2949; Upendeleo.

Rafiki yangu mpendwa,

Miaka ya nyuma niliwahi kuongea na rafiki yangu ambaye alikuwa ameomba kazi ya udaktari kwenye shirika fulani kubwa.
Alikuwa ananishirikisha baadhi ya maswali aliyoulizwa wakati wa usaili.
Moja ya maswali aliyoulizwa ni iwapo kuna foleni ya watu wanasubiria kuingia kwa daktari na kuna mtu wa kawaida na kiongozi wapo kwenye foleni, ataanza kumwita nani?
Yeye akajibu ataanza kumwita aliyeanza kufika.
Nilimwambia hakujibu kwa usahihi, hata kama mtu wa kawaida ndiye aliyetangulia kufika, alipaswa kumpa upendeleo kiongozi, kwa sababu akitoka hapo anakuwa na majukumu makubwa zaidi kuliko mtu wa kawaida.

Kocha mmoja wa mpira aliwahi kunukuliwa akisema iwapo mchezaji wake bora kabisa atasinzia wakati wa mazoezi, atahakikisha anapewa mto ili asiumie na pia mtu anakaa nyuma yake ili ilitokea ameyumba asianguke vibaya.
Lakini ikitokea mchezaji wa kawaida amesinzia wakati wa mazoea, atampa adhabu kali ili arudishe umakini wake wote kwenye mazoezi.

Kwa mifano hiyo miwili, unaweza kuona siyo sawa, kwa nini watu wote wasichukuliwe sawa, kwa nini kuwe na upendeleo kwa baadhi ya watu?

Hilo ndiyo tunakwenda kulijadili leo.
Pamoja na viwango na misimamo mbalimbali unayojiwekea kwenye maisha yako, kazi na biashara, unapaswa kuwa na upendeleo.

Kuna watu wachache sana, ambao wanaonyesha uwezo wa kipekee kabisa ambao unapaswa kuwapa upendeleo.
Hawa unawavumilia hata kama wanakwenda kinyume na utaratibu, kwa sababu matokeo wanayozalisha ni makubwa sana.

Kila sheria huwa ina upendeleo wake fulani, lakini huwa ni mchache na kwa matokeo ambayo siyo ya kawaida.
Sheria ikiwa na upendeleo mwingi, inaacha kuwa sheria.

Hivyo pamoja na vigezo vya juu unavyojiwekea kwenye maeneo yako mbalimbali, usiache kuwapa upendeleo wale wachache sana wanaokupa matokeo ya kipekee kabisa ambayo hakuna wengine wanaweza kukupa.

Inaweza kuwa ni mfanyakazi ambaye anakupa matokeo bora mno lakini kuna utaratibu hafuati. Au ikawa ni mteja anayeleta mamufaa makubwa kwenye biashara lakini anashindwa kutimiza baadhi ya vigezo ulivyoweka.

Kuwa na upendeleo kwa matokeo yasiyokuwa ya kawaida siyo kukosa msimamo au unafiki. Bali ni kuendana na uhalisia.
Vigezo na viwango unavyokuwa umeweka ni kwa ajili ya kuleta matokeo makubwa na ya uhakika.
Kama kuna ambao wanakupa matokeo hayo bila kutimiza vigezo na viwango vingine, unaweza kuwapa upendeleo kwa muda.

Upendeleo unapaswa kuwa wa nadra sana na kwa wachache mno ambao wamethibitisha kuweza kuzalisha matokeo ya viwango vya juu mno ambavyo hakuna mwingine anayeweza kufikia.
Lakini kwa wengine ambao wanazalisha matokeo ya kawaida, yanayozalishwa na walio wengi, wanapaswa kufuata kila kigezo na utaratibu uliopo.

Unaweza kusema wale unaowapa upendeleo watakusumbua kwa kuwa na kiburi. Watajiona wao ni muhimu kuliko wengine na itakuwa vigumu kwako kuwasimamia.
Hilo ni kweli, lakini wewe unawapa upendeleo siyo kwa sababu zao binafsi, bali kwa sababu ya matokeo wanayozalisha.
Hivyo kama kuna matokeo bora wanazalisha, unaweza kuvumilia usumbufu huo.
Lakini pale watakapoacha kuzalisha matokeo hayo ya tofauti, ndipo watakaposhangaa jinsi mambo yatakavyobadilika.

Kwenye ukurasa utakaofuata utajifunza hilo kwa kina, kupitia mfano wa kuku aliyekuwa anataga sana au ng’ombe aliyekuwa anatoa maziwa mengi. Wote huishia kuchinjwa pale uzalishaji wao unapopungua.
Hivyo pia ndivyo upendeleo unaotoa kwa watu unavyoisha.

Tunachoangalia ni mchakato na matokeo.
Haleti matokeo anapaswa kuwa kwenye mchakato kwa uhakika bila kuyumba.
Analeta matokeo makubwa sana na yasiyo ya kawaida, anaweza kuvumiliwa hata kama hakai kwenye mchakato.
Ila tu asiwe anatumia njia zilizo nje ya sheria kuzalisha matokeo hayo.

Kumbuka upendeleo tunaoongelea hapa ni kwa wachache wenye uwezo na vipaji vya kipekee kabisa na ambao matokeo wanayozalisha hakuna wengine wanaoweza kuyazalisha.
Hawa huwa ni wachache sana.
Usianze kutoa upendeleo kwa kila mtu kwa sababu tu amekufurahisha na matokeo fulani. Ni kwa wale wa kipekee sana, ambao huwa ni wachache mno na nadra kukutana nao.

Sheria au utararibu wowote ukiwa na upendeleo kwa wengi unakosa nguvu na kupuuzwa.
Hivyo hili ni eneo la kuwa nalo makini sana.

Pamoja na kuwa tayari kuwapa baadhi ya watu upendeleo, bado kuna mambo ya msingi anayopaswa kuyazingatia, ili upendeleo unaotoa usiwe wa kubomoa bali kujenga.
Lazima afuate taratibu za msingi zinazosaidia kujenga ushirikiano mzuri baina ya wote wanaojihusisha nao.

Msimamo lazima uwepo, lakini pia upendeleo kwa wachache wanaostahili haupaswi kukosekana.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe