2927; Nitavumilia matokeo, siyo mchakato.

Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye maisha kuna mambo mawili makubwa; mchakato na matokeo.

Mchakato ni yale unayofanya, hatua unazochukua kwenye kila jambo.

Matokeo ni kile kinachokuja kupatikana kutokana na hatua zinazokuwa zimechukuliwa.

Mchakato upo ndani ya uwezo wa mtu. Mtu ana uwezo wa kuamua nini afanye na kwa wakati gani.

Matokeo yapo nje ya uwezo wa mtu. Hata mtu afanye nini, bado matokeo yanakuja yenyewe kwa wakati wake.

Katika kushirikiana na wewe, nipo tayari kukuvumilia kama hupati matokeo unayotaka. Nitakuvumilia hata kwa zaidi ya miaka kumi, kwa sababu najua matokeo hayapo kwenye udhibiti wako.
Lakini pia najua kwa kukaa kwenye mchakato sahihi, matokeo ni swala la muda tu.

Lakini inapokuja kwenye mchakato, sipo tayari kukuvumilia kama hukai kwenye mchakato ambao tumekubaliana. Siwezi kukuvumikia hata kwa dakika kumi kama hukai kwenye mchakato.
Hiyo ni kwa sababu najua mchakato uko ndani ya uwezo wako, hivyo kama hukai kwenye mchakato ni hutaki tu.

Kama tumeshakubaliana kitu cha kufanya, halafu wewe unaamua hufanyi, nachukulia ni dharau na kupuuza.
Ni kuchagua kutokuheshimu muda na juhudi ninazoweka katika kuhakikisha wewe unakaa kwenye mchakato sahihi ili uweze kuathiri matokeo bora.

Kuwa tu muwazi, siwezi kuendelea kutoa muda na juhudi zangu kwa mtu ambaye haviheshimu.
Sitakuhukumu kwa matokeo unayopata, lakini nitakuhukumu vikali sana kwenye juhudi unazoweka.

Nimekuwa nakushirikisha kuhusu makundi matano ya watu. Haupo kwenye kundi la kwanza au la pili, siwezi kukupa nafasi kwenye maisha yangu.
Siyo jambo la ubaguzi, bali maamuzi ya watu sahihi wa kushirikiana nao ili kufika kule ninakotaka kufika.

Muda na nguvu ni rasilimali muhimu na zenye uhaba mkubwa.
Nikizitumia rasilimali hizo kuhangaika na mtu asiyetaka kukaa kwenye mchakato, nashindwa kuzitumia rasilimali hizo kwa wale wanaokaa kwenye mchakato.

Kama unapata matokeo bora nje ya mchakato, nikupongeze sana na kukutaka uendelee na huo utaratibu wako.
Lakini kama unataka twende pamoja, kaa kwenye mchakato ambao tumekubaliana.
Kaa kwenye mchakato huo kwa msimamo, muda wote na kwa asilimia 100.
Usichague nini unataka kufanya na nini hutaki.
Unakaa kwenye mchakato kamili na matokeo yanakuja kwa wakati wake.

Nakupenda na kukuheshimu, ndiyo maana nakuandalia mchakato na kukutaka ukae kwenye huo.
Hata kama hunipendi, wewe niheshimu tu kwa kukaa kwenye mchakato huo. Na kama huwezi hilo basi achana na mimi kabisa, maana haitakuwa na msaada kwetu wote.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe