3040; Raha ya mchezo.

Rafiki yangu mpendwa,
Watu wengi huwa wanapenda kufuatilia michezo mbalimbali.
Japokuwa hakuna mtu anapenda kuona timu anayoshabikia ikifungwa, kama timu hiyo inaweza kushinda mara zote bila ya kusumbuka, mchezo hauwi na raha ya kuangalia.

Kadhalika sinema na maigizo mbalimbali.
Kama mhusika mkuu hakutani na changamoto mbalimbali kwenye safari yake, hainogi kuangalia.

Raha ya michezo mbalimbali ni ugumu ambao wachezaji wanakutana nao, uwezekano wa wao kushindwa.
Huo ndiyo unawasukuma kuweka juhudi zaidi ili kupata ushindi mkubwa.

Mchezo ukiwa rahisi sana watu hawafurahii kuuangalia, kwa sababu wanajua ushindi ni uhakika.
Na pia mchezo ukiwa mgumu sana watu wanakata tamaa kuuangalia, kwa sababu wanajua hakuna namna ya kushinda.

Hivyo raha kuu ya mchezo wowote ule ipo kwenye ugumu ambao upo ndani ya uwezo wa mku kuukabili.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye maisha yetu na mambo mengine yote tunayoyafanya.
Yakiwa rahisi sana yanatuchosha kufanya, maana hatupati msukumo wowote.
Na yakiwa magumu sana yanatukatisha tamaa, kwa kuwa tunaona hayawezekani kabisa.

Tunachohitaji ili kupambana na kujituma ni kiwango cha ugumu ambacho tukiweka juhudi tunaweza kupata matokeo ya tofauti.
Siyo rahisi sana kuwa na uhakika wa ushindi mara zote.
Na wala siyo ngumu sana kukosa kabisa tumaini lolote lile la ushindi.

Kwa upande mmoja tusikimbilie mambo rahisi tukidhani maisha yetu ndiyo yatakuwa ya raha.
Yatatuchosha haraka na kukosa maana.
Lakini pia tusijidanganye na mambo magumu sana ambayo hayawezi hata kufikiria, yatatukatisha tamaa.

Tuchague mambo yanayotusukuma kuwa bora kwa sababu ya nafasi iliyopo kwenye kushindwa, kisha tujisukume kuwa bora zaidi kwenye kuyafanya.
Na hata kama tunayopanga kufanya ni magumu sana, ili tusikate tamaa tuyagawe kwenye ngazi ambazo tunaweza kuzifikia.
Kwa kifikia ngazi kwa ngazi inakuwa rahisi kufikia chochote kigumu kabisa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe