2975; Huu ndiyo ushindi.

Rafiki yangu mpendwa,
Wote tulio hapa tuna lengo kubwa moja ambalo ni kufikia ubilionea.
Hilo ndiyo lengo kuu ambalo kila mmoja wetu analipambania.
Ni lengo ambalo tunaamini bila ya shaka yoyote kwamba tutakifikia.
Kwa sababu tupo tayari kulipambania bila ya kuchoka wala kukata tamaa.

Katika kufikia lengo hilo la ubilionea, kuna sehemu kuu mbili.
Sehemu ya kwanza ni juhudi ambazo tunaweka. Hii ni zile hatua tunazochukua ili kulifikia lengo.
Na sehemu ya pili ni matokeo yenyewe. Hapo ndipo kufikia lengo husika.

Katika sehemu hizo mbili, sehemu ya kwanza ipo ndani ya udhibiti wetu kwa asilimia 100. Tunaweza kuifanyia kazi kwa uhakika bila kushindwa kwa namna yoyote ile.
Lakini sehemu ya pili haipo ndani ya udhibiti wetu kwa asilimia 100. Ni zao la sehemu ya kwanza, ambalo hatuwezi kupangilia utokeaji wake.

Kitu kimoja tunachojua ni kwamba kama tutatekeleza sehemu ya kwanza kwa uhakika mkubwa, tunakuwa tumeathiri sana sehemu ya pili.
Kwa kukamilisha sehemu ya kwanza kwa asilimia 100 bila kushindwa, kuna nguvu kubwa ya kusababisha sehemu ya pili nayo ikamilike.

Sasa basi, watu wengi hupima ushindi kwa matokeo, kwa ukamilikaji wa sehemu ya pili.
Kwenye kipindi chote wanachokuwa wanafanyia kazi sehemu ya kwanza hawahesabu ushindi.
Ni mpaka pale wanapopata matokeo wanayotarajia ndiyo wanahesabu ushindi.

Hiyo siyo sahihi na ndiyo kimekuwa chanzo cha wengi kukata tamaa, hasa wanapokutana na magumu na changamoto.
Kadiri lengo na matokeo yanayotarajiwa yanavyokuwa makubwa, ndivyo muda mrefu zaidi unavyohitajika ili kufikia.
Sasa mtu anaposubiria ushindi kwenye matokeo, inakuwa rahisi kukata tamaa.

Ushindi sahihi wa kupima ni kwenye kukamilisha sehemu ya kwanza, yaani kuchukua hatua unaopaswa kuchukua.
Hii ndiyo tunayoita kukaa kwenye mchakato kwenye safari yetu ya ubilionea.

Kukaa kwenye mchakato, kwa asilimia 100 bila kuyumba ndiyo ushindi mkubwa sana kwetu.
Hiyo ni kwa sababu ndiyo kitu tunachoweza kukiathiri, lakini pia ndiyo chenye mchango kwenye matokeo tunayotaka kupata.

Kukaa kwenye mchakato ndiyo ushindi mkuu kwa sababu tungeweza tusikae.
Tungeweza kutoa sababu na visingizio mbalimbali kwa nini tumeshindwa kukaa kwenye mchakato.
Lakini pale tunapojisukuma kwa kila namna na kukamilisha kukaa kwenye mchakato tunakuwa tumepata ushindi mkubwa sana.

Ni kwa kuendelea kukaa kwenye mchakato kwa ushindi mara zote ndipo penye nguvu ya kupata kile tunachotaka.
Na huu ni ushindi mkubwa kwa sababu japo mchakato upo wazi kwa wote, siyo wengi wanaoweza kuukamilisha.
Wengi ni wavivu, wazembe na wajinga ambao hawataki kujisumbua kwa namna yoyote ile.
Wewe kuwa tu tayari kujisumbua kwa kukaa kwenye mchakato kwa asilimia 100 ni ushindi mkubwa bila kujali matokeo gani umepata.

Ili uweze kukaa kwenye mchakato kwa asilimia 100, lazima ujikubali na ukikubali sana kile unachofanya.
Lazima uuamini na kuupenda mchakato mzima.
Na lazima uwe na maono ambayo mchakato ndiyo njia sahihi ya kuyafikia.
Halafu wewe unapambana na mchakato wako, ukijua huo ndiyo ushindi mkubwa kwako.
Matokeo ya mwisho ni kitu cha ziada, ambacho kitakuwa kizuri kulingana na ukaaji wako kwenye mchakato.

Kukaa kwenye mchakato kwa asilimia 100 mara zote ndiyo ushindi mkubwa kwako.
Ndiyo kitu unachoweza kukiathiri moja kwa moja.
Na ndiyo kitu chenye nguvu ya kuathiri matokeo ya mwisho unayoyataka.
Usisumbuke sana na hayo matokeo ya mwisho, wewe sumbuka na kukusanya ushindi wako wa kila siku kwa kukaa kwenye mchakato kwa asilimia 100.

Hakuna namna unaweza kushindwa kama utafuata huu mwongozo kwa uhakika.
Ushindi ni kwako, labda tu uamue kushindwa wewe mwenyewe.
Maana hakuna chochote unachoweza kukisingizia kwa kushindwa kukaa kwenye mchakato.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe