2996; Fanya vitu vya maana.

Rafiki yangu mpendwa,
Sisi binadamu tuna rasilimali tatu ambazo zina uhaba mkubwa sana.
Rasilimali hizo ni muda, nguvu na umakini.
Hizo ni rasilimali ambazo ukishaziweka kwenye kitu kimoja, huwezi kuziweka tena kwenye kitu kingine.

Chochote unachofanya kwenye maisha yako, lazima utahusisha rasilimali hizo tatu, utaweka muda wako, utamia nguvu za mwili na umakini wa akili yako.

Hivyo basi, kama unakwenda kufanya kitu, basi hakikisha ni kitu cha maana kweli kwako wewe kufanya.
Fanya kitu ambacho kinaleta tofauti kubwa kwako na kwa wengine pia.
Fanya kitu ambacho utajivunia kweli ni matumizi sahihi ya rasilimali zako muhimu na matokeo yake kuwa yenye manufaa makubwa kwa kila anayehusika.

Muda wetu ni mfupi sana hapa duniani.
Nguvu za miili yetu zinapungua kadiri tunavyozitumia.
Na umakini wa akili zetu hauwezi kwenda kwenye mambo mengi kwa wakati mmoja.
Swali muhimu la kujiuliza ni unakwenda kutumiaje rasilimali hizo muhimu sana kwako ambazo zina uhaba mkubwa?

Jibu sahihi ni kutumia rasilimali zako adimu kwenye mambo ya maana, mambo ambayo ni muhimu zaidi na yenye mchango kwako na kwa wengine pia.
Mambo ya maana kufanya ni yale yanayoacha maana fulani kwa kila anayehusika.
Mambo ambayo ukiangalia nyuma unaona mchango wake kwenye hatua ambazo mtu umepiga.

Hiyo ndiyo njia sahihi ya kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako.
Ndiyo njia sahihi ya kutoa thamani kubwa kwa wengine na wewe mwenyewe kupokea thamani kubwa pia.

Ni rahisi sana mambo yasiyo muhimu kuteka rasilimali zako tatu muhimu na kujikuta zinapotea bila manufaa.
Kuna mengi sana yanayowinda rasilimali hizo muhimu, mambo ambayo hayana tija yoyote.

Ni muhimu sana kila wakati kujikumbusha nini unafanya na kina umuhimu kiasi gani.
Unafanya hivyo kwa kujiuliza mara kwa mara, je hiki ninachofanya sasa ndiyo kitu cha maana zaidi kuliko vingine ambavyo ningeweza kuvifanya?
Kama jibu ni ndiyo endelea kufanya, lakini kama jibu ni hapana, acha mara moja kufanya na uende kwenye kile cha maana zaidi.

Maisha ni kuchagua,
Maisha ni vipaumbele,
Maisha siyo kufuata mkumbo.
Weka vipaumbele vyako kwa usahihi na vifuate vipaumbele hivyo bila kuyumbishwa na mengine yasiyo na maana.

Kila utakachofanya kwenye maisha yako, kitatumia muda, nguvu na umakini wako.
Hivyo badala ya kupoteza rasilimali hizo adimu kwenye mambo yasiyokuwa na tija, ni bora kuhakikisha unapeleka rasilimali hizo kwenye mambo ya maana zaidi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe