2969; Tegemeo lako.

Rafiki yangu mpendwa,
Hakuna kipindi kizuri kwenye kujenga biashara kama kipindi ambacho biashara ina wateja wachache.

Wengi hukihofia kipindi hiki na kukimbilia kufafuta wateja wengi zaidi kabla hawajawajua vizuri wateja wachache walionao.

Hakuna tatizo lolote kwenye kutaka kufikia wateja wengi zaidi. Lakini itapendeza sana kama utawatumia vizuri wateja wachache wa awali unaokuwa nao.

Wakati biashara yako inakuwa na wateja wachache ndiyo kipindi kizuri kwako kuwajua kwa kina.
Ndiyo kipindi cha kujifunza mengi sana kutoka kwao kwa namna ya kuwahudumia vizuri.
Ndiyo kipindi cha kuwahudumia vizuri sana na kuwapa thamani kubwa ili kuwajengea imani kwako.
Na pia ndiyo kipindi cha kupata wateja wengine bora zaidi kutoka kwa wateja ulionao.

Kwa umuhimu huo wa wateja wa awali, wanakuwa ndiyo tegemeo la biashara yako.
Washike mikono yao, wajue kwa kina na wape mapenzi ya kweli.
Wajibu wako mkubwa ni kuhakikisha wateja hao wa mwanzo wanafanikiwa kwenye eneo unalowahudumia, ili wasiwe na sababu ya kwenda kwa washindani wako.

Na hilo halina muujiza wowote kwenye kulifanya. Unapaswa kuwapigia simu, kuwatembelea na kuongea nao kwa kina.
Unapaswa kuwauliza nini hasa wanachotaka, nini cha kuboresha na mawazo mengine yoyote waliyonayo.
Waombe ushauri na maoni yao kisha fanyia kazi mapendekezo wanayotoa.

Wafanyabiashara wengi wamekuwa wanapuuza hili na baadaye kujikuta kwenye changamoto kubwa.
Kila wanapokazana kufikia wateja wengi wapya, wanajikuta wakipoteza wa zamani waliokuwa nao.

Biashara yako inapokuwa na wateja chini ya 100, ni kipindi cha kuwajua wateja hao wote kwa undani na kuwapa thamani kubwa sana.
Na hata kama biashara yako ina wateja zaidi ya 100, chagua 100 ambao hutaki uwapoteze kwa namna yoyote ile. Kisha wajue kwa kina na uwape thamani kubwa mno kiasi cha wao kukosa sababu ya kwenda kununua pengine.

Ni jambo la kuumiza sana pale unapotumia nguvu kubwa kufikia wateja wapya na kuwashawishi kununua, wakati wale ambao tayari walishanunua hawarudi tena, badala yake wanaenda kununua kwa wengine.

Ni uzembe wa hali ya juu sana pale mfanyabiashara anapokuwa hana taarifa za wateja ambao wameshanunua kwenye biashara yake na mwenendo wao kwenye matumizi.
Na uzembe wa aina hii ndiyo umekuwa chanzo cha biashara nyingi kufa.

Iko hivi rafiki, ni rahisi sana kumuuzia mteja ambaye ameshanunua kuliko ambaye ni mpya kabisa.
Na kama mteja ameshanunua kwako mara moja, anapaswa anunue kipindi chote cha maisha yako.
Kama wateja wananunua mara moja na hawarudi, kuna uzembe mkubwa sana unaofanyika na hata uhangaike na kufikia wateja wapya wengi kiasi gani, bado biashara itashindwa kukua.

Biashara yako inahitaji wateja wasiopungua elfu 1 ili iweze kujiendesha kwa faida na kupata ukuaji.
Lakini wewe binafsi kama mfanyabiashara, unahitaji wateja wasiopungua 100 ambao unawajua hao ni mashabiki wa kweli, wasioweza kwenda kununua pengine ila kwako, na hao ndiyo watakuwezesha kukaa kwenye mapambano ya kujenga biashara yako.

Unawajengaje wateja hao 100 ambao ndiyo tegemeo lako?
Ni kwa kuwajali kwa kupitiliza.
Kuwajua kwa undani, kuwapa thamani kubwa sana na kuwa nao karibu mno.
Kuwa tayari kuacha mengine yote na kuwahudumia vizuri wateja 100 ambao ndiyo tegemeo lako.
Kuna mengi utakayojifunza kwa wateja hao 100 ambayo yatakuwezesha kuikuza sana biashara yako.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwa wafanyakazi wa biashara yako.
Wakati unapokuwa nao wachache, chini ya 30, wajue kila mmoja kwa undani na kuwajali sana.
30 ni idadi ambayo mnaweza kuenea kwenye chumba kimoja cha kufanya mkutano. Ni rahisi kumjua kila mtu kwenye wafanyakazi 30.
Lakini wanapokuwa wengi zaidi, wanakuwa chini ya viongozi wengine, hivyo wewe unaweza usiwajue moja kwa moja na kwa undani.

Tumia sana fursa za awali wakati wafanyakazi ni wachache kujenga utamaduni bora kabisa wa eneo lako la biashara.
Tumia yale unayojifunza kwa wafanyakazi wachache unaokuwa nao kuweza kujenga timu kubwa zaidi ya wafanyakazi sahihi kwenye biashara yako.

Kwa sababu tunataka sana kukua, huwa hatupapendi chini, lakini ndivyo asili inavyofanya kazi.
Mbegu hukaa chini kwa muda na kushika mizizi kabla haijakua.
Nyumba hujengewa msingi imara sana chini ya ardhi kabla haijapandishwa na kuwa nyumba.

Zingatia sana hatua za awali, hapo ndipo penye nguvu kubwa ya kujenga biashara kubwa na itakayokufikisha kwenye malengo makubwa uliyonayo.
Usitake tu kukimbia, jua unakimbia kuelekea wapi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe