Kwenye safari ya mafanikio, bahati huwa ina nafasi yake. Kuna wakati watu huwa wanakutana na fursa fulani ambazo zinawanufaisha sana, siyo kwa sababu ya kitu chochote cha tofauti ambacho wamefanya. Bali wanakuwa wamekutana na bahati fulani.

Lakini sasa, bahati haijawahi kumfuata mtu aliyelala au ambaye hafanyi kile ambacho alipaswa kufanya. Bahati huwa inaenda kwa yule ambaye yupo kwenye mchakato wa kufanya. Hata kama ni kuokota fedha, ataokota yule ambaye anatembea na siyo aliyelala.

Japokuwa bahati siyo mkakati wa mafanikio, lakini lazima kwenye safari yako ya mafanikio utengeneze nafasi za kunufaika na bahati. Hutaiweka bahati kwenye mipango yako, lakini kwa namna unavyofanya mambo yako, unakuwa umejiweka kwenye nafasi nzuri ya kunufaika na bahati pale inapotokea.

Kitu kikubwa unachopaswa kufanya ili uweze kuivuta bahati kuja kwako ni USIFE. Ninaposema usife maana yake ni uendelee kufanya kile unachofanya kwa muda mrefu zaidi. Kadiri unavyodumu kwenye kitu kwa muda mrefu bila kuacha, ndivyo unavyojiweka kwenye nafasi ya kunufaika na bahati zinazoweza kujitokeza.

Kwenye safari ya mafanikio, watu wengi sana wamekata tamaa na kuacha wakiwa wamekaribia kabisa kupata walichotaka. Ni vile watu huwa hatujui wakati wa kupata, lakini kwa wengi, pale wanapokata tamaa ndiyo wanakuwa wameyakaribia zaidi mafanikio yao.

Hivyo wajibu wako ni kuhakikisha unaendelea na mapambano bila ya kukata tamaa. Pale unapofikia hali ya kukata tamaa, jiambie upo karibu sana na ushindi na umeshapambana sana huwezi kuishia hapo. Inuka na uendelee na mapambano, kwa sababu ukiishia hapo unakuwa umepoteza juhudi zote ulizoweka.

Juhudi unazoweka kwenye safari yako ya mafanikio ni sana wa kupampu maji kwenye kisima. Unaweza kupampu kwa muda na usione maji yakitoka. Ukichoka na kusema humu hakuna maji, hata yale ambayo yalikuwa yameanza kupanda yanarudi chini yote. Unachotakiwa kufanya ni kuendelea kuyapampu maji bila kuacha, mpaka pale yatakapotoka.

SOMA; 3117; Usife.

Ili udumu kwenye kile unachofanya kwa muda mrefu, lazima uwe na mpango mzuri ambao utakupa nafasi ya kuendelea kufanya.

Kwanza kabisa lazima uziepuke hatari ambazo zinaweza kukuondoa kwenye mchezo haraka sana. Kuna fursa zinaweza kujitokeza na ukaziona ni nzuri, lakini ukizifanyia kazi unaharibu hata kile ambacho ulishajenga. Hivyo unapaswa kuchunguza vizuri kila kitu kabla ya kufanya.

Pili unapaswa kupangilia vizuri rasilimali zako ili uweze kudumu kwa muda mrefu. Afya yako ni muhimu uitunze ili uweze kuendelea kufanya kwa muda mrefu. Ukikosa afya, utashindwa kuendelea na ufanyaji kwa muda mrefu.

Lakini pia unapaswa kuendelea kujikumbusha kusudi lako na kwa nini inayokusukuma kufanya unachofanya. Kila unapokaribia kukata tamaa unajikumbusha hilo. Jikumbushe ile picha kubwa uliyonayo ya matokeo unayotegemea kupata ili upate nguvu ya kuendelea na safari bila kukata tamaa.

Kukaa kwenye safari kwa muda mrefu bila kuishia njiani haimaanishi unarudia kufanya kitu kile kile hata kama hakifanyi kazi. Bali inamaanisha unaendelea na maono na malengo uliyonayo, lakini mipango na mikakati ya kufikia malengo hayo inabadilika kulingana na matokeo unayoyapata.

Kwa chochote unachotaka, mwanzo unaweza kudhani njia fulani itakupatia. Unapotumia njia hiyo unakutana na vikwazo ambavyo vinafanya safari ionekane kama haiwezekani. Badala ya kuendelea kubamiza kichwa kwenye vikwazo hivyo na kuumia, unapaswa uangalie namna ya kuvuka vikwazo hivyo au kupita njia nyingine.

Lengo lako linabaki kuwa lile lile na mapambano yanaendelea bila kukwama, lakini njia ndiyo zinabadilika kulingana na matokeo unayokuwa umeyapata. Ili uweze kubadili njia, lazima uwe unajifanyia tathmini za mara kwa mara kwenye kila hatua unayochukua. Ni tathmini hizo ndiyo zinakuonyesha nini kinafanya kazi na nini hakifanyi kazi ili kiboreshwe zaidi.

Kadiri unavyodumu kwenye kitu chochote kwa muda mrefu zaidi, ndivyo unavyojiongezea nafasi ya kupata mafanikio makubwa kupitia kitu hicho. Lakini ili hilo litokee, lazima uendelee kuwa bora kwenye hicho unachofanya kadiri muda unavyokwenda. Huwezi kuwa unarudia kufanya kitu kile kile kwa namna ile ile kwa muda mrefu na kutegemea matokeo ya tofauti.

Jiambie wewe ni mwenye bahati, kwa sababu ukishachagua kile unachotaka, unang’ang’ana nacho mpaka ukipate. Huruhusu kitu chochote kiwe kikwazo kwako kupata kile unachotaka. Unajipanga kuhakikisha unaendelea kubaki kwenye mwendo kwa muda mrefu zaidi. Nenda hivi na mafanikio makubwa yatakuwa yako kwa uhakika.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.