Habari njema mstoa wa zama hizi,

Kuna wakati tunajipa kazi ambayo siyo yetu. Kazi ya kuwa kiranja wa dunia ambayo hata hatuiwezi. Kuwa kiranja wa dunia ni pale unapotaka mambo yaende au yatokee kama vile unavyotaka wewe.

Kwenye falsafa ya ustoa, tuna dhana moja ambayo inaitwa amori fati ikiwa na maana kwamba, ipende hatima yako yaani love your fate.

Maana kubwa ya dhana hii kwenye falsafa ya ustoa ni kwamba wastoa waliamini tunapaswa kupokea kila kitu kinachotokea kama vile tulitaka kitokee.

Hii ina maana kwamba, chochote kile kinachotokea, kwanza unakipokea na kukikubali kisha unachukua hatua kuhakikisha kinakuwa na manufaa kwako.

Kukataa kupokea na kukubali mambo kama vile yalivyotokea huko ndiyo kutaka kuwa kiranja wa dunia. Unataka mambo yaende kama vile unavyotaka wewe.

Kwenye falsafa ya ustoa kuna upacha wa kila kitu, kama kuna mazuri basi unapaswa kujua kuwa kuna mabaya pia. Pale leo unapopitia mazuri jua kwamba kuna siku utakuja kupitia na mabaya.

Kupenda hatima yako ni kukubaliana na yote ambayo asili imeamua juu yako na wala siyo kulalamika.

Kulalamika kwa chochote kile kinachotokea ni kujidanganya kwa sababu wewe siyo kiranja wa dunia, wewe siye unayepanga nini kitokee na nini kisitokee.

Kwa nini falsafa ya ustoa inatufundisha hili?

Msingi mkuu wa Ustoa kwenye hili ni kuacha vitu vitokee kama vinavyotokea na siyo kutamani vingetokea kwa matakwa yetu au kwa namna fulani.

Wajibu wako ni kutumia kila kinachotokea kwa namna ambayo kitakuwa na manufaa kwako na siyo kulalamika.

Hatua ya kuchukua hapa;

Kila tulichonacho ni zawadi kutoka kwenye asili na tumekopeshwa tu.

Itafikia kipindi ambapo tutahitajika kurudisha zawadi au mkopo huo.

Kama unavyojua ukichukua mkopo unapaswa kurudisha kwa wenyewe muda wa kurudisha ukifika.

Hatupaswi kulalamika, bali kushukuru kwa wakati wote ambao tumekuwa na kitu hicho.

Kwa maana hiyo, kulalamika ni kukosa shukrani kwa yale mazuri ambayo asili imekupa na ukanufaika nayo.

Kitu kimoja zaidi, kamwe usiwe mtu wa kulalamika, usiwe kiranja wa dunia, huko ni kukosa shukrani kwa mengi mazuri ambayo umekuwa nayo kwenye maisha yako.

Asili imetukopesha vile tulivyonavyo, tuvitumie vizuri sana na kunufaika navyo hata siku vikiondoka tunapaswa kushukuru kwa muda ambao asili umetupa nafasi ya kuwa na vile tulivyonavyo.

Rafiki na Mstoa mwenzako

Mstoa Mwl Deogratius Kessy