2997; Wingi na ubora.

Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye kila kitu tunachofanya, kuna njia mbili za kukiendea; wingi na ubora.

Kwenye wingi unaangalia namba.
Na kadiri namba inavyokuwa kubwa, ndivyo matokeo yanavyokuwa mazuri pia.

Kwenye ubora unaangalia viwango.
Kadiri viwango vinavyokuwa vya juu, ndivyo matokeo yanavyokuwa mazuri.

Kwa bahati mbaya sana wingi na ubora haviwezi kwenda pamoja.
Ukiangalia wingi, inabidi uachane na ubora, maana vilivyo bora huwa siyo vingi.
Kadhalika ukiangalia ubora inabidi uachane na wingi.

Unapokuwa unaanza kwenye jambo lolote lile, utaanza kwa kuzingatia wingi.
Lakini kadiri unavyokwenda, utahamia kwenye kuzingatia ubora.
Kuanza na wingi kunakufikisha kwenye ubora kwa urahisi zaidi kuliko kuanza na ubora.

Tuangalie mfano wa mauzo.
Unapokuwa unaanza biashara, unakuwa huna wateja kabisa.
Hivyo mwanzo unaanza kwa kukazana kuwafikia wateja wengi zaidi ili uweze kufanya mauzo makubwa.

Kwa wateja wengi unaowafikia, manunuzi yao hayalingani. Lakini mwanzo watakuwa wanachukua nguvu zako kwa usawa.

Na hapo ndipo unapohitaji kubadilika na kuzingatia zaidi ubora kuliko wingi.
Hapo unaangalia wateja wachache wanaofanya manunuzi makubwa zaidi. Kwa kuwajua hao na kuwapa huduma bora zaidi, unapata fursa ya kuwauzia kwa wingi zaidi.

Kwa lengo lolote la mauzo ulilonalo, kuna wateja wachache bora wanaoweza kukufikisha kwenye lengo hilo.
Kama lengo ni kuuza milioni 100, unaweza kuuzia wateja elfu 1 wanaonunua kwa wastani wa laki moja, au wateja 100 wanaonunua kwa miloni 1, au wateja 10 wanaonunua kwa milioni 10.

Ipi rahisi na ipi sahihi?
Kwa haraka haraka inaonekana kuwauzia wengi ni rahisi kufikia lengo kuliko wachache.
Lakini kama tunavyojua, rahisi siyo sahihi na sahihi siyo rahisi.
Unaweza kuona kuwauzia wengi inarahisisha kufikia lengo.
Lakini kuwahudumia wengi hao kwa viwango vya juu kabisa unavyotaka siyo rahisi.
Pia kupata wengi waaminifu siyo rahisi, kuna ambao utakuwa tayari kuwapa zaidi, lakini akitokea mshindani wako, wanakuwa tayari kukimbilia kwenda kujaribu kwa mshindani na kukuacha wewe.

Kuangalia ubora kunaonekana ni kugumu, lakini ndiyo kuliko sahihi.
Hiyo ni kwa sababu idadi ndogo unaweza kuihudumia kwa ukaribu zaidi na kutoa thamani kubwa ambayo pia italeta marejesho makubwa.
Ugumu wa ubora ni kwenye kuufikia.
Kuwafikia wateja wachache na walio bora kunahitaji kazi kubwa sana.
Kunahitaji mtu kujitoa kweli na kuzama kwenye maisha ya wengine, kuwajua kwa undani na kuwapa kile ambacho kina manufaa makubwa zaidi kwao.

Hilo ni zoezi ambalo huwezi kulifanya kwa wengi.
Ndiyo maana unapoanza utazingatia wingi, kisha katika hao wengi utachagua wachache ambao utawahudumia vizuri zaidi na wakakupa matokeo makubwa zaidi.
Unapozingatia ubora, ni lazima uzame ndani kweli kweli, uwapende kwa dhati wachache uliowachagua na kuhakikisha nao pia wanakupenda na kukukubali.
Hilo ni zoezi ambalo huwezi kulikuza kwa haraka, lakini lina nguvu kubwa ya kukujengea sifa ya kipekee ambayo unaweza kuitumia kuwapata wengine walio bora.

Ukiwazingatia kweli wachache ambao ni bora, wanaofanya manunuzi makubwa, utaweza kuwashawishi wanunue zaidi na pia utaweza kuwaomba wakupe wateja wengine ambao ni bora kama wao.
Na hata pale inapotokea kuna washindani wako wanamwinda kwa mbinu mbalimbali, hawatakimbilia kwa washindani na kukuacha wewe.
Badala yake wataongea na wewe kwanza, kukujulisha kinachoendelea ili kuona kama unaweza kuboresha zaidi.

Tunapochagua kuweka juhudi kubwa zaidi kwa wachache walio bora, wanalijua hilo hasa na kulithamini. Ni kuthaminiwa huko ndiko kunaleta matokeo makubwa na mazuri.

Mwanzoni kazana sana na wingi,
Kadiri unavyokwenda hamia kwenye ubora zaidi.
Na kadiri unavyoendelea, tengeneza wingi ndani ya ubora.
Fikia wengi walio bora na hapo ndipo ulipo ufunguo wa ndoto kubwa ulizonazo.
Kama kweli unaweka muda, nguvu na umakini kwenye kile unachofanya, unaziona fursa za kufikia ubora ulio mwingi.
Hilo linahitaji kazi kubwa ili liweze kutokea.
Kazi ambayo hupaswi kuikimbia mtu mwenye ndoto kubwa kama wewe.

Kwenye maisha usifuate mkumbo wa kukimbilia wingi kama wengi wanavyokushauri na kufanya.
Wewe piga hesabu zako vizuri, ni idadi ya chini kiasi gani inaweza kukufikisha kwenye lengo lako.
Kisha weka kazi kwenye kufikia idadi hiyo ndogo ambayo ni bora zaidi.
Kwa namba ndogo utaweza kuzalisha matokeo makubwa kuliko kuhangaika na namba kubwa.

Msisitizo mkubwa ni utaanza na wingi kwanza kabla ya kwenda kwenye ubora.
Lazima uwafikie wengi kisha kuwachuja na kupata wachache ambao ni bora.
Kisha hao wachache ndiyo unaendelea kuwapa thamani kubwa zaidi ili waridhike na kukupa fursa zaidi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe