3001; Wape ushindi.

Rafiki yangu mpendwa,
Falsafa kuu ambayo ndiyo huwa naendesha nayo huduma zangu, ambayo nilijifunza kutoka kwa Zig Zigler inasema; unaweza kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako, kama utawasaidia watu wengi zaidi kupata kile wanachotaka.

Swali ni watu wengi wanataka nini ili uweze kuwapatia na wewe upate unachotaka?
Jibu ni moja, watu wanataka ushindi.

Ushindi ndiyo kitu ambacho watu wengi wanakitaka sana, lakini pia hawakipati.
Na watu wanapokosa ushindi kwao binafsi, wanajipa ushindi usio halisi.

Angalia jinsi ambavyo michezo imepata umaarufu zama hizi, ambapo watu wengi sana wanaifuatilia michezo.
Ni kwa sababu michezo inawapa watu ushindi feki, wanajiona wameshinda wakati siyo ushindi wao.

Pale ambapo timu ambayo mtu anashabikia inashinda, mtu huyo anaona amepata ushindi.
Atatumia nguvu kubwa kusherekea ushindi wa timu yake, kwa sababu tu hana ushindi wa kusherekea kwenye maisha yake.

Tunaona pia wanaowapa watu ushindi huu feki wanapata wanachotaka.
Vyombo vya habari vimekuwa na vipindi vingi vya michezo.
Kumekuwa na wachambuzi wengi wa michezo.
Na hata michezo mingi ya kubahatisha imewekwa kwenye michezo.

Wote walio nyuma ya hiyo michezo wananufaika sana, kwa kuwapa watu ushindi feki.

Sasa hebu pata picha utanufaika kiasi gani kama utawapa watu ushindi halisi.
Lazima watakuwa tayari kukupa kila unachotaka.

Na ushindi halisi namba moja kwa wengi ni kwenye eneo la fedha.
Ndiyo unataka fedha, lakini lazima kwanza uwasaidie watu wengi zaidi kupata fedha nyingi kadiri wanavyotaka.

Kwa kila unachofanya, jiulize kinawasaidiaje watu kupata ushindi kwenye fedha.
Je kinawawezesha watu kuongeza kipato chao au kinawasaidia kupunguza gharama?

Ni lazima uguse eneo moja au yote mawili kama unataka kuwavuta watu kuja kwako na kukupa unachotaka.

Watu wanahangaika na ushindi wa michezo kwa sababu hawana ushindi wa kutosha kwenye maisha yao.
Wawezeshe watu kupata ushindi halisi kwenye maisha yao na wao watakuwezesha kupata ushindi mkubwa unaoutaka kwenye maisha yako.

Hii pia inaenda kwa watu tunaofanya nao kazi, yaani wafanyakazi tunaowaajiri. Kama tunataka wafanye kile tunachowataka wafanye, tuwape ushindi.
Kwa majukumu tunayowapa wafanye, tuweke vigezo ambavyo wakifikia wanakuwa wamepata ushindi.
Hilo litawasukuma kufikia vigezo hivyo na kupata ushindi, kitu kitakachokupa yale unayotaka.

Kwa maana hiyo basi, watu hatari na wa kuwaepuka sana kwenye maisha yako ni watu ambao hakuna ushindi wanaoutafuta.
Hawa ni watu ambao hawawezi kukupa ushindi unaoutaka hata uwafanye nini
Utahangaika nao sana, lakini wataishia kukuangusha.

Tumia njaa ya ushindi kama mchujo wa watu utakaojihusisha nao.
Jihusishe na wale tu ambao wana kiu kubwa ya ushindi kwenye maisha yao.
Ona jinsi utakavyoweza kuwasaidia kupata ushindi mkubwa kwenye maisha yao ili na wao wakuwezeshe wewe kupata ushindi mkubwa kwenye maisha yako.

Usipoteze muda na nguvu zako kwa watu wasio sahihi.
Unataka ushindi, ambatana na wanaotaka ushindi pia.
Wawezeshe kupata ushindi ili nao wakuwezeshe kupata ushindi pia.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe