina ya maisha unayochagua, lakini ni lazima uwe na kipato, uwe na akiba ya dharura na uwe na uwekezaji unaotosha kuendesha maisha yako yote hapa duniani.

Ni lazima UJENGE BIASHARA INAYOJIENDESHA BILA KUKUTEGEMEA MOJA KWA MOJA. Kwa sababu biashara ndiyo njia huru ya mtu kuingiza kipato, ni lazima uwe nayo. Na inapaswa iweze kujiendesha kwa kila kitu bila kukutegemea wewe moja kwa moja.

Hayo matatu ni LAZIMA YATOKEE, siyo kwa haraka, wala kwa mara moja, lakini lazima kila unachofanya kiwe kinachangia kukupeleka kwenye hayo matatu.

Na hayatatokea kwa kubahatisha, bali kwa kufanyia kazi kanuni yetu, ambayo imekuwa inafanya kazi kwa uhakika kabisa. Kanuni hiyo ni MAARIFA + VITENDO = MAFANIKIO.

Eneo la MAARIFA halina uhaba kabisa. Nimekuwa nakuandikia barua hizi kila siku, kuna vitabu, kuna dakika za kocha, kuna ongea na kocha na mafunzo mengine mengi. Na bado nje ya jumuia hii unaweza kupata mafunzo kadiri ya unavyotaka.

Eneo la VITENDO lipo ndani ya udhibiti wako wewe. Utayapata maarifa, lakini kuamua kuyaweka kwenye vitendo au la, wewe ndiye mwenye mamlaka hiyo. Hayupo yeyote anayeweza kukulazimisha wewe uweke kwenye vitendo yale unayojifunza, ili upate matokeo unayotaka.

MAFANIKIO siyo kitu kinachotokea mara moja, ni matokeo endelevu, ambayo yanapatikana kila unapopata MAARIFA na ukayaweka kwenye VITENDO. Kwa maana hiyo hakuna siku moja ambayo ndiyo utayapata mafanikio yote unayoyataka. Bali kila siku ni siku ya mafanikio, kama tu utajifunza vitu vipya na kuvifanyia kazi kwa vitendo.

Na hapo sasa ndipo linapokuja povu langu na kukuua. Kama kichwa cha barua hii kinavyosema, nikikuona unalalamika hufanikiwi, kwa maana kwamba huridhiki na maisha uliyonayo, wakati pia huchukui hatua kwenye haya tunayojifunza, nitakuua.

Sasa nielezee huko kukuua kabla hujapiga simu polisi na kusema umetishiwa maisha. Simaanishi kukuua kimwili, hilo siwezi kufanya kabisa. Bali nitakuua kwenye maisha yangu, nitakufuta kabisa kwenye fikra zangu. Nitakuchukulia ni mtu ambaye haupo tena. Kama kuna kumbukumbu nzuri tumewahi kuwa nazo pamoja nitazitunza, kama mtu ambaye umewahi kuwepo. Lakini sitakuhesabia tena kama mtu ambaye upo kwenye safari ya mafanikio.

Na kama unavyojua, mtu akifa hafufuki, hivyo nikishakuua kwenye safari yetu ya mafanikio, maana yake huwezi kurudi tena. Na kunakuwa hakuna sababu ya kurudi, kwa sababu hakikuwa kitu chenye thamani kwako. Inawezekana ulipenda, kama sehemu ya kujifurahisha, lakini unapoenda kwenye jambo ambalo wengine wameweka maisha yao na wewe unaenda kujifurahisha, unakuwa hatari kwa walioweka maisha yao yote.

Na ieleweke, nikikuua kimafanikio simaanishi kwamba huwezi tena kufanikiwa. Sijachanganyikiwa kiasi hicho cha kuamini mimi ndiye mgawa mafanikio. Bado unakuwa na fursa za kufanikiwa, kwa sababu njia zipo nyingi. Ila kwa njia yetu, huenda haijaendana na wewe. Na hakuna ubaya wowote kwenye hilo.

Na zaidi, nitakapokuua kimafanikio, haimaanishi kwamba siwezi tena kushirikiana na wewe kwenye jambo jingine. Haimaanishi tukikutana hatuwezi kusalimiana. Sisi ni binadamu, maisha mengine lazima yaendelee. Ila kwa haya mapambano makubwa ambayo wengi wetu tumeweka maisha yetu yote, ndipo unapokosa nafasi.

Naamini tumekaa sawa hapo, sasa karibu kwenye barua, upate ufafanuzi wa kwa nini barua hii imekuwa kali kuliko nyingine zote.

1. Hotuba Ya Kocha Pep Guardiola Iliyonisukuma Kuandika Barua Hii

Rafiki, kuna vitu unaweza kuwa unavifikiria kwa muda mrefu, lakini hupati maneno mazuri ya kuviweka. Halafu unakuja kukutana na kitu ambacho kinakupa maneno mazuri ya kueleza kile ambacho umekuwa unafikiria.

Mimi siyo shabiki wa mpira wa miguu na wala sifuatilii kabisa mchezo wa aina yoyote ile. Lakini kitu chochote kinachohusu mafanikio kinapotokea kwenye eneo lolote, lazima nitakijua. Maana akili yangu muda wote inakamata mawimbi ya kila kinachohusu mafanikio.

Hivi karibuni nimekutana na filamu ya makala inayoitwa A beautiful Obsession, ambayo inahusu maisha ya Kocha Pep Guardiola kwa miaka 10 ambapo alikuwa anafundisha timu ya Manchester City.

Kwa kipindi hicho cha miaka 10, aliweza kuibadili kabisa timu hiyo na kuipatia makombe 20, ambapo sita ni ya ligi kuu ya Uingereza. Filamu hiyo, ambayo inaonyesha matukio halisi ya safari ya kocha huyo, ina mengi sana ya kufundisha na kuhamasisha kwenye safari ya mafanikio.

Moja ya eneo ambalo limenasa sana umakini wangu na kunipa maneno mazuri ya kuweka kile ambacho nimekuwa nafikiria ni hotuba yake baada ya timu yake kufungwa. Naiweka hotuba hiyo hapa kwa tafsiri isiyo rasmi ya Kiswahili;

Hotuba ya Pep Guardiola kwenye chumba cha kubadilishia nguo baada ya Manchester City kufungwa 0-2 na Bayer Leverkusen katika Ligi ya Mabingwa, Novemba 2025

Kutoka kwenye filamu ya makala A Beautiful Obsession.

“Labda ninapaswa kuomba msamaha kwa kufanya mabadiliko 10.

Haiwezekani kucheza mpira wa miguu bila ujasiri, lakini jamani, aisee! Kila mmoja anapaswa kuonesha: “Mimi ndiye bora. Nitamwonesha huyu kocha mshenzi kwamba mimi ni bora kuliko wengine.”

Ninajiona mjinga sana. Ninafika hapa saa mbili asubuhi na kukaa kwa saa nyingi nikijaribu kutafuta kitu ambacho kitagusa moyo wako.

Nataka kuwaonesha kwamba ninaipenda kazi yangu na ninataka kuwapa upendo huo, lakini ninyi hamnirudishii chochote, jamani.

Na mnajua nini kitatokea?

Mtapata kocha mwingine.

Nikiona hata uso mmoja wenye huzuni mwishoni mwa msimu, nitakuua. Jamani, nitakuua.

Nikiona uso wako ukilalamikia jambo fulani au maamuzi yangu, nitakuua kabisa.

Ninaposema, “Habari,” unaniambia, “Habari.”

Ninaposema, “Habari,” na kukukumbatia, nawe unanikumbatia.

Kwa sababu ninafanya kazi kwa ajili yenu. Ninaishi maisha yangu—talaka yangu, familia yangu kuwa mbali na kila kitu—kwa ajili yenu nyote.

Na ninyi mnanirudishia nini?

Kiwango kile cha kipumbavu cha uchezaji mlichokionesha, ninyi nyote.

Ni aibu, jamani. Aisee!

Hali hii ya kukosa ujasiri, ari, upendo na hamu ya kushinda na kufanya vizuri zaidi haikubaliki.

Ninajihisi mpweke.

Mnapocheza namna hii, ninajihisi mpweke.

Kwa kweli nimechoka sana.

Ninapoona hali kama hiyo, ninachoka kabisa, nguvu zinaniishia.

Ninataka kuacha.”

Unapoisoma hatuba hiyo, unaona kabisa jinsi ambavyo inatoka ndani ya moyo wa mtu anayependa sana kile anachofanya, aliyejitoa maisha yake yote kukifanya kwa viwango vya juu.

Lakini anavunjika moyo kutokana na kile ambacho wale anaowategemea watekeleze hawafanyi hivyo. Anapoona kabisa kwamba ipo ndani ya uwezo wao, lakini hawafanyi, anaumia sana.

Kwenye kipengele cha tano cha hii barua, nitashirikisha barua yangu kwako, ambayo ina yale niliyokuwa nafikiria ambayo sikuwa nimepata namna ya kuyaweka vizuri mpaka nilipopata hotuba hii ya Pep Guardiola.

Kwenye #BaruaYaKocha nimekupa hotuba yangu, yenye tathmini ya safari ambayo tumekuwa nayo mpaka sasa na mwelekeo wake kwa miaka kumi ijayo. Ni muhimu sana kusoma hotuba hiyo kama wewe ni sehemu ya hii safari.

Soma barua hapa; #BZK076; Nikikuona Unalalamika Hufanikiwi, Wakati Huchukui Hatua, ‘Nitakuua’.