#SheriaYaLeo (342/366); Kutembea na kifo.
Watu wengi huwa wanaishi maisha yasiyo na maana na kupoteza muda kwa kuona wana muda mwingi wa maisha.
Ni mpaka pale wanapokutana na hali ya kukabiliana na kifo, ndipo wanaiona thamani ya muda na kuutumia kwa uangalifu mkubwa.
Kwa mfano mtu anapogundulika kuwa na saratani ambayo itakatisha maisha yake ndani ya muda mchache ujao, hapo sasa muda unakuwa na thamani kubwa kwake na hakubali kuupoteza kwenye mambo yasiyokuwa na tija.
Kadhalika mtu anayenusurika kufa kwenye ajali, anaona jinsi maisha yalivyo na thamani na kuacha kupoteza muda.
Hatupaswi kusubiri mpaka tukutane na kifo ndiyo tuzinduke na kuanza kuishi.
Badala yake tunapaswa kutambua kwamba tunatembea na kifo muda wote.
Na kwa sababu wote tutakufa na hakuna ajuaye wakati wake, ni vyema kutumia vizuri muda wako wote bila kuupoteza.
Huwezi kujua kesho ina nini kwa ajili yako, hivyo tumia leo yako vizuri.
Kifo unatembea nacho, mara zote kuwa tayari kukikabili, kwa kutumia muda wako vizuri na kwa tija.
Usipoteze muda wako kwa mambo yasiyo na maana, hujui ni muda kiasi gani umebakiwa nao.
Tumia kila muda wako kama ndiyo wa mwisho, kwa sababu kuna wakati itakuwa hivyo.
Sheria ya leo; Hatima yetu ni kifo, kila siku inayopita tunakikaribia zaidi kifo chetu. Ni muhimu kutambua na kukubali hilo ili kutumia muda kwa umakini mkubwa.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji