2970; Kosa la uzururaji.

Rafiki yangu mpendwa,
Kipindi nikiwa mdogo, nilikuwa nashangaa sana pale niliposikia kuna watu wamekamatwa na posili kwa kosa la uzururaji.
Nilikuwa nashangaa mtu mzima anazururaje.
Maana nilizoea unapoambiwa acha kuzurura, maana yake ni uache kwenda kila mahali na kutulia sehemu moja.

Baadaye nilikuja kujifunza kwamba kumbe uzururaji siyo tu kuzunguka kila mahali, bali hata kuwa eneo ambalo hukupaswa kuwa ni uzururaji.
Kwa mfano kama umekubwa upo baa wakati ambao ni wa kazi, hapo unazurura.

Ni kupitia maana hiyo ya uzururaji nimekuwa natafakari jinsi watu wengi kwenye maisha wanavyozurura.
Kwa maana ya uzururaji kwamba ni kuwa eneo ambalo hukupaswa kuwa, watu wengi sana wanazurura kwenye maisha yao.

Na kiashiria kikubwa kinachounga mkono hilo ni jinsi ambavyo watu wengi wanashindwa kupata mafanikio licha ya kuonekana ni wachapakazi saba.
Kwa nje tunaweza kuona mtu anajituma sana.
Lakini ni kwa ndani ndiyo tunaweza kuona kama anajituma kweli au anazurura tu.

Kama hulijui kusudi la maisha yako, kama huna ndoto kubwa unazozipigania, kama huna malengo na mipango unayojisukuma nayo, sehemu kubwa ya unayofanya yanakuwa ni uzururaji, maana hakuna yanakokupeleka.

Watu wengi kwa zama hizi wanaweza wasikamatwe kwa kosa la uzururaji, kwa sababu wanakuwa wanaonekana kama vile kuna kitu wanafanya na mahali wanaenda.
Lakini uhalisia ni wanajiendea tu, hawajui hata wapi wanaenda.

Dalili nzuri ya mtu mzururaji ni mambo mapya anauojihusisha nayo kila wakati.
Kila wakati kuna fursa mpya na inayolipa sana anayokuwa anazungumzia.
Kuwa mtu wa kukimbizana nafursa mpya kila wakati siyo sifa nzuri, bali ni kiashiria hakuna chochote kimoja ambacho umejitoa kweli kuhakikisha umekipata.

Kwa upande mmoja tunaita uzururaji ni kuhangaika na vitu vingi badala ya kuweka juhudi zako zote kwenye vitu vichache na vyenye tija.

Kwa upande wa pili, uzururaji ni kuwa sehemu ambayo hukupaswa kuwa.
Katika hali hiyo, unakutana na mambo ambayo hukuwa umepanga kukutana nayo, kitu kinachoweza kuwa usumbufu au kikwazo kwako.

Kwa mfano umeibiwa au kutapeliwa, hapo tatizo siyo wizi wala utapeli, bali tatizo ni wewe.
Ni wewe mwenyewe umejiweka kwenye hali ya kuibiwa na kutapeliwa kirahisi.
Nina imani kwamba kama ungekuwa umeweka umakini wako kwenye vitu sahihi kwako, usingepata nafasi ya kutapeliwa.
Kuzurura kwako ndiyo kumekuweka kwenye hatari ya kuibiwa na kutapeliwa.

Kadhalika, kama kuna watu wamekufanyia namna ambavyo hukuridhika, kosa linarudi kwako, uzururaji.
Ni wewe umejipeleka kwa watu au hali ambazo hazina heshima ya kutosha kwako.
Kama ungekuwa unajua kwa hakika kile unachotaka na kujitoa kukipata, ungepunguza mno kutendewa isivyo sahihi.

Sehemu kubwa ya watu tunaopishana nao kila siku wanaweza kuonekana kama kuna mahali wanaenda.
Lakini kwa hakika wengi ni wazururaji tu.
Nikupe mfano mzuri, pita barabarani na ukute kuna ajali imetokea. Utashangaa jinsi ambavyo utakuta watu wengi wamezingira eneo hilo na wanakaa hapo muda mrefu. Hata wale wanaopita wakiendesha magari, wanapunguza mwendo kuangalia nini kinachoendelea, kitu kinachopelekea foleni kubwa kubwa zaidi.
Wote hao hawana mahali pa muhimu wanaenda, wanazurura tu na maisha yao.
Maana naamini kama mtu kuna mkutano wa muhimu sana anaowahi na muda umekwenda, hatapoteza muda kuangalia nini kinaendelea, badala yake ataendelea na kasi yake ya kuwahi kule anaenda. Anajua kama kuna taarifa zozote muhimu anapaswa kuzijua, atazisikia kwa wengine.

Hapo hatujagusa wale wanaoamka na kujikuta wamevaa ajenda ya siku kwenye habari zinazoendelea.
Na wale wanaoshinda kwenye mitandao ya kijamii.
Na wanaobishana na kufuatilia mambo ya burudani zaidi.
Yote hayo ni uzururaji, kiashiria kwamba mtu hajui anakokwenda hivyo inakuwa rahisi kuchukua njia yoyote inayojitokeza mbele yake.

Ili kuondokana na uzururaji, kujua kwa hakika kile unachotaka na kukipambania muda wote ni muhimu.
Pale unachotaka kinapokuwa kikubwa na kukutaka wewe ujitoe sana ili kukipata, hupati kabisa nafasi ya kuzurura.
Muda wote unakuwa umetingwa na hicho unachotaka.

Hatua ya kwanza ya kupata mafanikio makubwa kwenye maisha ni kuacha kuzurura.
Hilo ni kosa ambalo lina adhabu kubwa ya kukunyima mafanikio bila ya wewe kujua.
Weka umakini wako wote kwenye vitu vichache muhimu na utaweza kufanya makubwa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe